Monday, August 13, 2012





 

HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA GERTRUDE K. MPAKA WAKATI WA KUFUNGA MAFUNZO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI MWAKA 2012 KWA WAANDISHI WA HABARI WA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI PAMOJA NA MIKOA YA LINDI NA MTWARA YALIYOFANYIKA CHUO KIKUU RUAHA IRINGA,  TAREHE 13 AGOSTI, 2012


Ndugu Mwenyekiti,
Mratibu wa Mratibu wa Sensa Mkoa,
Watendaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Watendaji kutoka Sekretarieti ya Mkoa,
Ndugu Washiriki wa Mafunzo,
Mabibi na Mabwana,


Ndugu Mwenyekiti,kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa na kuhudhuria mafunzo haya hadi kufikia hatua ya mwisho yaani hatua ya kumaliza.  Aidha nachukua fursa hii kuwashukuru sana washiriki wote kwa kuheshimu mwaliko wa kuhudhuria mafunzo haya muhimu ambayo yalihusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na nafasi ya vyombo vya habari katika kufanikisha zoezi hilo.

Ndugu Mwenyekiti, nilipopata mwaliko kuwa Mgeni Rasmi kufunga mafunzo haya kwanza nilifurahi kwa kuwa niliona nimepata fursa ya pekee kukutana na kundi kubwa la waandishi wa habari kwa pamoja kitu ambacho ni nadra kutokea katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku. Pili nimefarijika na mwaliko wenu kwa kuwa utanipa fursa ya kuchangia mawazo katika baadhi ya maeneo ambayo yamezungumziwa katika mafunzo haya.

Ndugu Mwenyekiti, mafunzo haya nimeelezwa kuwa yamezungumzia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi iliyopangwa kufanyika tarehe 26 Agosti, 2012. Nimeelezwa kuwa jumla ya mada tano ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa kina ambapo pia washiriki walipata fursa ya kufanya mazoezi kwa vitendo kwa baadhi ya mada walizojifunza.

Kwa ujumla nimeelezwa kuwa mada zote ziliibua majadiliano na hoja mbali mbali pamoja na changamoto za hapa na pale lakini jambo muhimu ni kuwa lengo la majadiliano hayo yalilenga katika kujifunza zaidi na kuongeza ufahamu kwa kila mshiriki juu ya masuala ya msingi kuhusu Sensa. Mimi naamini kuwa wataalamu wetu hapa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu wamejitahidi kadri ya utaalamu wao na uwezo waliojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuyafafanua kinagaubaga masuala yote yanayohusu Sensa ambayo yalihitaji maelezo ya ziada ya yale yaliyowasilishwa. Mbali ya maelezo ya wataalamu nimeelezwa kuwa mmepatiwa nyaraka muhimu zenye kueleza na kufafanua masuala ya msingi ya Sensa. Nyaraka hizo zitawasaidia kuongeza ufahamu wenu kuhusu suala zima la Sensa.

Ndugu Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo ninaamini kuwa ndugu washiriki mmefaidika na maelezo hayo na sasa mmekamilika katika suala zima linalohusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Maana yake ni kuwa sio tu mko katika nafasi nzuri ya kuandika na kutangaza kwa usahihi habari za Sensa lakini pia mafunzo haya yatakuwa yamewatia shime na ari ya kushiriki katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012. Matarajio yetu basi ni kuona taarifa zaidi za Sensa hasa zile za kuhamasisha wananchi kushiriki zinatolewa mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini na hususan vyombo vyetu vilivyomo katika mikoa ya kanda yetu.

Ndugu Mwenyekiti, nafasi niliyopewa ni kuyafunga mafunzo haya lakini kabla ya kufanya hivyo ningependa kusisitiza mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la ushirikiano. Waswahili tuna msemo usemao ‘kidole kimoja hakivunji chawa’. Kama ilivyoelezwa na wataalamu, mafanikio ya Sensa yanategemea sana ushiriki na ushirikishwaji wa kila mdau katika nchi. Kwa maana hiyo ni ukweli usiopingika kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikisha Sensa kwa sababu mchakato wake ni mkubwa unaohitaji ushiriki wa wadau wa kila aina na kutoka sekta mbalimbali. Miongoni mwa wadau hao ni vyombo vya habari.

