Friday, November 30, 2012

WAHASIBU WATAKIWA KUBADILIKA


Wahasibu nchini wametakiwa kubadilika na kuendana na mabadiliko ya kimfumo hasa imapoanzishwa kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa kazi na kupunguza upotevu wa fedha za Serikali.

Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa alipokuwa akiongea na maafisa wa Serikali Mkoani Iringa muda mfupi kabla ya kuhudhuria Mahafari ya Chuo kikuu cha Ruaha Iringa (RUCO).

Akifafanua kuhusu changamoto za mfumo wa Epicor 9.05 katika utekelezaji wa kazi za kihasibu na malipo, Dkt. Mgimwa ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kalenga amesema kuwa lengo la Serikali kuanzisha mfumo huo ni kuhakikisha ufanisi katika matumizi ya fedha za serikali na kuondoa mianya ya upotevu wa fedha hizo. Amesema “tumekuwa na kipindi kifupi sana cha kuwawezesha wahasibu wetu juu ya kuutumia mfumo wa Epicor 9.05”. Akiufafanua mfumo huo, amesema kuwa mfumo huo ulianzia Marekani mwaka 1996 na kuanzishwa nchini kutokana na uwezoz wake wa kuchukua maagizo ya kimalipo kwa wingi, ukubwa, wepesi na haraka na sifa yake nyingine ni kukidhi viwango vya kihasibu vya kimataifa. Amesema kuwa mfumo huo pia unauwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa nyingi kwa wakati. 

Amesema kuwa ili kuweza kuenda vizuri na mfumo huo ni lazima wahasibu wakubali kubadilika na kuwa wepesi zaidi kuyakubali mabadiliko hayo.

Akiongelea uidhinishwaji wa fedha za miradi ya maendeleo ambao umekuwa ukilaumiwa sana kuwa umekuwa ukichelewa sana, Waziri wa Fedha amesema kuwa mchanganuo wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ni muhimu sana na ndio unaozingatiwa kabla ya kuidhinishwa malipo wengine ya miradi ya maendeleo. Amesema kuwa thamani ya fedha ni jambo linalopewa uzito katika miradi yote ya maendeleo ili fedha ya serikali inayotolewa iendane na mradi uliokusudiwa. Amesema kuwa changamoto iliyopo katika kodi ya Serikali ikihusishwa na miradi ya maendeleo, amesema “tunaruhusiwa kutoa asilimia tano tu iliyopatikana na kupeleka katika miradi ya maendeleo na asilimia nyingine inabaki kwa ajili ya kulipa mishahara na shughuli nyingine za uendeshaji wa Serikali” amesisitiza Dkt. Mgimwa.  

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe ameelezea changamoto inayoukabili Mkoa wa Iringa kuwa ni ukomo wa bajeti hasa katika miradi ya maendeleo. Amesema kuwa katika miradi ya maendeleo fedha hizo zimepungua kutoka shilingi bilioni 1 hadi milioni 274. Ametolea mfano miradi inayoendelea kuwa ndiyo inayoathirika zaidi, kama ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa mwaka 2012/2013 imetengewa shilingi milioni 51 tu kati ya milioni 700 zinazohitajika.

Aidha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ameiomba Hazina kuwa inatoa kipaumbele kwa miradi ya maendeleo inayoendelea. Akiongelea fedha za matumizi ya kawaida amesema kuwa kupungua kwa fedha hizo kumekuwa kukisababisha kutokueleweka katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Amesema mfano mwaka 2011/ 2012 fedha za matumizi mengine Mkoa ulipangiwa shilingi bilioni 2.7 ingawa hazikutolewa zote. Aidha, mwaka 2012/2013 Mkoa umepangiwa shilingi bilioni 1.9.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amempongeza Waziri wa Fedha kwa kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo na kuomba ushirikiano wa viongozi na wadau wote katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
=30=