Sunday, January 26, 2014

DKT. ISHENGOMA APIGA MARUFUKU KUCHOMA MISITU



Serikali imepiga marufuku tabia ya wananchi kukata na kuchoma moto misitu mkoani Iringa ili kulinda misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. 
Marufuku hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya uzinduzi wa siku ya upandaji miti katika kijiji cha Mtili, wilaya ya Mufindi.
Dkt. Christine amesema kuwa juhudi za upandaji miti katika wilaya ya Mufindi ili ziwe endelevu ni lazima kukomesha tabia ya kukata na kuchoma miti. “Ndugu wananchi, ili juhudi hizi ziweze kuwa endelevu, natoa wito kwenu kuwa kuanzia sasa iwe ni mwiko, na aibu kuharibu miti na misitu, kwa kuichoma moto ovyo, kwa kuikata au kuifyeka ovyo, kuiharibu kwa kuishi ndani ya misitu. Kwa kufanya hivyo utakuwa umetenda kosa la jinai na unastahili kupewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria za misitu” aliongea kwa ukali Mkuu wa Mkoa. Amesema kuwa iwe tabia na utamaduni wa wananchi wa wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla kutunza miti iliyopandwa ili kuepuka janga la kuongezeka kwa mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, amewataka wananchi wote kuwa walinzi kwa kuwakamata na kuwaripoti wale wote watakao kiuka taratibu zilizopo za utunzaji wa misitu kwa mujibu wa sheria.
Katika risala ya wilaya ya Mufindi kuhusu siku ya upandaji miti kiwilaya iliyowasilishwa na Afisa Ardhi na Maliasili wilaya ya Mufindi, Jeswald Ubisimbali amesema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi imekuwa ikiwashirkisha wananchi wake katika ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo kwa lengo la kutekeleza mkakati wa taifa wa kupunguza umasikini miongoni mwa jamii (MKUKUTA). Aidha, ameeleza kuwa lengo kuu la Halmashauri ni kupanda miti zaidi, kuhifadhi mazngira na maliasili zote zilizopo na kuziendeleza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Akiongelea ukuzaji wa pato la Halmashauri, Ubisimbali amesema kuwa Halmashauri imejitita zaidi katika ununuzi wa Ardhi kwa madhumuni ya kupanda miti zaidi ili kukuza pato la Halmashauri na kuhifadhi mazingira kwa ujumla. Katika kuonesha umakini wa suala hilo, amesema kuwa Halmashauri imenunua ekari 1,607 katika kijiji cha Ukani na kufiksha jumla ya ekari 2,771 zinazomilikiwa na Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kwa lengo la kupanda miti.
Aidha, katika siku ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika wilaya ya Mufindi, zaid ya miti 1,300 ilipangwa chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Katika msimu wa mwaka 2012/2013 ilipandwa miti 33,445,960 ya aina mbalimbali sawa na hekta 20,903 katika wilaya ya Mufindi.
Ikumbukwe kuwa wilaya ya Mufindi ina eneo la Misitu la Hekta 203,791 ikiwa ni misitu ya hifadhi Hekta 57,031, misitu ya Miombo Hekta 80,012 na Hekta 66,748 misitu ya kupandwa.
=30=

No comments:

Post a Comment