Wednesday, November 13, 2013

BODI YA LIGI YAFUNGIA VIWANJA SABA



Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za mpira wa miguu.

Uamuzi huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi (Novemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa kwanza.
                               Boniface Wambura

Viwanja vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika kwanza ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji), na Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing rooms) havina hadhi).

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni mbovu), Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha (pitch ni mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya awali), Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu). 

Klabu ambazo timu zake zinatumia viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo ambapo ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo ili wafanye marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.

Kwa upande wa ripoti za mechi za VPL; Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga. Pia wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga baada ya gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi. 

Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kushambulia basi la wachezaji wa Tanzania Prisons baada ya mechi dhidi yao, na kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi.

Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu.

Beki wa Coastal Union, Hamad Khamis wa Coastal Union amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.

Mchezaji Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kupiga kelele wakati mgeni rasmi akisalimia timu na kukataa kupeana mkono na kamishna kwenye mechi dhidi ya Rhino Rangers, hivyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000.

Mtunza vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu, Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la ufundi wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya City kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa refa, hivyo suala lake litapelekwa katika Kamati ya Maadili.

Kocha Msaidizi wa Oljoro JKT, Fikiri Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi yao dhidi ya Ashanti United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin amepelekwa Kamati ya Maadili kwa kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.

Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar. 

Katika FDL, mchezaji Ally Mtoni wa Villa Squad amepigwa faini y ash. 200,000 na kufungiwa mechi tano. Kosa lake ni kujisaidia haja ndogo golini wakti wa mechi dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa mjini Mtwara.

Kamishna Paul Opiyo wa mechi ya FDL kati ya Villa Squad na Transit Camp kwa kutokuwa makini. Katika ripoti yake ameeleza kuwa Transit Camp ilichelewa kufika uwanjani, lakini hakusema ilichelewa kwa muda gani.

Kocha wa Polisi Dar es Salaam, Ngelo Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi Masi wamepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi tatu kila mmoja kwa kuongoza kundi la washabiki kumvamia refa wa mechi yao dhidi ya Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.

Pia Bodi ya Ligi imeagiza Polisi waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati waamuzi wanapigwa walikuwepo lakini hawakutoa msaada kwa wakati.

Kocha wa Friends Rangers, Kheri Mzozo amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kosa la kumtukana refa na kutishia kuhamamisha washabiki waingie uwanjani kufanya fujo kwenye mechi dhidi ya Villa Squad.

Naye Kocha msaidizi wa timu ya Transit Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi ya Friends Rangers.

Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili (Novemba 17 mwaka huu).

FUTURE TAIFA STARS vs TAIFA STARS UWANJANI KARUME
Timu za Taifa za Future Taifa Stars na Taifa Stars zinacheza kesho (Novemba 13 mwaka huu). Mechi hiyo ya kirafiki itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mechi hiyo ni maalumu kwa Benchi la Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na Kim Poulsen kuangalia wachezaji kumi kutoka Future Taifa Stars watakaoongezwa katika Taifa Stars tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Novemba 19 mwaka huu jijini Arusha.

Watazamaji 300 tu wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini leo (Novemba 12 mwaka huu). Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni kipa Ivo Mapunda wa Gor Mahia.

Boniface Wambura
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

KINANA KUANZA ZIARA YA SIKU 22 MIKOA YA MBEYA NA RUVUMA




Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana ataanza ziara ya siku 22 kwenye mikoa ya Ruvuma na Mbeya kuanzia tarehe 15/11/2013 mpaka mwanzoni mwa mwezi wa Desemba 2013. 

Huu ni mwendelezo wa ziara za kichama katika kuimarisha chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010,  kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi. 
                            Ndugu Abdulrahaman Kinana

Katika ziara zilizopita na vikao kadhaa vya chama  Serikali iliagizwa kushughulikia baadhi ya kero, na tumeshuhudia baadhi ya hoja hizo zikichukuliwa hatua. Baadhi ya hoja zilizoanza kushughulikiwa na Serikali ni pamoja na:-

1)         Hoja ya kufufua viwanda nchini.

Baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu, uchambuzi na vikao kadhaa vya CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi vilivyo binafsishwa havifanyi kazi kama ilivyokusudiwa na vingine kufungwa kabisa na kugeuzwa magodauni.

