Sunday, August 26, 2012

VYOMBA VYA HABARI VYATAKIWA KUENDELEA KUHAMASISHA SENSA

Vyombo vya habari Mkoani Iringa vimeshauriwa kuendelea kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili liweze kufanikiwa katika Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma muda mfupi baada ya kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililoanza usiku wa Kuamkia leo nchini kote.
Dkt. Christine amesema kuwa zoezi hilo vimeanza vizuri na mdadisi ameonekana kubobea katika kazi hiyo. Aidha, amewamwagia sifa wakufunzi na wadadasi kwa jinsi walivyoonesha juhudi katika kufundisha na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu uelewa wa zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi.
 Dr. Christine Gabriel Ishengoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Sensa ya Mkoa amevipongeza vyombo vya habari vya Mkoa wa Iringa kwa weledi katika kuhamasisha zoezi hili. Amesema uhamasishaji ni muhimu sana katika kutoa hamasa kwa kazi ya Sensa ili asitokee mtu ambaye atakuwa hakupata taarifa na elimu juu ya umuhimu wa Sensa na kuhesabiwa. Aidha, ametoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea na uhamasishaji huo kwa kipindi cha wiki nzima ili kulifanikisha zoezi hili katika Mkoa wa Iringa. “kufanikiwa kwa zoezi hili Mkoani Iringa sit u kutakuwa na manufaa kwa Mkoa wetu, bali kwa nchi nzima na jambo hili litafikiwa pale tu wananchi wote watakapokuwa wameelewa umuhimu wa zoezi hili na kushiriki katika kulifanikisha” alisisitiza Dkt. Christine.

Akiongelea matukio yasiyo ya kawaida katika zoezi hili, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi hilo limeanza katika hali ya utulivu mkubwa na hakuna tukio lolote lisilo la kawaida lililotokea na kuripotiwa. Aidha, amewata wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa pindi watakapopita katika maeneo yao na kujibu kwa usahihi maswali watakayokuwa wakiulizwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka, akitoa maoni yake baada ya kuhesabiwa asubuhi ya leo amesema kuwa kazi ya kuhesabu na kuhesabiwa ni jukumu la kila mtanzania pasipo kujali mipaka ya aina yoyote. Amesema kila mtanzania anayo haki ya kuhesabiwa katika Sensa hii ili kuhakikisha Serikali yake inapata taarifa sahihi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake.
Mpaka amesema “miongoni mwa michango ya wananchi katika jitihada za kujiletea maendelea kwa kushirikiana na Serikali yao ni pamoja na kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu”. Amesema zipo njia mbalimbali za kushiriki katika shughuli za maendeleo katika kipindi hiki kutoa taarifa sahihi ni jukumu namba moja ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi. 

Sensa ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini ikiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa’ ipo katika siku yake ya kwanza nchini kote na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa mara moja tu.
=30=

SENSA YAANZA VIZURI MUFINDI

Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Wilayani Mufindi limeanza kwa hali ya utulivu mkubwa na wananchi wameendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Akiongea katika mahojiano maalumu na na gazeti la Uhuru, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amesema kuwa katika siku ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi Wilayani Mufindi, “kwa kweli zoezi hili lilianza saa sita kamili usiku katika maeneo ambayo si ya makazi ya kudumu, kazi ilifanyika katika Mji wa Mafinga katika maeneo ya stendi, nyumba za kulala wageni na maeneo yanapopaki magari makubwa ya mizigo. Aidha, zoezi kama hilo lilifanyika pia katika maeneo ya Nyololo, Igowole, Kibao, Malangali, Ihowanza, Mgololo na Usokami hadi asubuhi saa kumi na moja kazi hiyo ilikuwa imekamilika kwa mafanikio makubwa”. Amesema kuwa leo asubuhi pamoja na kuanza zoezi kwenye makazi ya watu, wagonjwa waliolazwa kwenye vituo vyote vya huduma wamehesabiwa asubuhi na zoezi linaendelea kwenye makazi ya kudumu ya watu.

Akiongelea tathmini yake, amesema kuwa kazi ya kuhesabu watu inaendelea vizuri sana na muitikio wa watu ni mkubwa sana katika zoezi hilo. Amesema ukubwa wa muitikio wa watu katika wilaya yake unatokana uhamasishaji mkubwa unaoendelea kufanyika na kiu kubwa waliyonayo wananchi ya kushirikiana na Serikali katika kujiletea maendeleo.

