Friday, April 20, 2018

Saratani ya Kizazi kuua Wanawake Iringa



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Saratani ya mlango wa kizazi imekuwa ikichangiwa na kujamiiana katika umri mdogo na kuwa na wapenzi wengi na kusababisha vifo vya wanawake wengi mkoani Iringa.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu huria jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Masenza alisema kuwa saratani ya mlango wa kizazi inachangiwa na mambo mengi. “Saratani ya mlango wa kizazi inachangiwa na vitu vingi ikiwemo kuanza kujamiana katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuwa na ndoa za mitala, kuzaa watoto wengi, na uvutaji wa sigara” alisema Masenza.

Akiongelea dalili za saratani hiyo, alisema kuwa mara nyingi hujitokeza ikiwa imeshasambaa mwilini. Dalili hizo alizitaja kuwa ni kutokwa damu ya hedhi bila mpangilio pamoja na kutokwa damu baada ya kujamiana. Nyingine alizitaja kuwa ni maumivu ya mgongo, miguu na kiuno. Nyingine ni kuchoka, kupungua uzito, kupungukiwa au kokosa hamu ya kula, kutokwa uchafu wa rangi ya kahawia au wenye damu kwenye uke, maumivu ya miguu au kuvimba. 

“Dalili mbaya zaidi zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuishiwa damu, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na fistula, na uvimbe wa tezi” alisisitiza Masenza.

Mkuu wa mkoa wa Iringa alielezea mkakati utakaotumika katika utoaji chanjo hiyo kuwa ni utaratibu wa kawaida katika vituo vya kutolea huduma za chanjo, baadhi ya shule zitachaguliwa na maeneo katika jamii na chanjo itatolewa kwa njia za huduma za mkoba.

Chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi itatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi bila malipo.
=30=