Thursday, June 9, 2011

MKOA WA IRINGA WAIBUKA MSHINDI WA USAFI NA MAZINGIRA

Mkoa wa Iringa umepongezwa kwa kuibuka mshindi wa jumla katika mashindno ya afya na usafi wa mazingira nchini na kupata zawadi ya kombe na kutakiwa mikoa mingine kuiga mfano huo ili mikoa yote iwe na mazingira safi na salama.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Mizengo Pinda katika utoaji zawadi kwa washindi wa shindano la afya na usafi wa mazingira, aliyewakilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka  kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kitaifa yaliyofanyika mjini Songea.
Katika mashindano hayo ya afya na usafi wa mazingira yaliyoratibiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Halmashauri za Manispaa (Iringa), Mji (Njombe) na Wilaya (Njombe) zimekuwa mshindi wa tatu (Manispaa ya Iringa), wa pili (Mji Njombe), na wa kwanza (Wilaya ya Njombe) katika ngazi ya Halmashauri za Manispaa, Miji na Wilaya.
Kitaifa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ndiyo mshindi kati ya majiji matatu yaliyoshindanishwa. Kwa upande wa Halmashauri za Manispaa jumla ya Manispaa 17 zilishindanishwa na Manispaa ya Moshi iliibuka msindi ikifuatiwa na Arusha na Iringa. Upande wa Halmashauri za Miji jumla ya Halmashauri sita zilishindanishwa na Mpanda iliibuka mshindi ikifuatiwa na Njombe. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilizishinda Halmashauri za Meru (namba mbili) na Rungwe (namba tatu). 
Mkoa wa Iringa umeibuka mshindi wa jumla wa mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira baada ya Halmashauri zake tatu za Iringa, Mji Njombe na Wilaya ya Njombe kushinda katika nafasi tofauti.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kitaifa kila mwaka tarehe 5 Juni na mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo ‘panda miti na kuitunza: hifadhi mazingira’ mkoani Ruvuma katika Manispaa ya Songea. Maadhimisho haya kimataifa yamefanyika katika miji ya Delhi na Mumbai nchini India.
JENGENI UTAMADUNI WA KUPANDA MITI
Watanzania wametakiwa kuachana na utamaduni wa kupanda miti kwa mazoea hasa katika kipindi cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira kitaifa na kujenga utamaduni kwa kupanda miti mara kwa mara ili kujihakikishia mazingira salama ya kuishi.
Rai hiyo imetolewa na Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka katika hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda alipomuwakilisha kwenye kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Mkoa wa Ruvuma, manispaa ya Songea.
Prof. Tibaijuka amesema “kupanda miti si fasheni bali ni kazi ya kudumu” hivyo utamaduni wa kupanda miti katika siku za maadhimisho hauna budi kuachwa na kufanya upandaji miti kuwa ni zoezi endelevu.  Amesema mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu na uhai hivyo utunzaji wake ni jambo la lazima kwa kizazi hiki ili kijacho kiweze kujivunia hazina hiyo.
Amesema maadhimisho haya yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘panda miti na kuitunza ili kuhifadhi mazingira’. Kaulimbiu inawataka watanzania kukaa chini na kutafakari na kujipima kama hatua zinazostahili zimechukuliwa katika kulinda.
Aidha, amesema kuwa misitu husaidia sana upatikanaji wa mvua jambo linalotegemewa sana katika kilimo na shughuli nyingine za kijamii. Vilevile, amekemea tabia inayoendelea kukua ya utakaji miti na uchomaji wa mioto ovyo. Amesema “kupanda miti si kuboresha mazingira tu bali na kuongeza kipato tukokana na mazao ya misitu”.
Awali katika utangulizi wake, Dkt.  Terezya  Huvisa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake imeandaa mkakati wa kuhifadhi mazingira uliojikita katika kuielimisha na kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa mazingira na uhifadhi wa uoto wa asili.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ni matokeo ya azimio la umoja wa Mataifa la mwaka 1972, la Stockhorm –Sweden na kitaifa yalizinduliwa tarehe 1 Juni, 2011 katika kiwanja cha Majimaji kilichopo Manispaa na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal. Maadhimisho yaha yamekwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuri wa Tanzania na miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


