Tuesday, November 26, 2013

RUCO YATOA WAWILI WA SHAHADA YA UZAMIVU KATIKA SHERIA, NI MARA YA KWANZA TANGU CHUO KIKUU CHA MT AUGUSTINO KIANZISHWE





KWA mara ya kwanza katika historia ya miaka 15 tangu kianzishwe, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) kimehudhurisha wahitimu wawili wa Shahada ya Uzamivu katika sheria (Ph.D).





Wahitimu hao, mtanzania Mandopi Kevin na mnaigeria Gbadebo Anthony Olagunju walitunukiwa shahada hizo juzi katika mahafali ya sita ya Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT cha Ruaha (Ruco), mjini Iringa.

Pamoja na madaktari hao wa sheria, MKUU wa Chuo Kikuu cha SAUT, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliwatunuku vyeti wahitimu wengine 1,777 wa astashahada, stashahada, shahada na shahada ya uzamili katika fani mbalimbali zinazotolewa Ruco.

Fani hizo ni katika sayansi za afya, ufundi sanifu madawa, sayansi ya kompyuta, sheria, biashara na utawala, sayansi ya ukutubi, elimu ya jamii na ualimu na sayansi ya lugha.

Kabla ya kuwatunuku vyeti hivyo, Askofu Ngalalekumtwa alisema “ulimwengu wa asa katika fani ya elimu ni wa ushindani mkubwa; haisaidii kulalamika kwamba elimu itolewayo katika vyuo vyetu ni duni wakati sisi wadau wa elimu hatufanyi juhudi yoyote katika kujikwamua kutoka katika hali hiyo.”

Alisema lipo tatizo la wahitimu wa vyuo vikuu kudhani kuwa elimu wanayopata ni kamilifu kumbe ni tone dogo katika bahari ya elimu na ni mwanzo wa njia ndefu ya kupambana na mazingira yanayowazunguka.

“napenda kuwaasa wahitimu waibweteke na kuridhika na kiwango cha alimu waliyopata; dunia ya sasa ni ya ushindani mkubwa. Mjenge dhana ya kutaka kujiendeleza zaidi kwani elimu haina mwisho,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Ruco, Dk Cephas Mgimwa alisema kutokana na mafanikio makubwa kinayozidi kuyapata, chuo chao kiko katika mchakato wa kuwa chuo kinachojitegemea.

“Tunataka kuwa chuo kikuu kinachojitegemea nje ya vyuo vya SAUT, naomba niwahakikishie mababa Askofu na wadau wengine wote kwamba tumejidhatiti na tupo tayari kujitegemea,” alisema.

Alisema adidu za rejea katika kufikia azma hiyo zinatekelezwa na kwamba hivisasa wanasubiri mamlaka inayohusika (TCU) iwakague pamoja na kupitia machapisho ya sera za chuo, kumbukumbu  mbalimbali na miundombinu.

Alisema chuo hicho na vingine vinavomilikiwa na makanisa havipendelewi bali vinapendwa kwasababu vinafanya kazi kwa faida na maendeleo ya Taifa.

Habari hii kwa hisani ya BONGO LEAKS

=30=