Friday, May 25, 2012



SENSA YA WATU NA MAKAZI KUTELA MAENDELEO
MUFINDI
Sensa ya Watu na Makazi inaumuhimu sana katika kutathmini utekelezaji wa mipango mikubwa ya maendeleo inayolenga kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Iringa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kijiji cha Igomaa, Wilaya ya Mufindi.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 ina umuhimu wa kipekee kwa sababu inalenga kutekeleza mipango ya kupunguza umasikini nchini. Amesema “Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 ina umuhimu wa kipekee kwani mbali ya kutimiza malengo ya kawaida, takwimu zitakazokusanywa katika Sensa hiyo zitatumika katika kutathimini utekelezaji wa mipango yetu mikubwa ya maendeleo ambayo ni Mpango wa kupunguza umasikini na kukuza uchumi Tanzania (MKUKUTA, na Mpango wa kukuza uchumi Zanzibar (MKUZA)”.

Amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012 manufaa yake ni makubwa sana katika mipango ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa na kusaidia kufanya mipango sahihi ya maendeleo kulingana na mahitaji halisi sambamba na kuweka uwiano mzuri wa matumizi ya rasilimali kulingana na idadi ya watu katika Mkoa.

Akiongelea maandalizi ya Sensa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa umekuwa ukichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linafanikiwa kwa ufanisi. Amezitaja hatua hizo kuwa ni uhakiki na utengaji wa maeneo madogo madogo ya kuhesabia watu na uhamasishaji wa ushiriki wa jamii katika Sensa.

Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake katika Mkoa wa Iringa ambapo unatarajiwa kukagua, kuzindua, kufungua na kuweka mawe ya msingi miradi 48 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,867,759,277.
=30=


MUFINDI

Wananchi wa Mkoa wa Iringa wamefahamishwa kuwa wanawajibu wa kuenzi misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa iliyoifanya nchi iwe na amani na utulivu jambo linalowawezesha wananchi kutekeleza shughuli za kujiingizia kipato kwa ufanisi mkubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akitoa taarifa ya mkoa wa Iringa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kijiji cha Igomaa wilayani Mufindi.


Dkt. Christine amesema kuwa “watanzania tunao wajibu wa kuwaenzi waasisi wa Taifa letu na kwa kuweka misingi mizuri ambayo imeendelea kulifanya Taifa letu kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine katika kudumisha amani, umoja wa kitaifa na mipango mizuri ya maendeleo. Hatuna budi kudumisha na kuendeleza tunu hizi kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu”.


Akiongelea mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wa iringa unaendelea na jitihada za kuhamasisha wananchi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kwa kutumia mpango wa polisi jamii na ulinzi shirikishi. 



Amesema kuwa Mkoa wa Iringa umeendelea kuendesha misako mbalimbali mijini na vijijini kwa malengo ya kuvunja vijiwe vya wauzaji wa dawa za kulevya na kukamata wamiliki wa mashamba ya bangi na kuyateketeza.  “Katika mapambano haya tayari jumla ya kesi 52 kati ya mwaka 2011 na 2012 za kupatikana na dawa za kulevya zimefikishwa mahakamani ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa” amesema Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Serikali ya Mkoa imeendelea kutoa elimu juu ya uanzishaji wa vikundi vya uzalishaji mali na kuhamasisha vijana kujihusisha na michezo mbalimbali ili kuepukana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya ukiwa ni mkakati kulitokomeza kabisa tatizo hili la dawa za kulevya.


Akiongelea mapambano dhidi ya rushwa, Dkt. Christine amesema kuwa mapambano dhidi ya rushwa katika Mkoa wa Iringa yanafanyika kwa kuzingatia Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na rushwa awamu ya pili. Ameseme “mkakati huu unalenga kuongeza ufahamu kwa wananchi juu ya rushwa, kuongeza wigo wa mapambano dhidi ya rushwa, kuboresha huduma za jamii na kuongeza uwezo wa ushiriki wa sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali katika mapambano hayo”.


Amesema kupitia mpango huo Mkoa wa Iringa umeweza kusambaza jumla ya machapisho 16,488 yenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa ambayo yamekuwa yakigawiwa katika semina 77, mikutano ya hadhara 27 na mijadala ya shule za sekondari.


Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake Mkoani Iringa ambapo utapitia jumla ya miradi ya maendeleo 48, kuweka mawe ya msingi, kukagua, kuzindua na kufungua miradi hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 1,867,759,277.