BAJETI YAUJENZI WA VIWANJA VYA MICHEZO IRINGA

Halmashauri za Mkoa wa Iringa zimeshauriwa kutenga bajeti ya kutosha ya kuhudumia michezo hasa ujenzi wa viwanja vya michezo ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa viwanja hivyo.
Ushauri huo umetolewa na George Lukindo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Njombe, wakati akifungua rasmi mashindano ya Umoja wa Michezo na Sanaa Sekondari Tanzania (UMISSETA) ngazi ya Mkoa yatakayopelekea kuundwa kwa timu ya UMISSETA ya Mkoa wa Iringa.
Lukindo amesema “upungufu wa viwanja vya michezo ni tatizo katika Mkoa wa Iringa kutokana na jiografia ya Mkoa wenyewe kutokuwa na maeneo mengi tambalale hivyo nazishauri Halmashauri za Mkoa huu zipange bajeti ya kutosha kwa shule kadhaa ili kujenga viwanja vya michezo”. Amesema huwezi kuongelea kuinua sekta ya michezo katika ngazi yoyote kama hutakuwa na viwanja vya kutosha na vilivyo katika ubora unaostahili kwa michezo husika.
Akiongelea ufinyu wa bajeti ya michezo ya UMISSETA, Lukindo amezishauri Halmashauri kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha za ziada ili kufidia upungufu unaojitokeza.
Akisisitiza suala la nidhamu amesema mchezaji asiye na nidhamu UMISSETA si mahali pake. Amesema “mchezaji asiye na nidhamu hata kama atakuwa ni mzuri kiasi gani asiingizwe katika timu ya Mkoa”.
Wakati akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mashindano ya UMISSETA, Mwenyekiti wa UMISSETA Mkoa wa Iringa ambae pia ni Afisa Elimu Mkoa, Joseph Mnyikambi amesema kuwa michezo ni upendo, furaha na msikamano na kusisitiza kuwa katika kipindi chote cha mashindano hayo suala la nidhamu lipewe umuhimu wa pekee. Vilevile, amewaasa wanamichezo kuwa wanapokuwa uwanjani lazima watarajie na kukubali kushinda, kutoka sare au kushindwa.
Katika risala iliyoandaliwa na UMISSETA Mkoa na kusomwa na Upendo Mdzovela iliainisha changamoto zinazoikabili michezo ya UMISSETA kuwa ni pamoja ufinyu wa bajeti inayotengwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Aidha, changamoto nyingine ni upungufu wa walimu wenye taaluma ya michezo na vifaa vya michezo na upungufu wa viwanja vya michezo.
Mechi za ufunguzi zilizofana sana kwa kuzishindanisha timu za mpira wa miguu ya Halmashauri ya Mji Njombe wasiosikia (viziwi) na timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ambapo Ludewa waliibuka kidedea kwa ushindi wa 1-0. Katika mechi nyingine ya mpira wa pete timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa iliibwaga timu ya Wasiosikia ya Halmashauri ya Mji Njombe kwa mabao 7-3.
MAAFISA MICHEZO LAZIMA MUONEKANE

Maafisa Michezo wa Halmashauri wametakiwa kutoka na kushiriki katika shughuli zote za michezo katika Halmashauri zao ili kudhihirisha uwepo wao na kuinua kiwango cha michezo katika Mkoa wa Iringa.
Agizo hilo limetolewa na Kenneth Komba, Afisa Michezo Mkoa wa Iringa, wakati akizungumza katika kikao maalumu cha kuweka mikakati ya kufanikisha michezo ya Umoja wa Michezo na Sanaa Sekondari (UMISSETA) mkoani hapa kilichowakutanisha Wakuu wa Shule za Sekondari, Maafisa Elimu Taaluma Sekondari, Walimu wa Michezo na Afisa Michezo Mkoa muda mfupi baada ya kuzipokea timu za michezo mbalimbali ya UMISSETA kutoka katika Halmashauri nane za Mkoa wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari ya Mpeche Wilayani Njombe.  
Komba amesema ili kuimarisha michezo yote katika Mkoa wa Iringa “ni lazima Maafisa Michezo wa Halmashauri watoke na kushiriki katika shughuli za michezo katika Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine wa michezo kwa sababu nyie ndio wataalamu katika tasmia ya michezo”. Aidha, amesisitiza ushirikishwaji wa Maafisa Michezo hao katika shughuli za michezo ili jamii iweze kunufaika na taaluma yao.
Komba ambaye pia ni Meneja wa timu ya UMISSETA ya Mkoa aliushukuru uongozi wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) ngazi ya Wilaya na Mkoa kwa kujipanga na kufanikisha kuanza kwa mashindano ya UMISSETA mkoani hapa. Amesema kuwa TAHOSSA wamefanikisha kuanza kwa mashindano hayo kutokana na nguvu waliyonayo iliyojengeka katika misingi madhubuti ya umoja wao na kuheshimiana. Amesema jambo lolote la kimichezo haliwezi kukwama kwa namna yoyote ile hasa likiwa ni shirikishi kwa wadau na likifanyika kwa moyo wa umoja na mshikamano mkubwa.
Mwenyekiti wa TAHOSSA Mkoa wa Iringa, Andrew Kauta, amewataka walimu wote kusimamia kwa dhati suala la nidhamu kwa wanamichezo wote pasipo kujali mipaka ya Halmashauri au Wilaya zao na kusisitiza kuwa katika nidhamu hakuna mipaka. Aidha, amesisitiza kuwa michezo ni umoja, mshikamano na burudani hasa suala la nidhamu likidhibitiwa zaidi katika mavazi na matumizi ya lugha.
Vilevile, amewata walimu wa michezo kuwasilisha takwimu sahihi za wanamichezo na michezo wanayoshiriki kwa kila Halmashauri ili kuondokana na upotoshaji wa takwimu na usalama wa wanamichezo.
Lengo la msingi la mashindano haya ya UMISSETA ngazi ya Mkoa ni kushindanisha Wilaya sita na Halmashauri zake nane za Mkoa wa Iringa na hatimaye kupata timu moja ya Mkoa itakayokwenda kushiriki mashindano ya Kanda yanayotarajia kutimua vumbi Mkoani Ruvuma kuanzia tarehe 2 Juni, 2011.
Michezo ya UMISSETA inatarajia kuanza leo ngazi ya Mkoa katika Wilaya ya Njombe na inatarajia kushirikisha jumla ya wanamichezo 1088 katika michezo mbalimbali. 
KILIMO CHA MTAMA KIIMARISHWE

