Wednesday, July 8, 2015

MIRADI 35 KUPITIWA NA MWENGE WA UHURU IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mwenge wa Uhuru utaweka mawe ya msingi, kukagua, kuzindua na kufungua miradi 35 yenye thamani ya shilingi 4,985,562,793 katika mkoa wa Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Bibi Amina Masenza alipokuwa akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajab Rutengwe katika eneo la Ruaha Mbuyuni wilayani kilolo.
Bibi. Masenza amesema “Mwenge wa Uhuru katika mkoa wa Iringa utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 35 yote ikiwa na thamani ya shilingi 4,985,562,793 ambapo kati ya fedha hizo serikali kuu imechangia shilingi 2,193,787,197 halmashauri za wilaya na manispaa shilingi 1,191,486,781, michango ya wananchi shilingi 1,158,299,859 na wadau wa maendeleo shilingi 441,988,956”. Amesema kuwa jumla ya miradi 6 itafunguliwa, miradi 18 itazinduliwa, miradi 5 itawekewa mawe ya msingi na miradi 6 itakaguliwa na Mwenge wa Uhuru. Miradi hiyo inatokana na sekta za kilimo, mifugo, maji, maliasili, ujenzi, barabara, afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zimebeba ujumbe usemao “tumia haki yako ya kidemokrasia; chini ya kaulimbiu; jiandikishe na kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2015. Amesema kuwa ujumbe huo ni muhimu katika kipindi ambapo watanzania wanapaswa kushikamana zaidi na kudumisha amani na utulivu licha ya tofauti za itikadi ya vyama.
Amesema kuwa ujumbe maalumu umeambatana na jumbe za kudumu nne ambazo ni mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya ukimwi na mapambano dhidi ya malaria.
=30=

No comments:

Post a Comment