Evarista ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amesema kuwa ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kwa asilimia 100, viongozi na jamii kwa ujumla hawana budi kuendelea kutoa hamasa na elimu ili wananchi wote waweze kushiriki kikamilifu katika upatikanaji wa takwimu hizo muhimu kwa mustakabali wa taifa. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa wanaoendelea kupita katika kaya zao kukusanya taarifa mbalimbali. Amesema wananchi watakapo jibu kwa usahihi maswali watakayoulizwa na makarani wa Sensa watakuwa wametimiza wajibu wao wa kushiriki katika kupanga mipango ya maendeleo yao kwa namna moja ama nyingine.

Katika mahojiano kwa njia ya simu na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Iringa, Fabian Fundi amesema, “kwa ujumla zoezi hili linaenda vizuri na tulianza saa sita usiku na kuendelea nalo hadi alfajiri. Na asubuhi hii tumeanza kuhesabu kaya binafsi ambazo ni makazi ya kudumu ya watu”. Amesema kuwa kamati ya Sensa Mkoa haijapata taarifa wala matukio yasiyo ya kawaida wala kupokea simu yoyote kutoka kwa makarani kutaarifu kuwa kuna mtu au kaya iliyogoma kuhesabiwa, hii ni dalili nzuri kuwa zoezi hili litakuwa la mafanikio katika Mkoa wa Iringa.

Sensa ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini kote ikiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo: Jiandae kuhesabiwa’ ipo katika siku yake ya kwanza na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa mara moja tu.
=30=

VYOMBO VYA HABARI IRINGA VYATAKIWA KUENDELEA KUHAMASISHA SENSA

Vyombo vya habari Mkoani Iringa vimeshauriwa kuendelea kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili liweze kufanikiwa katika Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma muda mfupi baada ya kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililoanza usiku wa Kuamkia leo nchini kote.
Dkt. Christine amesema kuwa zoezi hilo vimeanza vizuri na mdadisi ameonekana kubobea katika kazi hiyo. Aidha, amewamwagia sifa wakufunzi na wadadasi kwa jinsi walivyoonesha juhudi katika kufundisha na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu uelewa wa zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Sensa ya Mkoa amevipongeza vyombo vya habari vya Mkoa wa Iringa kwa weledi katika kuhamasisha zoezi hili. Amesema uhamasishaji ni muhimu sana katika kutoa hamasa kwa kazi ya Sensa ili asitokee mtu ambaye atakuwa hakupata taarifa na elimu juu ya umuhimu wa Sensa na kuhesabiwa. Aidha, ametoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea na uhamasishaji huo kwa kipindi cha wiki nzima ili kulifanikisha zoezi hili katika Mkoa wa Iringa. “kufanikiwa kwa zoezi hili Mkoani Iringa sit u kutakuwa na manufaa kwa Mkoa wetu, bali kwa nchi nzima na jambo hili litafikiwa pale tu wananchi wote watakapokuwa wameelewa umuhimu wa zoezi hili na kushiriki katika kulifanikisha” alisisitiza Dkt. Christine.

Akiongelea matukio yasiyo ya kawaida katika zoezi hili, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi hilo limeanza katika hali ya utulivu mkubwa na hakuna tukio lolote lisilo la kawaida lililotokea na kuripotiwa. Aidha, amewata wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa pindi watakapopita katika maeneo yao na kujibu kwa usahihi maswali watakayokuwa wakiulizwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka, akitoa maoni yake baada ya kuhesabiwa asubuhi ya leo amesema kuwa kazi ya kuhesabu na kuhesabiwa ni jukumu la kila mtanzania pasipo kujali mipaka ya aina yoyote. Amesema kila mtanzania anayo haki ya kuhesabiwa katika Sensa hii ili kuhakikisha Serikali yake inapata taarifa sahihi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake.
Mpaka amesema “miongoni mwa michango ya wananchi katika jitihada za kujiletea maendelea kwa kushirikiana na Serikali yao ni pamoja na kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu”. Amesema zipo njia mbalimbali za kushiriki katika shughuli za maendeleo katika kipindi hiki kutoa taarifa sahihi ni jukumu namba moja ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi. 

Sensa ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini ikiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa’ ipo katika siku yake ya kwanza nchini kote na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa mara moja tu.
=30=

Wednesday, August 22, 2012

...AMIA HUKU DIGITALI

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa elimu kwa umma ni nyenzo muhimu sana katika kuwaandaa wananchi kuhama kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analojia na kuingia katika mfumo wa digitali.

