Wednesday, May 16, 2018

IRINGA YATEKELEZA AGIZO LA SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKA


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa unatekeleza agizo la serikali ya awamu ya tano la kuufanya ushirika kuwa nguzo ya kuwasaidia wakulima.

Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Mrajis msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Iringa, Robert George alipokuwa akisoma taarifa ya hali ya ushirika katika mkoa wa Iringa katika jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa lililofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa hivi karibuni.
Kaimu Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Iringa, Robert George

George alisema kuwa mkoa unaendelea kutekeleza agizo la serikali la kujenga ushirika imara unaomsaidia mkulima. 

“Katika kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa imara na kuongeza idadi ya wanachama kama lilivyo agizo la Serikali ya awamu ya tano ambalo linatuhitaji sisi kama wasimamizi wa ushirika kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa ndio nguzo ya kumsaidia mkulima. Kwa mwaka 2017/2018 jumla ya vyama vya ushirika 8 vimeandikishwa zikiwepo SACCOS 5 na AMCOS 3” alisema George.

Uhamasishaji wa vyama vilivyosinzia ili viweze kuamka umefanyika kupitia chama kikuu cha ushirika na maafisa ushirika, jumla ya vyama vya ushirika vitano vimeamka ambavyo ni Magulilwa AMCOS Ltd, Ipilimo AMCOS Ltd, Matanana AMCOS Ltd, MVIKIMA SACCOS Ltd na Ikimo AMCOS Ltd.

Akiongelea utekelezaji wa maagizo ya serikali kuhusu mazao ya kimkakati, Mrajis msaidizi mkoa wa Iringa alisema kuwa halmashauri zimehamasisha kilimo cha mazao ya korosho na pamba katika kata za Nzihi na Malengamakali kupitia vyama vya ushirika vya Nzihi mixed na Usolanga.

Aliongeza kuwa mkoa unaendelea kusimamia na kuviimarisha vyama vya ushirika vitatu vinavyojishughulisha na kilimo cha chai. Vyama hivyo alivitaja kuwa ni Mkonge Amcos, Sawala Amcos na Luhunga Amcos. 

Kwa mwaka 2017/2018 jumla ya vijiji vitano vimehamasishwa kuanzisha vyama vya ushirika vya kilimo cha chai katika halmashauri ya Mufindi. Vijiji hivyo ni Igoda, Kibao, Udumka, Mninga na Makalala” alisema George.

Halmashauri zinaendelea kuhamasisha kilimo cha kahawa, korosho na pamba aliongeza. “Kwa msimu huu wa mwaka 2017/2018 wakulima wa halmashauri wilaya ya Iringa wamepanda karosho kwa wingi hivyo, kwa maeneo yote yaliooteshwa korosho uhamasishaji wa kuanzisha vyama vya ushirika utafanyika katika msimu wa 2018/2019. Kutokana na jiografia ya maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wetu mazao yote ya kimkakati yanaweza yakastawishwa na wanachama wa vyama vya ushirika” alisema George.

Jukwaa la ushirika ni jukwaa la pili kufanyika ngazi ya mkoa, likishirikisha Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, wadau wa taasisi za kifedha na wanaushirika.
=30=

WANAUSHIRIKA IRINGA WATAKIWA KULIPA MADENI


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wanaushirika mkoani Iringa wametakiwa kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka riba kubwa inayotokana na kuchelewa kulipa mkopo kutoka taasisi za kifedha.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Masenza alisema kuwa wanaushirika wamenufaika na mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali mkoani Iringa. Alisema kuwa pamoja na manufaa hayo, changamoto kubwa imebaki kurejesha mikopo hiyo kwa wakati. Aliwaasa wanaushirika kulipa kwa muda mikopo wanayokopeshwa. 

Nawaasa wanaushirika wenye mikopo kulipa madeni yao kwa wakati ili kuepukana na riba inayoendela kupanda. Tukifanya hivyo tutasaidia kujua hali ya uzalishaji hivyo kuvutia wanunuzi wengi zaidi katika Mkoa wetu” alisema Masenza.

Akiongelea sekta ya ushirika katika maendeleo ya wananchi, mkuu wa mkoa alisema kuwa ushirika ni nguzo muhimu katika kuwasaidia wananchi kupata huduma za ushirika kwa urahisi na gharama nafuu. 

Mwaka huu vyama vya ushirika vya kilimo sita vimepata mikopo ya pembejeo toka benki ya maendeleo ya kilimo wenye thamani ya Tsh. 277,905,600/= kwa lengo la kuendeleza Kilimo kwenye maeneo yao kupitia udhamini wa chama kikuu cha ushirika -IFCU (1993) LTD. Napenda kutoa wito kwa vyama hivyo vilivyopata mikopo ya kilimo kukusanya mazao yao kwa pamoja katika maghala ili waweze kuuza kwa pamoja na kupata soko zuri” alisema Masenza.

Jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa ni la pili na lilihudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za fedha na wanaushirika.
=30=



IRINGA KUENDELEZA MAZAO YA BIASHARA


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa unaendelea kuweka mikakati ya kuendeleza mazao ya korosho, pamba na kahawai ili yachangie katika kukuza uchumi wa wakulima na mkoa kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa kililofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo hivi karibuni.

Masenza alisema kuwa serikali inatambua mazao matano ya kimkakati na kuyataja kuwa ni korosho, kahawa, tumbaku, pamba na chai. 

Mkoa wetu wa Iringa una hali ya hewa nzuri inayofaa kwa kilimo cha mazao yote. Kumekuwa na maendeleo mazuri katika kilimo cha chai ambapo uzalishaji umefikia kiasi cha tani 18,930 kwa mwaka 2016/2017, kwa mazao ya korosho, pamba na kahawa mkoa wetu unaendelea kuweka mikakati thabiti wa kuyaendeleza” alisema Masenza.

Halmashauri zimeanza kuweka jitihada za kuhamasisha kulima mazao hayo alisema. “Kupitia jukwaa hili nawaagiza wakurugenzi wa halmashauri kukaa chini na vyama vya ushirika kuandaa mpango wa miaka mitano wa kuendeleza mazao hayo” aliagiza Masenza.

Alisema kuwa wananchi wakihamasishwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi, kutawaongezea wanaushirika kushiriki shughuli za uzalishaji mazao ya kibiashara na kuongeza kipato cha wanaushirika na wananchi kwa ujumla.

Akiongelea zao la tumbaku, mkuu wa mkoa alisema kuwa mkoa wa Iringa umekuwa ukizalisha tumbaku kwa zaidi ya miaka 50 lakini zao hili halijatoa mchango mkubwa kiuchumi kwa wananchi. 

Napenda kutoa rai kuwa tunatakiwa kujipanga upya ili kuendeleza uzalishaji wa zao hili. Uzalishaji wa zao la tumbaku umekumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa soko na uwepo wa madeni makubwa katika vyama vya msingi ambayo yanasababishwa na wanachama kutouza kupitia vyama vyao. Nachukua fursa hii kuwaasa wakulima wa zao hili kuzingatia taratibu za kilimo hicho hasa kutowatumia watoto, kupanda miti na kuuza kwa uaminifu kupitia vyama vya ushirika” alisisitiza Masenza.

Jukwaa la ushirika ni jukwaa la pili kufanyika ngazi ya mkoa, likishirikisha Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, wadau wa taasisi za kifedha na wanaushirika.
=30=