Tuesday, October 20, 2015

MATUKIO WAKATI WA KUAPISHWA MKUU WA WILAYA MTEULE YA IRINGA RICHARD KASESELAm

Mhe. Richard Kasesela akisaini kitabu cha wageni

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa

Mkuu wa Utawala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Scolastica Mlawi (kulia)

Mhe. Richard Kasesela akiapa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Amina Masenza (kulia) akimkabidhi Katiba ya Jamhurir ya Muungano wa Tanzania Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu (kushoto)

DC IRINGA SIMAMIA ULINZI NA USALAMA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela ametakiwa kusimamia ulinzi na usalama katika wilaya ya Iringa ili mkoa uwe salama katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza muda mfupi baada ya kumuapisha mkuu wa wilaya mteule wa Iringa katika ofisi ya mkuu wa mkoa leo.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa Amina Masenza
Masenza alisema “suala la ulinzi na usalama ni muhimu sana katika wilaya ya Iringa ili mkoa uwe salama. Hivyo, lazima ulisimamie ipasavyo. Binafsi nina imani na wewe na utendaji wako wa kazi hivyo hautashindwa katika kutekeleza majukumu yako”. Alisema kuwa wilaya ya Iringa ikiwa salama wananchi wataendelea kushiriki katika mampeni za kisiasa kwa uhuru na amani na hatimae kupiga kura salama.

Mkuu wa mkoa alimtaarifu masuala ya kipaumbele kwa mkoa wa Iringa kuwa ni lishe, ukimwi na usafi wa mazingira. Alimtaarifu kuwa katika ratiba yake ya kazi lazima ijikite katika utekelezaji wa mpango mkakati wa mkoa unaolenga kukabiliana na changamoto za lishe, hali ya maambukizi ya ukimwi na usafi wa mazingira.

Katika salamu za mkuu wa wilaya ya Iringa mteule Richard Kasesela alimshukuru Rais wa Jamhuri kwa imani aliyonayo kwake. Aidha, alisema kuwa katika kipindi hiki suala la amani ni agenda yake ya mwanzo kuelekea uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015. Alisema kuwa yeyote katika wilaya ya Iringa atakayetishia watu kwenda kupiga kura hasa wanawake atashughulikiwa. Alisema kuwa lazima wananchi wote katika wilaya ya Iringa washiriki katika zoezi la kupiga kura kikamilifu pasipo woga ili wafurahie haki yao ya kupiga kura kikatiba.

Akiongelea masuala ya kimkakati katika mkoa, mkuu wa wilaya mteule alisema “nitajitahidi kuhakikisha suala la lishe bora kwa wananchi hasa wanawake wajawazito na watoto wachanga linaboreka katika wilaya ya Iringa na mkoa kwa ujumla. Tatizo hili lazima liishe”.
 
Mkuu wa wilaya ya Iringa, Mhe. Richard Kasesela
Aidha, suala la ukimwi aliahidi kukabiliana nalo ipasavyo. Alisema kuwa ngono zembe ni jambo linalohitaji kuangaliwa kwa umakini zaidi. Wilaya itaangalia upya viashiria vya ukimwi na mitego ili kuangalia jinsi ya kuitegua mitego hiyo hatimae kupunguza maambukizi mapya. Akiongelea usafi wa mazingira alisema “mtu ni afya hivyo usafi wa mazingira ni afya pia. Lazima usafi wa mazingira uanzie kwa mtu mwenyewe katika mazingira ya nyumbani kwake na mazingira yanayomzunguka”.

Mkuu wa wilaya ya Iringa aliapishwa leo mjini Iringa kufuatia uteuzi wa Rais wa wakuu wapya wa wilaya 13 na kuhamishwa kwa wakuu saba wa wilaya tarehe 4/10/2015.
=30=

NEC YAVITAKA VYAMA KUELIMISHA WANANCHI TARATIBU ZA UCHAGUZI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevitaka vyama vya siasa nchini kuwaelimisha wananchi kufuata taratibu ili kufanikisha uchaguzi huru na salama nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume hiyo Jaji Mary Longway alipokuwa akifungua mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa mkoani Iringa.
 
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Mstaafu) Mary Longway akifungua mkutano
Jaji Longway alisema “vyama vya siasa vina nafasi kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, Tume inaamini kwamba ili mpiga kura aweze kufanya maamuzi sahihi ni muhimu kwake kupata elimu sahihi. Hivyo basi, Tume inatarajia kuona mkitumia majukwaa yenu vema katika kuhamasisha na kuelimisha si tu wananchi wenu bali jamii ya watanzania”. 

Alisema kuwa kuelekea uchaguzi mkuu, Tume imeandaa vituo vya kupigia kura 64,736. Tanzania bara vituo 63,156 na Zanzibar vituo 1,580. Aliongeza kuwa kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wapiga kura 450 na wasizidi 500. “Hata hivyo kituo kinapokuwa na wapiga kura zaidi ya 500 kinabidi kigawanywe ili viwe viwili yaani kituo “A” na “B” na namba ya wapiga kura itakuwa nusu kwa nusu. Mnaombwa kuwahamasisha wapiga kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikishia kupiga kura siku nane kabla ya siku ya kupiga kura ili kuweza kujua vituo vyao halisi vya kupigia kura” alisisitiza Jaji Longway.

Kamishna Longway alisema kuwa Tume imekuwa ikisikitishwa na baadhi ya vyama vya siasa kutumia majukwaa vibaya wakati wa kampeni. “Tume kwa namna ya pekee inawaomba katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kutumia nafasi zenu majukwaani kuelezea sera za vyama vyenu ili kuweza kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi baada ya kuwa na taarifa sahihi”. 

Tume imekuwa ikisikia katika vyombo vya habari malalamiko juu ya uvunjifu wa maadili ya uchaguzi katika kipindi hiki cha kampeni, “nitumie nafasi hii kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa kupeleka malalamiko yenu katika kamati za maadili na si kukimbilia katika vyombo vya habarir kama ambavyo baadhi ya vyama vya siasa na wagombea mmekuwa mkifanya”.
Viongozi wa Vyama vya Siasa Mkoa wa Iringa

Ndani ya ukumbi wa Siasa ni Kilimo

Aidha, aliwataka kuepuka kutoa taarifa na shutuma zisizo sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kujikita katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa wafuasi na wananchi kwa ujumla na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba, 2015.
=30=