Thursday, September 12, 2013

IRINGA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA JUHUDI




W
atumishi mkoani Iringa wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma ili kufikia malengo ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo na matokeo makubwa yanayoonekana.

Kauli hiyo imetolewa na Muu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa serikali wilayani Mufindi katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kupitia utaratibu wake wa kuongea na kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa serikali mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma

Dkt. Christine amesema kuwa kila mfanyakazi wa serikali lazima afanye kazi kwa nafasi yake na kwa kujituma ili kazi yake iweze kwenda vizuri na kufikia malengo ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wake. “Kazi hii ni yetu ya kumuendeleza mwana Mufindi na Iringa kwa ujumla. Hivyo, kila mmoja asipende kufanya kazi kwa kuchungwa ni vizuri kujichunga mwenyewe. Lazima muwe na ratiba zenu za kazi na zenye malengo” alisisitiza Dkt. Christine.

Amesema katika kuhakikisha matokeo makubwa yanapatikana na kuonekana kwa wananchi ni vizuri utaratibu wa matokeo makubwa sasa (BRN) ukaanzia nyumbani ili uweze kufahamika vizuri kuanzia ngazi ya familia. Amesema kuwa kabla ya kufikiria kutoa matokeo makubwa kwa ujumla wake ni vizuri kila mfanyakazi akajiangalia yeye mwenyewe. “Lazima uangalie wewe mwenyewe unaendaje na BRN” alisisitiza Dkt. Christine.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameyataja maeneo ya vipaumbele katika utaratibu wa matokeo makubwa sasa kuwa ni maji, kilimo, elimu, uchukuzi, nishati na mapato.

Akiongelea upande wa mapato, amesema kuwa ni lazima halmashauri ya wilaya ya Mufindi ikajipanga vizuri kuhakikisha inaongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi. Amesema “halmashauri hii inasikifa kwa uchapa kazi na ukusanyaji wa mapato hivyo hakikisheni mnaitendea haki halmashauri hii isirudi nyuma”alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa amekemea vikali siasa katika utekelezaji wa utaratibu wa matokeo makubwa sasa (BRN). Amesema “kwenye utaratibu wa BRN msiweke siasa, mpo hapa kwa ajili ya kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2010-2015.siaka kazini ni marufuku, fanyeni kazi za serikali kwa mujibu wa taratibu zilizopo” aling’aka Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Akiongelea maandalizi ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na Wiki ya Vijana, Mkuu wa Mkoa amewataka wafanyakazi hao kushirikiana na viongozi katika kufanikisha sherehe hizo kubwa mkoani hapa. “Amesema shirikianeni na viongozi wenu ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kuboresha maandalizi na maadhimisho ya sherehe hizi muhimu katika mkoa na taifa letu kwa ujumla”.

Akiongelea miradiitakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru mkoani Iringa, Mkuu wa Mkoa amezitaka wilaya kuhakikisha kuwa miradi ya Mwenye inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokubalika.
Mkoa wa Iringa umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na wikiya Vijana kitaifa kwa mwaka 2013.
=30=


IRINGA YAKOMESHA UDANGANYIFU KATIKA MITIHANI




Na. Bruno Machary
Serikali Mkoani Iringa imejidhatiti kufanikisha mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi unafanyika pasipo kuwepo na vitendo vya udanyanyifu.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Mwl. Joseph Mnyikambi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake ili kujua jitihada zilizochukuliwa na Mkoa katika kukabiliana na vitendo vya udanganyifu kwa walimu na wanafunzi wakati wa mtihani huo.

Akitoa ufafanuzi, Mnyikambi amesema kuwa wamejitahidi kutoa semina kwa walimu ili kuhakikisha  kuwa mtihani huo unafanyika kwa haki na amani pasipo kuwepo kwa vitendo vyovyote vya udanganyifu kwa wanafunzi wala walimu watakaosimamia mtihani huo. Kwa upande wa wanafunzi, amesema kuwa kila mwanafunzi atatumia dawati lake ili kuondoa mianya inayoweza kushawishi udanganyifu.

Akiongelea upande wa maandalizi ya mtihani huo, amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na  vifaa vyote vimeshafika Mkoani na vimeshapelekwa kila Halmashauri. “Vifaa vyote vinavyohusu masuala ya mtihani huo vimeshafika Mkoani hapa na vimeshapelekwa katika wilaya zote” amesema Mnyikambi.

Afisa Elimu huyo amesema kuwa katika mwaka wa masomo 2013  idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani huo imepungua kwa jumla ya wanafunzi 1194 ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2012. Kwa mwaka 2012 kulikuwa na watahiniwa 24,342 wakati mwaka huu wapo watahiniwa 23,148.

Mtihani huo unaotarajiwa kuanza kufanyika siku ya jumatano ya tarehe 11/9/2013 kitaifa, utajumuisha shule za msingi 466 za  Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa una jumla ya wilaya tatu ambazo ni Iringa, Mufindi na Kilolo, zenye jumla ya Halmashauri nne.
=30=

WATAHINIWA DARASA LA SABA WAPUNGUA IRINGA




Na Charles Amulike
Idadi ya watahiniwa wanaotarajia kufanya mtihani wa darasa la Saba mkoani Iringa imepungua kwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana 2012 kutoka wanafunzi 24,342 mpaka kufikia 23,148 kwa mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Joseph Mnyikambi, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kwa mwaka 2013.

Mnyikambi amesema kuwa jumla ya wanafunzi 23,148 tayari wamesajiliwa kufanya mtihani huo wa darasa la saba kwa mwaka huu 2013. Ameongeza kuwa kati ya watahiniwa hao wavulana 10,752 na wasichana 12,396. Akiongelea idadi ya watahiniwa hao kwa ulinganifu na mwaka jana, amesema “idadi ya watahiniwa waliofanya mtihani mwaka jana 2012 ni kubwa kuliko ya mwaka huu 2013”. Amefafanua kuwa mwaka jana jumla ya watahiniwa ilikuwa 24,342 waliofanya mtihani wa kumaliza darasa la saba. Kati yao wavulana walikuwa 11,484 na wasichana walikuwa 12,858.

Mnyikambi amesema kuwa idadi ya wanafunzi waliopungua kwa mwaka huu wa 2013 ni 1194 kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na mwaka jana 2012.

Akiongelea maandalizi ya kufanyika kwa mtihani huo, Mnyikambi amesema “maandalizi yamekamilika, ikiwa ni pamoja vyumba vya kufanyia mtihani huo na madawati ya kutosha wanafunzi wote wanaotarajiwa kufanya mtihani huo”. Amesema katika kukomesha vitendo vya udandanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, Mkoa umejipanga vizuri kuhakikisha kila mtahiniwa anakaa kwenye dawati lake peke yake. Ameongeza kuwa  wasimamizi wa mitihani wamepatiwa semina ili kuhakikisha wanadhibiti udanganyifu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza katika mitihani hiyo.

Afisa Elimu Mkoa amesema kuwa tayari vifaa vya mitihani vimefika na vimepelekwa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa. Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza Mkoani hapa.
=30=ᘖ