Pamoja na athari kubwa kwa uchumi wa nchi yetu, kufungwa na kutofanya vizuri kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira nchini kuwa kubwa. Hivyo Chama kiliagiza Serikali kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyo binafsishwa na hali yake kwa sasa na vile visivyofanya kazi kama ilivyokusudiwa vichukuliwe na Serikali na kutafuta njia sahihi ya kuvifufua upya.

Serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo kufanya tathmini na mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.

Tunajua zipo hatua kadhaa zimechukuliwa katika jitihada za kufufua viwanda vya kubangua korosho kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la soko na zao la korosho. Pia Serikali ipo katika hatua kadhaa za kushughulikia viwanda vingine nchini.

Tunaipongeza serikali kwa hatua hii muhimu ya kutekeleza agizo la chama. Tunaitaka serikali ikamilishe zoezi hili mapema iwezekanavyo ili nchi ifaidike na ufufuaji huu wa viwanda nchini.


2)         Changamoto kwa wakulima wa pamba

Katika ziara ya Katibu Mkuu mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa, alitumia muda mrefu kujifunza na kuzungumza na wakulima wa zao la pamba wa mikoa hiyo. Pamoja na tatizo kubwa la soko na bei ya pamba, pamekuwa  na changamoto kubwa ya mfumo unaosimamia zao la pamba ikiwemo upatikanaji wa pembejeo.

Hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na kukamua mafuta ya pamba. Tulishuhudia ujenzi wa viwanda kadhaa mjini Shinyanga, vingi vikijengwa na wawekezaji kutoka China.

Lakini wakati wa Bunge la juzi, Serikali imeamua kutoa ruzuku ya asilimia hamsini kwa mbegu bora za pamba ili kuwawezesha wakulima kumudu bei ya mbegu hizo na hivyo kuboresha zao la pamba nchini na maisha ya wakulima kuwa bora zaidi.(bei ya dukani kwa kilo moja ni Sh. 1,200/=; Serikali italipia
Sh.600/=).

Katika hili la mbegu bora na kilimo cha mkataba tunaitaka Serikali na hasa wakuu wa wilaya na mkoa kuacha mara moja kutumia nguvu kuwalazimisha wakulima kulima kwa mkataba na kutumia mbegu bora badala yake wawaelimishe na kuwashawishi badala ya kutumia nguvu.

Tunaipongeza Serikali kwa kuanza kuchukua hatua za kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya CCM ya namna ya kutatua matatizo yanayowakabili wakulima wa pamba nchini. Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya utatuaji wa changamoto hizo ili wakulima wa pamba wafaidike na uchumi wa nchi kukua kwa kasi nzuri.

3).        Migogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya   
ardhi

Katika ziara mbalimbali za Katibu Mkuu kwenye mikoa kama ya Morogoro, Njombe, Simiyu, Mara n.k. alishuhudia migogoro mingi sana juu ya wakulima, wafugaji na hifadhi  mbalimbali nchini. Hakuna shaka migogoro hiyo imegharimu sana maisha ya watu na mali zao na hata uchumi wa nchi yetu.

Chama kiliagiza migogoro hiyo kushughulikiwa mapema na kupata ufumbuzi wa kudumu. Chama kinalipongeza Bunge na hasa Wabunge wa CCM na Serikali yake kwa uamuzi wa kuunda Kamati teule ya Bunge kuchunguza na kutoa
mapendekezo ya hatua kadhaa za kuchukuliwa katika kufikia suluhisho la kudumu kwa migogoro hii.

Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa kamati teule ya Bunge ili kazi hii ya kamati iwe na matokeo mazuri yatakayosaidia kumaliza tatizo hili nchini. Wakati Kamati teule ya Bunge ikifanya kazi yake, tunawaomba wakulima na wafugaji kote nchini kutulia kusubiri matokeo ya kamati hii teule ya Bunge.

Hivyo basi,  ziara hii ya Katibu Mkuu imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha Chama, kukagua Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi. Tumeona jinsi ziara zilizotangulia zilivyokuwa na matokeo mazuri, tunaamini ziara hii pia itakua na matokeo mazuri.

Imetolewa na:-

Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
12/11/2013