Hivi sasa nchi yetu inajivunia utajiri mkubwa wa vyombo vya habari ambavyo ni matokeo ya mabadiliko ya sheria ya umiliki wa vyombo habari iliyopitishwa na Serikali. Dhamira ya Serikali kufanya marekebisho hayo ni kuwapa fursa zaidi watanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa kuamini kuwa vyombo hivi vitatumika kuwaendeleza wananchi kwa kuwaelimisha, kuwahabarisha na kuwaburudisha.

Historia ya nchi yetu inaonyesha kuwa vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Serikali sio tu katika kuboresha hali ya maisha ya kila mwananchi bali pia katika kuimarisha uzalendo na mshikamano miongoni mwa wananchi. Hivyo, wito wa Serikali kwa vyombo vya habari ni kuviomba viendeleze ushirikiano na mshikamano wa watanzania kama vinavyovyofanya katika masuala mengine yenye maslahi na Taifa letu ili kufanikisha Sensa.   

Ndugu Mwenyekiti, naelewa kuwa Serikali haina shaka hata kidogo kuhusu uwezo wa vyombo vya habari katika kulieleza jambo hili kwa usahihi kwani mnalifahamu na kwa mafunzo na uzoefu mlionao nyinyi ni walimu na wasemaji wazuri hivyo tumieni ujuzi na uwezo wenu huo kuwaeleza wananchi kwa ufasaha kuwa Sensa ni muhimu kwao na kwa Taifa lao hivyo wasisite kushiriki. Kwa hiyo, matarajio ya Serikali ni kuona kuwa mnakuwa waelimishaji wazuri na wahamasishaji makini wa Sensa ili kila mwananchi kwa hiari yake aone kuwa ana wajibu wa kuhakikisha anahesabiwa na anahesabiwa mara moja tu.

Ndugu Mweneykiti,
Jambo la pili ni suala la kutoa taarifa sahihi na kwa wakati. Leo zimebaki siku 12 tu kufika siku ya Sensa tarehe 26 Agosti 2012. Hivyo vyombo vya habari na wasemaji wote wa Sensa hawana budi kuepuka kufanya makosa katika uhamasishaji na zaidi walenge katika mambo muhimu ambayo mwananchi anapaswa kuyafahamu. Mambo hayo aliyaeleza Mkuu wa Mkoa wakati alipofungua mafunzo haya nami sina budi kuyarudia ili kuweka msisitizo.

1.0      Kuwa Sensa ya Watu na Makazi itafanyika tarehe 26 Agosti, 2012.
2.0      Watakaohesabiwa ni wale tu watakaokuwa nchini usiku wa Jumamosi tarehe 25 Agosti kuamkia Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012.
3.0      Watakaohesabiwa katika Kaya ni wale watakaokuwa wamelala katika Kaya usiku wa kuamkia Siku ya Sensa ambao, kama nilivyoeleza awali, ni usiku wa Jumamosi ya tarehe 25 Agosti, 2012 kuamkia Jumapili terehe 26 Agosti, 2012 pamoja na wanakaya wanaofanya kazi za usiku ambao kwa usiku ule hawakulala kwenye Kaya.  Hawa ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya, ulinzi na usalama na hata sekta ya habari.
4.0      Ni muhimu Mkuu wa Kaya akaweka kumbukumbu sahihi za watu wake wote zikiwemo za umri,kiwango cha elimu, ajira anayofanya, mahali anaposhinda mwanakaya wakati wa mchana na kwa wanawake hali zao za uzazi.

Ndugu Mwenyekiti, mwisho, ningependa kueleza furaha yangu kwa washiriki wote kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa na uvumilivu wakati wote wa mafunzo. Ushirikiano na uvumilivu wenu huo ulikuwa muhimu katika kufanikisha mafunzo haya hadi sasa tunayafunga rasmi. Nichukue fursa hii kuwatakia safari njema wageni wetu wote kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na wenzetu kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara.

Baada ya kusema hayo naomba sasa nitamke kuwa Mafunzo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa waandishi wa habari wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja mikoa ya Lindi na Mtwara yamefungwa rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza
 
SENSA KWA MAENDELEO: JIANDAE KUHESABIWA