Sunday, December 29, 2013

IRINGA YAVUKA LENGO LA BRN KATIKA ELIMU








Mkoa wa Iringa imevuka lengo la matokeo makubwa sasa (BRN) kwa zaidi ya asilimia 60 kwa kiwango cha ufaulu kwa mtokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 ukishika nafasi ya tatu kitaifa.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kikao cha kamati ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mkoa wa Iringa mwaka 2014, Wamoja Ayubu katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha kamati ya uchaguzi mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.


 Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wamoja Ayubu (kulia) akifungua kikao (kushoto) ni Afisa Elimu Mkoa wa Iringa Mwalimu Joseph Mnyikambi

Wamoja amesema “kiwango cha ufaulu ni kizuri sana na mkoa wa Iringa umeshika nafasi ya tatu kati ya mikoa 25 ya Tanzania bara. Pia kiwango cha ufaulu kimepanda kwa Halmashauri zote. Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuzipongeza Halmashauri zote kwa kuvuka lengo la matokeo makubwa sasa ambalo ni asilimia 60 kwa mwaka 2013”. Amesema kuwa mwaka 2013 mkoa wa Iringa ulikuwa na watahiniwa 23,148 waliosajiliwa kufanya mtihani wakiwemo wavulana 10,752 na wasichana 12,396. Amesema miongoni mwao watahiniwa 22,922 wavulana wakiwa 10,630 na wasichana 12,292 sawa na asilimia 99 walifanya mtihani.

Akiongelea ufaulu, Wamoja ambaye pia ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amesema kuwa watahiniwa 14,956 (wavulana 7,042 na wasichana 7,914) ndio waliofaulu kwa kupata alama kati ya 100-250 sawa na asilimia 65.25. Aidha, amekieleza kikao hicho kuwa ni wakati muafaka kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu zaidi hadi kufikia asilimia 70 ambalo ni lengo la matokeo makubwa sasa kwa mwaka 2014.

Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 mkoa wa Iringa, Afisa elimu mkoa wa Iringa, Mwalimu Joseph Mnyikambi  amesema kuwa katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi uliofanyika tarehe 11-12 Septemba, 2013 shule za msingi 449 kati ya shule 482 ndizo zilizokuwa na watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Mwalimu Mnyikambi amesema kuwa mahudhurio katika siku za mitihani yameongezeka kutoka asilimia 98.3 mwaka 2012 hadi asilimia 99 mwaka 2013 likiwa ni ongezeko la asilimia 0.7 . Amesema kuwa kiwango cha kumaliza elimu ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 82 (2012) hadi asilimia 84 (2013) ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.

Afisa Elimu Mkoa wa Iringa amezitaja shule 10 bora za serikali na binafsi kimkoa kutoka kila Halmashauri kwenye mabano kuwa ni:- Sipto, Ummusalaama, Ukombozi, St. Dominic Savio, Star, Wilolesi, St. Charles (zote za Manispaa ya Iringa) nyingine ni Brooke Bondi na Southern Highland (Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi) na Mapinduzi (Manispaa ya Iringa). 

Akiongelea mwongozo wa uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2014, Mwalimu Mnyikambi amesema kuwa nafasi zilizotengwa kwa shule za vipaji maalum kwa mkoa wa Iringa ni Mzumbe (6), Kibaha (7) kwa wavulana na Kilakala (8) na Msalato (5) kwa wasichana. Nafasi za shule za bweni zilizotengwa kwa mkoa wa Iringa ni Malangali (12) na Songea (9) kwa wavulana na Sekondari ya wasichana ya Iringa (9) na Mgugu (8) wasichana. Shule za ufundi ni Ifunda (15), Iyunga (10) wavulana na Tanga (2) wasichana.

=30=