Wednesday, July 8, 2015

CMT H/W IRINGA ITEKELEZE MPANGO NA BAJETI MWAKA 2015/2016



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Menejimenti ya halmashauri ya wilaya ya Iringa yatakiwa kufanya maamuzi sahihi kwa kufuata mpango na bajeti wa mwaka 2015/2016 ili kutokujitengenezea madeni.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, bibi Amina Masenza wakati wa uvunjaji wa Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Iringa lililofanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Mkuu wa mkoa amewataka kuhakikisha maamuzi yatakayofanywa baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani yanakuwa yale tu yaliyo ndani ya mpango na bajeti ya halmashauri wa mwaka 2015/2016 kama ilivyoidhinishwa na Baraza la Madiwani. Amewataka kutunza vizuri nyaraka zote za maamuzi yatakayofanyika katika kipindichote baada ya Baraza hilo kuvunjwa. “Natambua kuwa waheshimiwa madiwani wote na hata watendaji mnatambua kuwa wakati madiwani watakuwa hawapo katika nafasi zao ndani ya halmashauri, maamuzi ambayo yangefanywa na madiwani sasa yatafanywa na Kamati ya Menejimenti ya halmashauri (CMT), wafanye maamuzi ya busara na yenye manufaa kwa halmashauri” alisema bibi Masenza. 

Amesema kuwa mkoa utaendelea kuwa karibu na halmashauri kwa ushauri na ufuatiliaji wa masuala ya serikali za mitaa. Aidha, amezitaka serikali za mitaa mkoani Iringa kuomba usaidizi unaotakiwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya halmashauri.

Mkuu wa mkoa wa Iringa amewahakikishia madiwani hao kuwa serikali itaendelea kujivunia michango yao waliyoitoa na kuifanya halmashauri ya wilaya ya Iringa kuwa mfano kwa kuongoza katika ukusanyaji wa mapato ya ndani mwaka 2013/2014, kupata hati safi, kuwa mshindi wa mkoa katika mashindano ya nanenane kikanda yaliyofanyika mkoani Mbeya mwaka jana na kuwa halmashauriya kwanza kimkoa katika mashindano ya ukimbizaji Mwenge wa Uhuru mwaka jana.

Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa amesema kuwa anajivunia uhusiano mzuri baina ya baraza lake na watendaji wa halmashauri katika kufanikisha shughuli za kuwahudumia wananchi. Ameitaka halmashauri kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuboresha huduma kwa wananchi. Amesema kuwa mapato ya ndani ya halmashauri ndiyo msingi wa kuwaletea maendeleo wananchi kwa sababu mipango na matumizi yake inaendana na mazingira halisi ya halmashauri.
=30=

MIRADI 35 KUPITIWA NA MWENGE WA UHURU IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mwenge wa Uhuru utaweka mawe ya msingi, kukagua, kuzindua na kufungua miradi 35 yenye thamani ya shilingi 4,985,562,793 katika mkoa wa Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Bibi Amina Masenza alipokuwa akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajab Rutengwe katika eneo la Ruaha Mbuyuni wilayani kilolo.
Bibi. Masenza amesema “Mwenge wa Uhuru katika mkoa wa Iringa utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 35 yote ikiwa na thamani ya shilingi 4,985,562,793 ambapo kati ya fedha hizo serikali kuu imechangia shilingi 2,193,787,197 halmashauri za wilaya na manispaa shilingi 1,191,486,781, michango ya wananchi shilingi 1,158,299,859 na wadau wa maendeleo shilingi 441,988,956”. Amesema kuwa jumla ya miradi 6 itafunguliwa, miradi 18 itazinduliwa, miradi 5 itawekewa mawe ya msingi na miradi 6 itakaguliwa na Mwenge wa Uhuru. Miradi hiyo inatokana na sekta za kilimo, mifugo, maji, maliasili, ujenzi, barabara, afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zimebeba ujumbe usemao “tumia haki yako ya kidemokrasia; chini ya kaulimbiu; jiandikishe na kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2015. Amesema kuwa ujumbe huo ni muhimu katika kipindi ambapo watanzania wanapaswa kushikamana zaidi na kudumisha amani na utulivu licha ya tofauti za itikadi ya vyama.
Amesema kuwa ujumbe maalumu umeambatana na jumbe za kudumu nne ambazo ni mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya ukimwi na mapambano dhidi ya malaria.
=30=