Tuesday, August 6, 2013

H/W IRINGA YABORESHA MAZINGIRA YA KAZI KWA WATUMISHI WA PEMBEZONI




Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweka mkakati wa kuimarisha mazingira mazuri kwa wafanyakazi wake hasa wanaofanya kazi pembezoni ili kuongeza ari na ufanisi wa kazi.
 Mkuu wa Mkoa wa iringa Dkt. Christine Ishengoma (watatu kushoto) akitoa maelekezo katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo (kushoto) akifafanua jambo mbele ya kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Utumishi, Robin Gama alipokuwa akijibu swali kutoka kwa wananchi waliotembelea banda la Halmashauri hiyo na kuhoji ushiriki wa Idara ya Utumishi katika maonesho ya Nanenane mwaka 2013 tofauti na miaka mingine.

Gama amesema kuwa Idara ya Utumishi ndiyo inayoajiri na kupanga maeneo ya kufanyia kazi kwa mujibu wa mahitaji hivyo ushiriki wake katika maoensho hayo ni wa kimkakati kuja kuangalia matunda halisi ya watumishi wetu. Amesema kuwa mtumishi anapofanya kazi vizuri hupewa motisha na anapofanya vibaya tofauti na kanuni na taratibu za utumishi wa umma huwajibishwa kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Akiongelea changamoto ya watumishi kutopenda kukaa na kufanya kazi maeneo ya pembezoni, Gama amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, Halmashauri ya wilaya ya Iringa, kupitia Idara ya Utumishi imekuwa ikiwapatia motisha ikiwa ni pamoja na kuwapa vipaombele na vivutio kadhaa ili wabaki na kupenda mazingira ya kazi. Amevitaja vivutio hivyo kuwa ni pamoja na mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri na mafuta.

Afisa Utumishi amesema kuwa Idara ya utumishi ndiyo mfano hivyo ikifanya vizuri, watumishi wote watafanya vizuri na wananchi kunufaika na huduma zitolewazo na Serikali. Amesmea kuwa katika kutekleleza hilo, halmashauri yake imekuwa ikiishirikisha jamii katika kuibua na kuandaa mipango ya maendeleo katika vijiji.

Gama amewsema kuwa dhana ya maonesho ya Nanenane kwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa ni mafanikio makubwa na mazuri kwa wakulima yanategemea ushauri mzuri kutoka kwa wataalamu wa ugani wa kilimo, mifugo na ushirikika waliopata mafunzo, wenye uzoefu, ubunifu na utendaji kazi mzuri.

Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa mufibu wa sense ya watu na makazi ya mwaka 2012 ina watu 254,032 kati yao wanawake ni 130,789 na wanaume 123,243. Tarafa 6, Kata 25, vijiji 123 na vitongoji 716. Aidha, Halmashauri ina Idara 13 na vitengo 6.
=30=


VYUO VIKUU VYATAKIWA KUANDAA PROGRAMU ZA KILIMO




Vyuo vikuu nchini vimeshauriwa kuwekeza katika kuandaa program za shahada za kilimo na mifugo ili kuzalisha wataalamu wengi zaidi wa kilimo nchini.
 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akisaini kitabu cha wageni katika banda la University Computing Cente
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipotembelea maonesho ya Nanenane kanda ya Nyanda za Juu kusini yanayoendelea katika uwanja wa John Mwakangale mjini Mbeya.

Dkt. Christine amesema kuwa ni vizuri sasa vyuo vikuu vikawekeza katika kuandaa program za shahada za kilimo na mifugo ili kutayarisha wataalamu wengi zaidi katika kada hizo. Amesema kwa sasa chuo kinachotegemewa ni chuo kikuu cha Sokoine, pamoja na kuwa kinafanya vizuri, ni vizuri vyuo vingine vikaanzisha program hizo ili kuongeza wigo wa kuandaa wataalamu nchini. 

