Saturday, October 24, 2015

KUELEKEA SIKU YA KUPIGA KURA MKOANI IRINGA


Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mhe. Amina Masenza



"Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuwalinda wananchi wote, hivyo, rai yangu kwa Wananchi ni kuwa jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura mapema na baada ya kupiga kura rudini kwenye maeneo yenu kuendelea na shughuli nyingine. Wananchi wasibaki kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura'

Tuesday, October 20, 2015

MATUKIO WAKATI WA KUAPISHWA MKUU WA WILAYA MTEULE YA IRINGA RICHARD KASESELAm

Mhe. Richard Kasesela akisaini kitabu cha wageni

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa

Mkuu wa Utawala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Scolastica Mlawi (kulia)

Mhe. Richard Kasesela akiapa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Amina Masenza (kulia) akimkabidhi Katiba ya Jamhurir ya Muungano wa Tanzania Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu (kushoto)

DC IRINGA SIMAMIA ULINZI NA USALAMA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela ametakiwa kusimamia ulinzi na usalama katika wilaya ya Iringa ili mkoa uwe salama katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza muda mfupi baada ya kumuapisha mkuu wa wilaya mteule wa Iringa katika ofisi ya mkuu wa mkoa leo.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa Amina Masenza
Masenza alisema “suala la ulinzi na usalama ni muhimu sana katika wilaya ya Iringa ili mkoa uwe salama. Hivyo, lazima ulisimamie ipasavyo. Binafsi nina imani na wewe na utendaji wako wa kazi hivyo hautashindwa katika kutekeleza majukumu yako”. Alisema kuwa wilaya ya Iringa ikiwa salama wananchi wataendelea kushiriki katika mampeni za kisiasa kwa uhuru na amani na hatimae kupiga kura salama.

Mkuu wa mkoa alimtaarifu masuala ya kipaumbele kwa mkoa wa Iringa kuwa ni lishe, ukimwi na usafi wa mazingira. Alimtaarifu kuwa katika ratiba yake ya kazi lazima ijikite katika utekelezaji wa mpango mkakati wa mkoa unaolenga kukabiliana na changamoto za lishe, hali ya maambukizi ya ukimwi na usafi wa mazingira.

Katika salamu za mkuu wa wilaya ya Iringa mteule Richard Kasesela alimshukuru Rais wa Jamhuri kwa imani aliyonayo kwake. Aidha, alisema kuwa katika kipindi hiki suala la amani ni agenda yake ya mwanzo kuelekea uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015. Alisema kuwa yeyote katika wilaya ya Iringa atakayetishia watu kwenda kupiga kura hasa wanawake atashughulikiwa. Alisema kuwa lazima wananchi wote katika wilaya ya Iringa washiriki katika zoezi la kupiga kura kikamilifu pasipo woga ili wafurahie haki yao ya kupiga kura kikatiba.

Akiongelea masuala ya kimkakati katika mkoa, mkuu wa wilaya mteule alisema “nitajitahidi kuhakikisha suala la lishe bora kwa wananchi hasa wanawake wajawazito na watoto wachanga linaboreka katika wilaya ya Iringa na mkoa kwa ujumla. Tatizo hili lazima liishe”.
 
Mkuu wa wilaya ya Iringa, Mhe. Richard Kasesela
Aidha, suala la ukimwi aliahidi kukabiliana nalo ipasavyo. Alisema kuwa ngono zembe ni jambo linalohitaji kuangaliwa kwa umakini zaidi. Wilaya itaangalia upya viashiria vya ukimwi na mitego ili kuangalia jinsi ya kuitegua mitego hiyo hatimae kupunguza maambukizi mapya. Akiongelea usafi wa mazingira alisema “mtu ni afya hivyo usafi wa mazingira ni afya pia. Lazima usafi wa mazingira uanzie kwa mtu mwenyewe katika mazingira ya nyumbani kwake na mazingira yanayomzunguka”.

Mkuu wa wilaya ya Iringa aliapishwa leo mjini Iringa kufuatia uteuzi wa Rais wa wakuu wapya wa wilaya 13 na kuhamishwa kwa wakuu saba wa wilaya tarehe 4/10/2015.
=30=

NEC YAVITAKA VYAMA KUELIMISHA WANANCHI TARATIBU ZA UCHAGUZI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevitaka vyama vya siasa nchini kuwaelimisha wananchi kufuata taratibu ili kufanikisha uchaguzi huru na salama nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume hiyo Jaji Mary Longway alipokuwa akifungua mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa mkoani Iringa.
 
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Mstaafu) Mary Longway akifungua mkutano
Jaji Longway alisema “vyama vya siasa vina nafasi kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, Tume inaamini kwamba ili mpiga kura aweze kufanya maamuzi sahihi ni muhimu kwake kupata elimu sahihi. Hivyo basi, Tume inatarajia kuona mkitumia majukwaa yenu vema katika kuhamasisha na kuelimisha si tu wananchi wenu bali jamii ya watanzania”. 

