Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa
umekamilisha maandalizi ya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2015 na
mitihani yote imefikishwa vituoni.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu
afisa elimu mkoa wa Iringa, Mwalimu Euzebio Mtavangu alipokuwa akiongelea maandalizi
ya mitihani ya kumaliza kidato cha nne kwa mkoa wa Iringa ulionza leo nchini
kote ofisini kwake.
Mwalimu Mtavangu alisema
kuwa mkoa wa Iringa una jumla ya vituo 196 vya kufanyia mtihani huo. Alivitaja
vituo hivyo kwa kila halmashauri kuwa ni halmashauri ya Manispaa ya Iringa (44),
halmashauri ya wilaya ya Iringa (33), halmashauri ya wilaya ya Kilolo (49),
halmashauri ya wilaya ya Mufindi (70) na mitihani yote imefikishwa katika vituo
husika.
Akiongelea idadi ya
wasimamizi, alisema kuwa mkoa unao jumla ya wasimamizi 527. Alisema kuwa kwa
mujibu wa muongozo wa mitihani hiyo msimamizi mmoja anatakiwa kusimamia wastani
wa watahiniwa 40. Aliongeza kuwa wasimamizi hao miongoni mwao ni walimu kutoka
katika shule za mkoa wa Iringa. Utaratibu wa kuwapata wasimamizi hao ni pamoja
na kuwafanyia upekuzi wa kina na kula kiapo cha kutunza siri kwa mujibu wa
sheria Namba 3 ya mwaka 1970. Alisema kuwa semina kwa wasimamizi wa mitihni
hiyo zilianza kutolewa kwa halmashauri zote kuanzia tarehe 28-30/10/2015.
Kaimu afisa elimu mkoa wa Iringa alisema kuwa
jumla ya watahiniwa 15,818 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya
sekondari mwaka huu. Mgawanyo wa watahiniwa hao katika halmashauri ni halmashauri
ya Manispaa (4,785), halmashauri ya wilaya ya Iringa (3,368), halmashauri ya
wilaya ya Kilolo (2,784) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi (4,881).
Akiongelea matarajio ya
ufaulu katika mkoa, Mwl Mtavangu alisema kuwa mkoa unatarajia kufanya vizuri na
kupindukia matarajio ya BRN ya 80%. Alisema kuwa matarajio hayo yanatokana na
mkoa kuwa uliboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Sababu nyingine
alizitaja kuwa ni wanafunzi wa masomo ya sayansi kufanya majaribio halisi baada
ya kuwa na maabara za kutosha na kufanya ufaulu kwa masomo ya sayansi kuwa mzuri.
Aidha, wingi wa walimu wenye shahada umeongeza chachu ya mafanikio katika sekta
ya elimu mkoani Iringa.
=30=
No comments:
Post a Comment