Aidha, ameshauri kuwa vyuo vikuu vyote vya ukanda wa Nyanda za Juu Kusini vishirikishwe ipasavyo katika maandalizi na maonesho ya Nanenane kutokana na nafasi yao muhimu katika uzalishaji wa wataalamu wa fani mbalimbali.

Akiongelea ushiriki wa Halmashauri za mkoa wa Iringa katika maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa halmashauri hizo zinafanya vizuri ikiwa ni pamoja na kuonesha uhalisia wa shughuli zinazofanyika katika halmashauri zao. “Halmashauri za mkoa wa Iringa zinaonesha uhalisia wa shughuli zinazofanyika huko, hii ni hatua nzuri zaidi ukilinganisha na mwaka jana” alisisitiza Dkt. Christine.

Ametoa wito kwa wakulima wa pareto nchini kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutokana na uhitaji wake katika soko kuwa juu tofauti na uzalishaji wake. Amesema kuwa kiwanda cha pareto nchini kipo kimoja tu wilayani Mufindi na kimekuwa kikifanya kazi chini ya kiwango kutokana na kutokuzalishwa kwa wingi kwa zao hilo.
=30=

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma aliyekaa akiangalia kielelezo toka UCC. Kushoto ni Kaimu RAS Wamoja Ayubu.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma aliyekaa akiangalia kielelezo toka UCC

DKT. CHRISTINE ISHENGOMA AITAKA TRA KUKAZA BUTI




Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma ameitaka Mamkala ya Mapato Tanzania kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili kuongeza wigo wa utoaji huduma nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. christine Ishengoma (Mb.)

Kauli hiyo ameitoa katika majumuisho ya ziara ya Nanenane baada ya kutembelea mabanda ya maonesho likiwemo banda la mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) yaliyopo katika uwanja wa Mwakangale, Uyole Mbeya.


Dkt. Christine amesema kuwa mamlaka ya mapato Tanzania inafanya kazi nzuri, lakini bado inatakiwa kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Amesema kuwa Serikali bado inapoteza mapato mengi kwa sababu mamlaka hiyo haijakusanya mapato kiasi cha kutosha. Aidha, ameitaka mamlaka hiyo kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali ili kuongeza wigo wa serikali katika kutoa huduma kwa wananchi wake.


Amesema kuwa katika kipindi hiki ambapo serikali inaendelea kutekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) ni pamoja na kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu.


Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyekuwa mgeni rasmi katika siku ya mkoa wa Iringa katika maonesho ya Nanenane, amewataka mamlaka ya mapato kuongeza kasi na mikakati ya kuwahamasisha wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa ili kuziba mwanya wa upotevu wa mapato ya Serikali. Katika kuimarisha elimu na hamasa kwa wananchi juu ya kudai risiti wanaponunua bidhaa, Dkt. Christine ametaka viongozi na wadau wote kushirikiana katika kutoa elimu hiyo. Amesema “jukumu hili si la TRA pekee, bali ni jukumu letu sote. 

Lazima viongozi wote na wadau mbalimbali kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kudai risiti”. Amesema kuwa kwa kufanya hivyo tutapunguza mwanya na hatimae kuondoa kabisa upotevu wa mapato ya serikali kwa njia hiyo.


Akiongelea hali halisi ya maonesho ya Nanenane baada ya kutembelea mabanda,, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu amepongeza jinsi Halmashauri na wadau walivyojipanga katika kuonesha bidhaa zinazozalishwa katika maeneo yao na shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo yao. Aidha, ametoa wito kwa washiriki wote kutumia maonesho hayo, si kuona tu, bali pia kujifunza juu ya matumizi ya teknolojia katika kukuza na kuboresha kilimo na mifugo.


Maonesho ya Nanenane mwaka 2013 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “zalisha mazao ya kilimo na mifugo kwa kulenga mahitaji ya soko”.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. chrisrine Ishengoma (mwenye kofia) na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Wamoja Ayubu wakipata maelezo katika Banda la TRA


=30=