Alisema kuwa kuelekea uchaguzi mkuu, Tume imeandaa vituo vya kupigia kura 64,736. Tanzania bara vituo 63,156 na Zanzibar vituo 1,580. Aliongeza kuwa kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wapiga kura 450 na wasizidi 500. “Hata hivyo kituo kinapokuwa na wapiga kura zaidi ya 500 kinabidi kigawanywe ili viwe viwili yaani kituo “A” na “B” na namba ya wapiga kura itakuwa nusu kwa nusu. Mnaombwa kuwahamasisha wapiga kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikishia kupiga kura siku nane kabla ya siku ya kupiga kura ili kuweza kujua vituo vyao halisi vya kupigia kura” alisisitiza Jaji Longway.

Kamishna Longway alisema kuwa Tume imekuwa ikisikitishwa na baadhi ya vyama vya siasa kutumia majukwaa vibaya wakati wa kampeni. “Tume kwa namna ya pekee inawaomba katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kutumia nafasi zenu majukwaani kuelezea sera za vyama vyenu ili kuweza kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi baada ya kuwa na taarifa sahihi”. 

Tume imekuwa ikisikia katika vyombo vya habari malalamiko juu ya uvunjifu wa maadili ya uchaguzi katika kipindi hiki cha kampeni, “nitumie nafasi hii kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa kupeleka malalamiko yenu katika kamati za maadili na si kukimbilia katika vyombo vya habarir kama ambavyo baadhi ya vyama vya siasa na wagombea mmekuwa mkifanya”.
Viongozi wa Vyama vya Siasa Mkoa wa Iringa

Ndani ya ukumbi wa Siasa ni Kilimo

Aidha, aliwataka kuepuka kutoa taarifa na shutuma zisizo sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kujikita katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa wafuasi na wananchi kwa ujumla na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba, 2015.
=30=

Friday, October 16, 2015

MATUKIO KATIKA PICHA YA PRESS CONFERENCE IRINGA











TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MWENENDO WA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI ILIYOTOLEWA NA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA AMINA MASENZA TAREHE 16/10/2015



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MWENENDO WA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI ILIYOTOLEWA NA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA AMINA MASENZA TAREHE 16/10/2015

1.0 Utangulizi
Mkoa wa Iringa unaendelea na maandalizi mbalimbali kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 25/10/2015. Maandalizi hayo ni pamoja na Wagombea kuendelea na kampeni kunadi sera zao, mafunzo kwa watendaji, maandalizi ya vituo vya kupigia kura, uhakiki wa taarifa zilizomo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na mapokezi ya vifaa.  
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza (kulia) na Katibu Tawala wa Mkoa Wamoja Ayubu
2.0 Hali ya Kampeni za Uchaguzi
Kampeni za uchaguzi zilianza rasmi tarehe 22/08/2015 na zitaendelea hadi tarehe 24/10/2015. Ratiba za kampeni zimeandaliwa na Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kwa kuvishirikisha vyama vya siasa. Kwa ujumla Kampeni hizo katika mkoa wa Iringa zinaendelea kwa hali ya amani na utulivu. 

3.0 Kamati za Maadili
Wasimamizi wote wa Uchaguzi wa Majimbo ya Uchaguzi wameunda Kamati za Maadili katika ngazi ya Jimbo. Kamati hizo pia zimeundwa katika ngazi ya Kata kwa Kata zote za Mkoa wa Iringa. Lengo la kuundwa kwa Kamati hizi ni kusimamia utekelezaji wa maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015.

4.0 Mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi
Mafunzo tayari yametolewa kwa Wasimamizi wa uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mafunzo hayo yalitolewa kwa Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi katika ngazi ya Jimbo. Aidha, Halmashauri zimeendesha mafunzo pia kwa Wasimamizi Wasaidizi ngazi ya Kata zote za Mkoa wa Iringa kuanzia tarehe 3/10/2015 hadi 13/10/2015. 

5.0 Utangazaji wa nafasi za Wasimamizi wa Vituo, Wasimamizi Wasaidizi  wa Vituo, na Makarani waongozaji  
Matangazo hayo yalitolewa katika Halmashauri zote 5 za Mkoa wa Iringa tarehe 1/10/2015 hadi 5/10/2015. Zoezi linaloendelea ni kufanya uchambuzi wa walioomba nafasi hizo ili kupata wenye sifa stahiki.

6.0 Vituo vya Kupigia Kura
Awali Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa orodha ya vituo 1,641 vitakavyotumika katika zoezi la upigaji kura kwa Mkoa wa Iringa kwa Halmashauri zote 5. Idadi hiyo imepungua kufikia vituo 1,601 baada ya uhakiki wa wapiga kura kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea kufanywa na Wasimamizi wa Uchaguzi.  

7.0 Mapokezi ya Vifaa
Halmashauri zimepokea vifaa kama masanduku, mifuniko, Tshirts, kofia, Vituturi, na fomu mbalimbali kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. 
Aidha, Wasimamizi wanaendelea kufanya tathmini ili kujiridhisha  endapo  vifaa vilivyopokelewa vinakidhi mahitaji.

