Wednesday, May 18, 2011

ZAIDI YA BIL NNE ZAKUSANYWA KUTOKA VYANZO VYA NDANI IRINGA

Serikali za Mitaa mkoani Iringa zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni nne kutokana na vyanzo vyake vya ndani (own sources).

Akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo na bajeti kwa mwaka 2010/ 2011 na mapendekezo ya mpango wa matumizi ya muda wa kati na bajeti (MTEF) mwaka 2011/ 2012- 2013/2014, Katibu Tawala Msaidizi- Sehemu ya Mipango na Urabitu, Nuhu Mwasumilwe amesema katika kipindi cha mwaka 2010/2011 Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa zilitarajia kukusanya jumla ya shilingi 7,051,034,698.00 kutokana na vyanzo vyake vya ndani.
Aidha, hadi kufikia mwezi Machi, 2011 jumla ya shilingi 4,476,848,601.96 zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 63 ya lengo.

Kuhusu mapokezi na matumizi ya fedha zilizodhinishwa mwaka 2010/ 2011, Mwasumilwe amesema kuwa mwaka 2010/2011, mkoa wa Iringa uliidhinishiwa kutumia jumla ya shilingi 142,573,623,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.

Aidha, kati ya hizo shilingi 105,256,869,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 37,316,754,000.00 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Hadi kufikia mwezi Machi, 2011 mkoa umetumia jumla ya shilingi 78,469,247,154.70 ambazo ni sawa na asilimia 81 ya fedha iliyopokelewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

WIZARA YAANZISHA MPANGO WA KUENDELEA UTALII NCHINI

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanzisha mpango kamambe wa kuendeleza sekta ya utalii nchini utakaohusisha rasilimali za utalii zilizopo.

Hayo yamesemwa na Deograsias Mdamu, Afisa Utalii Mkuu kutoka Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, wakati akiwasilisha mada juu Sera ya Utalii na Mkakati ya kuendeleza Utalii nchini katika kikao cha Kamati ya Uchauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo leo.

Mdamu amesema “mpango huu ni mkakati unaoelekeza jinsi ya kuendeleza utalii nchini kwa kuzingatia rasilimali za utalii, maendeleo ya mifumo mbalimbali, vivutio vikuu vya utalii, masoko ya utalii, taaluma ya kuhudumia sekta ya utalii, sera, sheria, taratibu na miongozo iliyopo”.

Akifafanua mikakati ya kukuza utalii, Mdamu ameitaja kuwa ni kuendeleza mazao mapya ya utalii, kutafuta masoko mapya na kuimarisha masoko ya zamani pia kuimarisha utafiti katika eneo la utafiti.

Vilevile, kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji baina ya Wizara na Taasisi za Serikali zinazohusika na maendeleo ya sekta ya utalii pamoja na kuongeza mapato ya utalii kutokana na leseni za biashara, mikataba ya uwekezaji na kodi.
Mikakati mwingine ameitaja kuwa ni pamoja na kuhimiza ubora wa huduma kwa utalii kama afya, benki, usalama na mawasiliano.

Kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi na haki za binadamu katika sekta ya utalii.
Kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya sekta za uzalishaji wa bidhaa na huduma nyingine zitumikazo na sekta ya utalii na kupanua ushiriki wa sekta hizi katika biashara za utalii.

Afisa Utalii Mkuu, ameongelea pia mtawanyiko wa sekta ya utalii na kusema kuwa sekta hiyo ni kubwa na imetawanyika katika makundi anuai huku kundi kubwa likiwa ni wafanyabiashara wenye mitaji midogo huku kundi dogo sana likiwa ndilo lenye wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa.

Aidha, ameupongeza mkoa wa Iringa kwa kuwa na Maafisa Utalii katika Halmashauri zake ukiwa ni mkoa pekee wenye maafisa hao katika kila Halmashauri na kuahidi kuwapa ushirikiano stahiki katika kuiendeleza sekta ya utalii nchini.

Sekta ya utalii huchangia katika kuzalisha ajira, mapato ya fedha za kigeni na maendeleo katika sehemu mbalimbali mijini na vijijini.    