Viongozi wa Mkoa wa Iringa wameshauriwa kuweka juhudi za dhati katika kilimo cha mtama ili kukabiliana na baa la njaa linayoyakabili baadhi ya maeneo katika Wilaya za Iringa na Kilolo mkoani hapa.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Darry Rwegasira wakati akitoa uzoefu wa jinsi Wilaya ya Mpwapwa ilivyofanikiwa katika kilimo cha mtama na kukabiliana na baa la njaa.
Rwegasira amesema mapokeo ya viongozi ni jambo la msingi sana katika kufanikisha kilomo cha zao la mtama. Kwa upande wa Wilaya yake amesema “mapokeo ya viongozi wa Wilaya ya Mpwapwa ni mazuri sana”. Amesema Wilayani kwake kuanzia Mkuu wa Wilaya, Madiwani, Afisa Kilimo, Katibu wa CCM na Maafisa Watendaji wanalima zao la mtama jambo linalowafanya wananchi kuona mfano na umuhimu wa kilimo hicho kutoka kwa viongozi wao.
Mkuu wa Wilaya amesema kuwa Wilaya ilitengeneza sheria mdogondogo zinazosimamia utekelezaji wa mkakati wa kilimo cha mtama Wilayani hapo. Aidha, alishauri kuwa nguvu kupindukia zisitumike badala yake uhamasishaji na elimu ndio msingi pekee wa kuwafanya wananchi kukubaliana na kilimo hicho na kwa kuangalia mifano kutoka kwa viongozi wao.
Vilevile, mkakati mwingine uliotumika ulikuwa ni uundaji wa timu na kamati kuanzia ngazi za kijiji hadi Wilaya zikiwahusisha wataalamu wa kilimo na viongozi.
Wilaya ya Mpwapwa ilichagua kata tisa za mfano na kila kijiji kilikuwa na wakulima 98 wanaotumika kama walimu wa kuwaelimisha wenzao.
Nae kiongozi wa timu iliyokwenda kujifunza kilimo cha mtama Wilayani Mpwapwa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Asseri Msangi, amewashauri wakulima wa Wilaya ya Mpwapwa kutumza ardhi vizuri dhidi ya uharibifu unaotokana na mmea uitwao kidua. Amesema kutokana na hatari yam mea huo kwa ardhi na mazao Serikali ya kikoloni ilitunga Sheria ya 1946 kwa ajili ya kulinda ardhi dhidi ya kuharibika. Msangi amesema “tunzeni ardhi yenu vizuri, ardhi ni mali msipoitunza mtaumbuka”, “msipoitunza ikaharibika mtaenda wapi kwingine tumejaa”. Vilevile, amewashauri wataalamu wa kilimo kuwa watu wanaopenda mabadiliko na kwenda na wakati katika kuboresha na kuinua kilimo. 
VYUO VIONGEZA MAPATO KWA KUANZISHA MIRADI

Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vimetakiwa kufikiria mikakati ya kuongeza mapato kwa kupitia miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujielekeza katika mahitaji ya msingi ya jamii inayovizunguka.
Rai hiyo imetolewa na Ummy Ally Mwalimu, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto alipotembelea chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Ruaha kilichopo katika Manispaa ya Iringa.
Mwalimu amesema “lazima mfikirie jinsi ya kuongeza mapato kwa kupitia miradi mbalimbali na mahitaji ya jamii ili muweze kuongeza mapato ya chuo”. Amesema vyuo vikiweka mkakati wa kuongeza mapato vitaweza kutatua matatizo yaliyo ndani ya uwezo wa vyuo husika badala ya kuisubiri Serikali kufanya kila kitu. Aidha, amevishauri vyuo vya maendeleo ya wananchi kuangalia fursa na vikwazo vilivyopo katika jamii na kuandaa programu za kuisaidia jamii. Ametolea mfano kuazisha programu za kuwawezesha kinamama kuondokana na umasikini na kujitegemea na programu za elimu ya ujasiliamali.
Naibu Waziri amehimiza kuendeleza na kudumisha ushirikiano baina Mkoa, Halmashauri na vyuo hivyo ili jamii iweze kunufaika na huduma zitolewazo kwasababu wote wanategemeana.
Awali alitembelea shule ya sekondari wasichana ya Iringa na kuongea na wasichana kwa minajili ya kuhamasisha maendeleo na usawa wa kijinsia na kuwatia moyo wanafunzi hao.
Kaimu Mkuu wa chuo cha maendeleo ya jamii Ruaha, Gaspar J. Msigala alizitaja baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo hicho kuwa ni pamoja na upungufu wa miundombinu ya kitaaluma jambo linalosababisha udahili wa wanafunzi wachache ukilinganisha na uhitaji wa wanafunzi wanaotuma maombi na kuwa na sifa. Aidha, mkakati wa awali uliotumika kukabiliana na changamoto hiyo ni pamoja na kugawa wanafunzi katika awamu mbili za masomo yaani wanaoanzi asubuhi na wengine jioni.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto yupo katika ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani hapa kutembelea vyuo maendeleo ya jamii na vyuo vya maendeleo ya wananchi kuzifunza fursa na changamoto zilizopo, kuongea na watumishi na kuongeza hamasa ya kimaendeleo.
Chuo cha maendeleo ya jamii Ruaha kipo kilometa tatu kutoka Iringa mjini na kilianza mwaka 2007 baada ya kubadilishwa toka chuo cha maendeleo ya wananchi.    
MGAWANYO WA RASILIMALI USIO HAKI CHANZO CHA KUVUNJIKA KWA AMANI NCHINI

Mgawanyo wa rasilimali za nchi usio usiozingatia usawa na haki ni miongoni mwa vyanzo vya kuvunjika kwa amani katika jamii.
Rai hiyo imetolewa na Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fredrick Sumaye katika hotuba yake wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha teknolojia ya Habari na mawasiliano (Orphanage ICT and School) kwa ajili ya watoto yatima mkoani Iringa iliyofanyika katika uwanja wa Samora mjini hapa.
Sumaye amesema “mgawanyiko wa mali usiozingatia usawa na haki na hasa utajiri unapojikusanya kwa wachache lazima amani itatoweka”. Amesema nchi ikiwa na matajiri sana na masikini wa kutisha hasa wakiwa ndio wezi sana amani hutoweka. Aidha, amesisitiza kuwa amani ni rasilimali kubwa kuliko zote katika taifa na pindi inapotoweka si rahisi kuirudisha.
Amesema kuwa ubaguzi na chokochoko za kiimani nazo huchangia uvunjifu wa amani. Amesisitiza kuwa “ubaguzi wa dini unapoota mizizi amani huyeyuka kama pande la barafu”.
Kuhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini amesema “uvumilivu wa vyama vya siasa ni jambo la msingi sana katika kulinda amani ya nchi”. Amesema ni lazima taifa lijifunze kujadiliana bila kupigana na kupingana kwa sera na hoja pasina kupigana na kuchochea uvunjifu wa amani.
Kwa upande wa rushwa na ufisadi, Waziri Mkuu mstaafu amesema “penye rushwa mwenye haki hunyimwa stahili yake na asiye na haki hununua haki ya mwingine”. Amesema kuwa rushwa hupofusha macho ya wanaoona na ni adui wa haki.
Awali akitoa taarifa fupi ya kituo hicho, Mratibu wa shirika la Children Care Development Organization (CCDO) Sixtus Kanyama amesema kuwa lengo kuu la shirika lake ni kuimarisha uwezo wa jamii katika kukuza elimu, afya na kutoa msaada wa kimaeneleo kwa jamii kupitia mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT). Amesema kituo hicho kitatoa mafunzo ya teknolojia kwa watoto kuanzia shule ya awali, msingi na sekondari na lugha za kigeni za kiingereza, kichina, kifaransa, kijerumani na kiarabu. Kituo hicho kwa kuanzia kinatarajiwa kugharimu shilingi milioni 120.