8.0 Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Halmashauri zote.  Kazi inayoendelea hivi sasa ni uhakiki wa idadi ya wapiga kura kwa kila kituo.

9.0 Mambo Muhimu ya Kuzingatiwa na Wapiga Kura na Wananchi
(a)    Sifa za Mpiga Kura
  • Mpiga kura ni raia yeyote wa Tanzania,
  • Aliyefikisha umri wa miaka 18,
  • Aliyeandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,
  • Mwenye kadi ya kupigia kura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
  • Lazima awe Mkazi wa eneo analotaka kupiga kura na jina lake limeorodheshwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura au Orodha iliyobandikwa katika Kituo cha Kupigia Kura.
  • Orodha ya Wananchi wanaoshahili kupiga kura itabandikwa kwenye Vituo husika siku 8 kabla ya Uchaguzi hivyo wananchi wapitie Orodha hiyo mapema ili wajue vituo watakavyopigia kura.  
  • Vituo vyote vya kupigia kura havitawekwa katika nyumba za watu binafsi, vituo vidogo vya Polisi wala nyumba za Ibada kwa lengo la kuwapa nafasi na uhuru wapiga kura.
  • Katika zoezi la Kupiga Kura kipaumbele kitatolewa kwa watu wenye Ulemavu, Wanawake Wajawazito na wale wenye Watoto Wachanga, Wagonjwa na Wazee ili wasikae muda mrefu kwenye mistari.
  • Wapiga kura wasioweza kupiga kura wao wenyewe, wasioona au wasiojua kusoma watasaidiwa na watu watakao wateua wao wenyewe. Aidha, Tume imeandaa kifaa (Tactile Ballot Folder) kitakachowasaidia wapiga kura wasioona ili waweze kupiga kura zao wao wenyewe.
  • Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na vitafungwa saa 10.00 Jioni, iwapo kutakuwa na wapiga kura katika mistari muda huo, wapiga kura hao wataruhusiwa kupiga kura. Aidha, wapiga kura watakaofika baada ya muda huo hawataruhusiwa kupiga kura.
10.0 Makosa ya Uchaguzi (Makosa ya Jinai kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Sura 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura 292)
  • Kujaribu kupiga kura wakati muda wa kupiga kura umekwisha,
  • Kujaribu kupiga kura wakati hauruhusiwi kisheria kupiga kura,
  • Kujaribu kupiga kura zaidi ya mara katika uchaguzi,
  • Kujaribu kupiga kura kwa kutumia kadi ya mtu mwingine,
  • Kuweka kitu kingine zaidi ya karatasi ya kupigia kura katika sanduku la kuhifadhia kura.
  • Kuchana orodha ya wapiga kura au mabango yoyote ya elimu kwa mpiga kura.
  • Kughushi au kuharibu karatasi ya kura,
  • Kuchapisha na kusambaza karatasi za kura bila mamlaka kisheria,
  • Kupokea au kutoa rushwa kabla na wakati wa uchaguzi,
  • Kumzuia mtu kupiga kura yake kwa uhuru na amani,
  • Kutoa siri ya mpiga kura mwenzio kuwa anakwenda kumpigia kura Fulani au amempigia mtu Fulani.
  • Kuvaa au kuonesha alama yoyote ya chama wakati wa zoezi la upigaji kura.
  • Kuchukua kadi za Wapiga Kura ili wasiweze kupiga Kura.
  • Kutumia vitisho na nguvu kuwashawishi wapiga kura ili wakupigie kura.

11.0 Ulinzi na Usalama
Mkoa wa Iringa umejipanga vizuri kuhakikisha amani na usalama kwa kipindi chote cha kampeni za Uchaguzi na wakati wa zoezi la kupiga kura vyote vinafanyika vizuri kwa mujibu wa ratiba na kwa kuzingatia sheria za nchi ili Wananchi waendelee kuwa salama na kutekeleza majukumu yao.

Napenda kutoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kufahamu na kukubaliana kuwa yapo maisha na yataendelea kuwepo hata baada ya Uchaguzi Mkuu hapo tarehe 25 Oktoba, 2015. Hivyo, kila mmoja wetu lazima atimize wajibu wake katika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo katika kipindi hiki chote ili tumalize zoezi hili tukiwa wamoja na wenye mshikamano mkubwa.

Katika kuhakikisha mkoa unakuwa na utulivu kwa kipindi chote, nimekutana na makundi mbalimbali kujadili suala la amani kuelekea Uchaguzi Mkuu. Makundi hayo ni viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini, wazee na watu wenye ushawishi katika jamii na waandishi wa habari.
Lengo ni kupata maoni yao na ushauri wa jinsi ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwathibitishia Wananchi wa Mkoa wa Irirnga kuwa, ulinzi utakuwepo wa kutosha katika kipindi chote cha kampeni na siku ya kupiga kura tarehe 25/10/2015.

Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuwalinda wananchi wote, hivyo, rai yangu kwa Wananchi ni kuwa jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura mapema na baada ya kupiga kura rudini kwenye maeneo yenu kuendelea na shughuli nyingine. Wananchi wasibaki kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura.
Asanteni kwa kunisikiliza