Mil 226 ZATOZWA KWA MAGARI KUZIDISHA UZITO

Zaidi ya shilingi milioni 226 zimelipwa kama tozo la uharibifu wa barabara kwa wakala wa barabara Mkoa wa Iringa kutokana na magari kuzidisha uzito imefahamishwa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa matengenezo na ukarabati wa barabara kwa mwaka wa fedha 2010/ 2011 kwa kipindi kinachoanzia Julai 2010 hadi Machi, 2011 na mpango wa mwaka wa fedha 2011/ 2012, katika kikao cha Bodi ya barabara Mkoa wa Iringa, Meneja wa wakala wa barabara (Tanroads) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Paul Lyakurwa amesema katika kipindi cha Julai, 2010 hadi Machi, 2011 magari yaliyopimwa katika mizani isiyohamishika iliyopo katika mji mdogo wa Makambako ni 19,104 na kati ya magari hayo magari 2,494 (sawa na asilimia 13) yalizidisha uzito na kulipishwa tozo la uharibifu wa barabara kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Barabara Na. 30 ya mwaka 1973 na Kanuni zake za mwaka 2001 ambapo jumla ya shilingi milioni 226.582 zililipwa .

Meneja wa wakala wa barabara mkoani hapa amekemea vikali tabia inayoendelea kila kukicha ya matumizi mabaya ya hifadhi ya barabara kwa baadhi ya wananchi kuendea kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo na biashara ndani ya hifadhi ya barabara jambo linalosababisha kuziba kwa mifereji na makalavati na kusababisha maji kutuama barabarani na kusababisha harufu mbaya na magonjwa ya mlipuko. 

Baadhi ya Wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Iringa 


Baadhi ya Wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Iringa 

Aidha, amesema kuwa ofisi ya meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Iringa inalo jukumu la kudhibiti uzito wa magari barabarani kwa kutumia mizani isiyohamishika iliyopo katika mji mdogo wa Makambako, Wilayani Njombe.
AHADI ZA DR. JK ZAANZA KUTEKELEZWA NA TANROADS IRINGA

Ofisi ya Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa (TANROADS) imeanza utekelezaji wa ahadi za Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010 kuhusu sekta ya barabara mkoani hapa.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Iringa,
Mhandisi Paul Lyakurwa

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ahadi hizo katika kikao cha Bodi ya Barabara ya mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, meneja wa wakala wa barabara (TANROADS), Mhandisi Paul Lyakurwa amesema ujenzi wa barabara ya Iringa-Mtera-Dodoma yenye urefu wa Km 260 kwa kiwango cha lami umeanza.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika sehemu tatu za Iringa-Migoli (Km 95.2), Migoli- Fufu (Km 93.2) na Fufu- Dodoma (Km70.9).
Aidha, mkataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Iringa-Migoli (95.2)  ulisainiwa tarehe 13 Januari, 2011 kati ya TANROADS na Mkandarasi M/S China Sichuan International Cooperation Co. Ltd kwa gharama ya Tshs. 84,216,378,355.50 wakati muda wa kukamilisha kazi ni miezi 35. Sehemu ya Migoli-Fufu (93.2) mkataba ulisainiwa tarehe 13 Januari, 2011 kati ya TANROADS na Mkandarasi M/S China Sichuan International Cooperation Co. Ltd kwa gharama ya Tshs. 73,612,329,958.67 wakati muda wa kumaliza kazi ni miezi 35. Sehemu ya Fufu-Dodoma (Km 70.9) mkataba ulisainiwa tarehe 13 Januari, 2011 kati ya TANROADS na Mkandarasi M/S China Communication Construction Co. Ltd kwa gharama ya Tshs. 64,327,389,129 wakati muda wa kukamilisha kazi ni miezi 27 na mkandarasi anaendelea na ujenzi wa kambi.

Kuhusu kukamilisha ujenzi wa barabara ya Njombe- Makete yenye urefu (Km 109) kwa kiwango cha lami, Meneja wa TANROADS amesema kuwa ujenzi wa Km 9.5 kati ya Mang’oto na Tandala ndani ya Wilaya ya Makete umekamilika. Aidha, ujenzi wa Km 2 maeneo ya Mang’oto unaendelea na unatarajia kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2010/2011.

   Aseri Msangi, Mwenyekiti (wa pili kulia), Gertrude Mpaka, Katibu (wa pili kushoto), Dr. Binilith Mahenge, Makamu Mwenyekiti (wa kwanza kulia) na Deo Sanga, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa (wa kwanza kushoto)

Akiongelea mpango uliopo kwa mwaka 2011/ 2012 Meneja huyo ameutaja kuwa ni kufanya upembuzi yakinifu, usanifu pamoja na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara yote kwa kiwango cha lami kama fedha zitapatikana.

Kuhusu maeneo korofi amesema yataendelea kuimarishwa kwa changarawe ili barabara iendelee kupitika kipindi chote cha mwaka.