Ameyasema hayo katika mkutano wa viongozi wa mkoa wa Iringa kuhusiana na mabadiliko ya mfumo wa utangazaji kutoka analojia kwenda digitali uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu Huria, tawi la Iringa.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa akisoma hotuba yake

Picha ya Pamoja ya washiriki wa Warsha hiyo

Amesema katika kufanikisha jitihada hizo, “umeonekana umuhimu wa kuelimisha umma kwa kushirikisha wizara, idara za Serikali pamoja na wananchi wote ili kuweza kufanikisha mabadiliko haya kwa ufanisi bila kuathiri upatikanaji wa huduma za utangazaji nchini”. Ameishauri kamati maalumu ya kitaifa inayofanya kazi ya kuwaelimisha wananchi nchini juu ya mabadiliko ya teknolojia ya utangazaji kuhakikisha wananchi wengi wanapata elimu hiyo ili kuwaandaa na mabadiliko hayo. Amesema maana ya mabadiliko ya teknolojia, matarajio ya baada ya mabadiliko na wajibu wa mwananchi katika kufanikisha mabadiliko hayo ni mambo ya muhimu kutiliwa mkazo katika utoaji wa elimu kwa wananchi.

Akiongelea Sensa ya Watu na Makazi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ametoa wito kwa washiriki hao kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi. Amesema “natoa wito kwenu washiriki wa mkutano huu hasa waandishi wa habari kutumia nafasi hii kuhimiza jambo hili na kutumia muda wenu na vyombo vyenu kuwaelimisha wananchi ili waweze kushiriki katika zoezi hili na kulifanya liwe la manufaa na kuleta tija katika Mkoa wetu wa Iringa na Taifa kwa ujumla” alisisitiza Dkt Christine.
=30=

WAZAZI WASHAURIWA KUSHIRIKI KATIKA MALEZI YA WATOTO

Wazazi wameshauriwa kutoa ushirikiano kwa walimu katika malezi ya wanafunzi ili kuhakikisha jamii inakuwa na watu wenye nidhamu na maadili mema. 

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alikokuwa akiongea na wananchi, walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Ilambilole iliyopo katika Kata ya Nduli, Wilayani Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa suala la nidhamu kwa wanafunzi haliishii shuleni pekee bali ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha inawasaidia walimu katika malezi ya wanafunzi. Amesema “nidhamu inaanzia nyumbani hivyo lazima tusaidiane na walimu katika kudumisha nidhamu ya watoto wetu, lakini tukiwaachia walimu peke yao hatuwezi kufanikiwa. Walimu wana nafasi yao katika kukuza na kudumisha nidhamu na wazazi pia wana nafasi yao katika hili”.

Akiongelea changamoto ya upungufu wa walimu wanaofundisha masomo ya sayansi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa upungufu huo upo kwa sababu wanafunzi wengi hawataki kusoma masomo ya sayansi. “Tunaupungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwa sababu watoto wetu hawasomi masomo ya sayansi” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Katika kukabiliana na hali hiyo, alishauri wanafunzi wahamasishwe kusoma masomo ya sayansi ili kuweza kuziba pengo hilo. Aidha, alisema kuwa Serikali inaendelea na mipango ya muda mrefu ya kuhakikisha changamoto hiyo inabaki historia.   

Akiwasilisha taarifa ya shule ya Sekondari ya Ilambilole, Mkuu wa shule hiyo, Vicent Ngaya amesema kuwa shule yake inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba za walimu na walimu wa masomo ya sayansi. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni kukosekana kwa mabweni hasa kwa wanafunzi wa kike na umbali wa makazi ya walimu kutoka shuleni jambo linalosababisha kuchelewa kufika shuleni na kufika wakiwa wamechoka sana.
Kuhusu ufauli, Ngaya amesema kuwa shule imepata mafanikio makubwa katika ufaulu wa wanafunzi, ambapo kwa mwaka 2010 ufaulu ulikuwa ni asilimia 78 na mwaka 2011 ufaulu ulikuwa ni asilimia 61.

Wakati huohuo, suala la wivu limeelezwa kuwa halina nafasi katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti, mwaka huu. Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Msaidizi wa Sensa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga wakati akifafanua masuala mbalimbali ya Sensa katika Kijiji cha Ikengeza, Wilaya ya Iringa. Millinga amewataka akina baba kutokuwa na dhana ya wivu wa aina yoyote pindi wake zao watakapokuwa wakihojiwa na makarani wa Sensa kwa sababu baadhi ya maswali yatawahusu akina mama pekee. Amesema maswali hayo hayatahusiana na ndoa bali ni masuala ya uzazi na kuwataka kuwapatia uhuru na nafasi pindi watakapokuwa wanahojiwa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi.

Millinga amesema kuwa Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu sana kwa nchi kwa sababu pasipo kufahamu idadi sahihi ya watu inawezekana wananchi kupewa huduma pungufu ya mahitaj yao. Amesema Sensa hiyo itawahusisha watanzania wote na wageni watakaokuwa ndani ya nchi siku hiyo ya Sensa.
=30=