Monday, July 30, 2012

KKKT IRINGA WATAKIWA KUSHIRIKI KATIKA SENSA




Washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, usharika wa Iringa Mjini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya uundwaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kufanikisha uundwaji wa Katiba hiyo kwa kujumuisha mapendekezo ya watu wengi zaidi.

Wito huo umetolewa na mgeni rasmi Dkt. Christine Ishengoma katika harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa kanisa kuu la mtaa wa Wilolesi iliyofantik Katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzanaia, Usharika wa Iringa Mjini leo.

Dkt. Christine ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema “ndugu zangu Washarika natoa rai kwenu kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na kuwaeleza waumini wengine na wananchi kwa ujumla ili washiriki katika mchakato huu kwa kutoa elimu na hamasa”. Amesema “napenda kutoa wito kwenu wote kuwa huru kutoa maoni yenu Tume itakapopita katika maeneo na kukusanya maoni yenu”. 

Amesema kuwa baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa Katiba ya sasa inamapungufu kadhaa, hivyo huu ndio wakati wao wa kutoa maoni yao ili hayo mapungufu yaweze kufanyiwa kazi na kuingia katika Katiba mpya. Amesema hili litafanikiwa pale tu, washarika na wananchi watakapojitokeza kwa wingi kutoa maoni yao pindi tume ya kukusanya maoni itakapopita katika maeneo yao. Amewataka kuwa makini katika kusikiliza tarehe na sehemu ambazo mikutano hiyo itakuwa ikifanyika ili waweze kuwasilisha maoni yao kwa tume hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kuwa huru katika kutoa maoni yao na kuwahakikishia kuwa ukusanyaji wa maoni hayo hauhusiani na itikadi yoyote. Amesema ili Katiba hiyo mpya iwe ya mafanikio ni lazima maoni ya wananchi wengi yaweze kukusanywa na mafanikio hayo yanatokana tu, na wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa tume hiyo.  
=30=

TAASISI ZA DINI ZATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO ILI KUFANIKISHA SENSA




Serikali Mkoani Iringa imeomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa dini katika kuhakikisha kuwa elimu ya kutosha na hamasa vinatolewa ili uelewa huo uwafikie waumini na wananchi wengi kwa ujumla.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiendesha zoezi la harambee ya ujenzi wa kanisa kuu la mtaa wa Wilolesi mjini hapa katika ibada ya kwanza iliyofanyika katika kanisa kuu, usharika wa Iringa Mjini.

Dkt. Christine amesema kuwa Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi tarehe 26 Agosti, mwaka huu na kuendelea kwa takriban siku saba. Amesema “Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu za kidemografia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na Watu wote na Makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum”. Amesema kuwa Sensa hiyo ni zoezi lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsi, mahali wanapoishi, hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. 

Akiongelea malengo ya Sensa hiyo, Mkuu wa Mkoa amesema “Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inalenga kutathmini utekelezaji wa Mipango yetu mikubwa ya Maendeleo ambayo imekuwa ikitekelezwa katika kipindi kilichopita. Mipango hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania na Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar”.

Akiongelea nafasi ya kanisa katika kufanikisha Sensa hiyo, Dkt. Christine amesema “napenda kuongelea nafasi ya Kanisa katika kuhakikisha Sensa ya Watu na Makazi inafanikiwa. Ni kweli kuwa Kanisa linalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanikiwa kwa sababu takwimu hizo ndizo zitakazoiwezesha Serikali kutambua hali halisi na mahitaji halisi ya huduma zilipo katika maeneo yenu hivyo kuingizwa katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa”. Amesema “kwa msingi huo, ninawaomba sana kuwahamasisha waumini na wananchi kwa ujumla ili wahesabiwe na wahesabiwe mara moja tu, ili takwimu zitakazokusanywa ziwe sahihi”.

Ameyataja mambo muhimu ya kutiliwa mkazo wakati wa kuwahamasisha washarika na wananchi kwa jumla kuwa ni tarehe ya Sensa, umuhimu wa Sensa na yatakayojiri wakati wa zoezi la kuhesabu watu. Sensa hiyo ya Watu na makazi inaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa’.