Sunday, January 26, 2014

DKT. ISHENGOMA APIGA MARUFUKU KUCHOMA MISITU



Serikali imepiga marufuku tabia ya wananchi kukata na kuchoma moto misitu mkoani Iringa ili kulinda misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. 
Marufuku hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya uzinduzi wa siku ya upandaji miti katika kijiji cha Mtili, wilaya ya Mufindi.
Dkt. Christine amesema kuwa juhudi za upandaji miti katika wilaya ya Mufindi ili ziwe endelevu ni lazima kukomesha tabia ya kukata na kuchoma miti. “Ndugu wananchi, ili juhudi hizi ziweze kuwa endelevu, natoa wito kwenu kuwa kuanzia sasa iwe ni mwiko, na aibu kuharibu miti na misitu, kwa kuichoma moto ovyo, kwa kuikata au kuifyeka ovyo, kuiharibu kwa kuishi ndani ya misitu. Kwa kufanya hivyo utakuwa umetenda kosa la jinai na unastahili kupewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria za misitu” aliongea kwa ukali Mkuu wa Mkoa. Amesema kuwa iwe tabia na utamaduni wa wananchi wa wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla kutunza miti iliyopandwa ili kuepuka janga la kuongezeka kwa mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, amewataka wananchi wote kuwa walinzi kwa kuwakamata na kuwaripoti wale wote watakao kiuka taratibu zilizopo za utunzaji wa misitu kwa mujibu wa sheria.
Katika risala ya wilaya ya Mufindi kuhusu siku ya upandaji miti kiwilaya iliyowasilishwa na Afisa Ardhi na Maliasili wilaya ya Mufindi, Jeswald Ubisimbali amesema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi imekuwa ikiwashirkisha wananchi wake katika ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo kwa lengo la kutekeleza mkakati wa taifa wa kupunguza umasikini miongoni mwa jamii (MKUKUTA). Aidha, ameeleza kuwa lengo kuu la Halmashauri ni kupanda miti zaidi, kuhifadhi mazngira na maliasili zote zilizopo na kuziendeleza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Akiongelea ukuzaji wa pato la Halmashauri, Ubisimbali amesema kuwa Halmashauri imejitita zaidi katika ununuzi wa Ardhi kwa madhumuni ya kupanda miti zaidi ili kukuza pato la Halmashauri na kuhifadhi mazingira kwa ujumla. Katika kuonesha umakini wa suala hilo, amesema kuwa Halmashauri imenunua ekari 1,607 katika kijiji cha Ukani na kufiksha jumla ya ekari 2,771 zinazomilikiwa na Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kwa lengo la kupanda miti.
Aidha, katika siku ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika wilaya ya Mufindi, zaid ya miti 1,300 ilipangwa chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Katika msimu wa mwaka 2012/2013 ilipandwa miti 33,445,960 ya aina mbalimbali sawa na hekta 20,903 katika wilaya ya Mufindi.
Ikumbukwe kuwa wilaya ya Mufindi ina eneo la Misitu la Hekta 203,791 ikiwa ni misitu ya hifadhi Hekta 57,031, misitu ya Miombo Hekta 80,012 na Hekta 66,748 misitu ya kupandwa.
=30=

SERIKALI KUWASAIDIA WACHIMBAJI HARAMU KUPATA AJIRA



Magdalena Nkulu, Shinyanga
Serikali mkoani Shinyanga imelaani na kukemea tabia ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya migodi kwa lengo la kuiba mchanga wa madini kwa kuwa ni kinyume cha sheria na hatari kwa maisha ya wananchi hao.
 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally N. Rufunga akishuhudia shimo hilo alipotembelea kuona shughuli za wachimbaji haramu katika mgodi wa Mwadui wilaya ya Kishapu jana, kushoto kwake ni Afisa Tarafa ya Mondo Bi.Maria Makoye na aliyesimama mbele ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu Wilson Nkhambaku.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally Nasoro Rufunga ametoa tamko hilo alipotembelea Mgodi wa Almasi Mwadui katika wilaya ya Kishapu jana na kujionea hali ya uchimbaji haramu unavyofanyika katika mgodi huo na pia kuzungumza na wachimbaji hao wanaojulikana kwa jina la Wabeshi, ambapo amewaahidi serikali itawasaidia kutafuta shughuli mbadala na kuwataka waachane na shughuli hiyo mara moja.

Mhe. Rufunga amewaambia wabeshi hao kuwa, serikali itahahakisha wanapata ajira halali kupitia viwanda vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa mkoani hapa, kuwakopesha mitaji kwa mfuko wa maendeleo ya vijana wa asilimia 5, pamoja na kufanya taratibu za kuwapatia maeneo madogo ili wachimbe kihalali iwapo wataacha na biashara hiyo.

Amewaambia kuwa, uchimbaji huo ni kuwaibia wawekezaji na kuwakwamisha kulipa mapato kwa serikali, kwani nchi inapata kodi kutoka kwa wawekezaji waliopata leseni halali ya uchimbaji, kodi ambayo inawanufaisha wananchi wenyewe katika shughuli za maendeleo.

Amewaasa kuacha kutumiwa na watu wenye uwezo kuhatarisha maisha yao kwa kigezo cha ugumu wa maisha na kusema serikali ya mkoa inawabaini watu hao na itawashughulikia muda mfupi. 

Kwa upande wao wachimbaji hao wamekiri mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa, ni kweli wanafahamu kazi hiyo si halali na wamemuahidi kuachana nayo kama watasaidiwa shughuli mbadala kwani wanafanya hivyo kujitafutia riziki kutoka na hali ngumu ya maisha na masharti ya mikopo kuwa ni magumu.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amewaagiza wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa Mwadui kwanza kutoa elimu kwa wananchi hasa vijana na kuwakataza kufanya uchimbaji haramu, kwani tabia hiyo imeshaota mizizi na kuonekana ni halali katika jamii hiyo, pamoja na kuwasidia vijana hao katika kuibua miradi kutokana na fedha zinazotolewa na mgodiwa Mwadui kila Mwezi. Vilevile, kuwa na uhusiano mzuri na mwekezaji kwa manufaa ya vijiji hivyo.

Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Elisha Nkhamba kusimamia uundwaji wa vikundi vya vijana ili wawezeshwe kufanya shughuli za kuwaiingiziakipato.

Mhe. Rufunga pia ameutaka uongozi wa Mgodi kuimarisha ulinzi katika eneo lao kwa kushirikia na Kamanda wa Polisi wa Mkoa. Amewapongeza na kuwataka kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya mgodi na jamii ya Mwadui kwa kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo na za kuwainua kiuchumi wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Nae Meneja Mkuu wa Mgodi wa Mwadui Arlen Loehmer ameishukuru serikali kwa ushirikiano na kusaidiana kujua na kutatua changamoto mbalimbali, na anaamini katika mahusiano haya mazuri kunaimarisha juhudi za uwekezaji.

Magdalena Nkulu,
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Shinyanga
0766-289802




 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally N. Rufunga akizungumza   na wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa Mwadui jana alipotembelea mgodini hapo kuona uchimbaji haramu unaofanywa na wananchi wa vijiji hivyo.kushoto kwake ni Meneja mgodi Bw. Arlen Loehmer na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu Wilson Nkhambaku