=30=



WAKUU WA WILAYA WAAPISHWA IRINGA

IRINGA

Wakuu wapya wa Wilaya Mkoani Iringa wametakiwa kuwa karibu na wananchi katika wilaya zao ili kuweza kuzifahamu changamoto zinazowakabili na kuwahudumia kwa ufanisi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma muda mfupi baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za Mufindi, Iringa na Kilolo.

Dkt. Christine amesema kuwa ili kuweza kuwahudumia vizuri wananchi ni lazima kuzifahamu changamoto zinazowakabili wananchi husika. Amesema ili kuzifahamu changamoto hizo ni lazima kuwa nao karibu na baada ya kuzifahamu changamoto hizo na rahisi kuweza kuwahudumia kwa urahisi na ukaribu.

Amesema kuwa mkoa wa Iringa unasifika kwa ustadi katika shughuli za kilimo kwa mazao ya chakula na biashara ambazo ndizo shughuli kuu za uchumi. Amesema kuwa kilimo kinaajiri karibu asilimia 85 ya wakazi wa mkoa wa Iringa na kuchangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la mkoa.

Akiongelea matarajio yake kwa wakuu hao wa wilaya, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kwa kipindi mkoa umekuwa na upunguwa wa wakuu wa wilaya, hivyo uteuzi huo utawezesha kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Iringa.

Akielezea matarajio yake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amesema kuwa ushirikiano alioupata kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Mufindi ulimuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na jukumu lakekama Mkuu wa Wilaya kuwa rahisi. Amesema anatarajia ushirikiano huo kuendelea kwa kasi zaidi ili wote kwa pamoja waweze kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa Rais Jakaya Kikwete aliteua wakuu wapya wa Wilaya tarehe 09 Mei, 2012 na mkoa wa Iringa kupata wakuu watatu wa wilaya. Wakuu hao na wilaya zao katika mabano ni Evarista Njilekiro Kalalu (Mufindi), Dkt. Leticia Moses Warioba (Iringa) na Gerald John Guninita (Kilolo). 
=30=

UKUAJI WA UCHUMI UZINGATIE UHIFADHI WA MAZINGIRA
IRINGA

Serikali imeihimiza dhana ya ukuaji wa uchumi kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali yasiyoathiri mazingira kwa kuzingatia athari za muda za muda mrefu kwa mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal alipokuwa akihutubia uzinduzi wa jukwaa la uchumi wa kijani uliofanyika katika ukumbi wa St. Dominic mjini Iringa.

Dkt. Bilal amesema “matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali hauna manufaa katika dunia ya leo. Watu wanapaswa kuachana na mbinu za kizamani za ukuaji wa uchumi wa matumizi shinikizi ya rasilimali, ambapo maendeleo yamekuwa yakigharimu mazingira; badala yake, wanapaswa kufuata mbinu mpya ambazo tija huongezwa kwa kutumia na kusimamia maliasili kwa ufanisi zaidi”.

Amesema kuwa shughuli za kujiletea uchumi lazima ziangalie kwa makini athari za muda mrefu kwa mazingira na haja ya kuhifadhi urithi wa nchi kwa manufaa ya vizazi kilichopo na vizazi vijavyo. Amesema kuwa uchumi wa kijani ni muhimu kwa sababu huchochea ukuaji wa uchumi, mapato na ajira. Amesisitiza kuwa hii ndiyo aina ya uchumi inayoleta maendeleo ya kiuchumi ya muda mrefu na yanayotoa fursa kwa wananchi wengi.

Makamu wa Rais amesema kuwa katika sekta mbalimbali kama kilimo, ujenzi, misitu na usafiri, uchumi wa kijani ndio uchumi unaotengeneza ajira nyingi kuliko ajira zilizopo katika hali ya kawaida. Ametolea mfano wa sekta ya uvuvi, “uchumi wa kijani utalazimisha kushuka kwa mapato na ajira katika muda mfupi na wa kati ili kujazia hifadhi asilia, lakini hali hii hubakia ya muda mfupi na baadaye sekta hukua na kutoa tija kubwa wananchi”.

Dkt. Bilal amesema kuwa ili jitihada za maendeleo ziweze kufanikiwa nchini, lazima zielekezwe katika uhalisia wa mambo. Amesema “zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wan chi hii huishi vijijini. Hivyo, jitihada madhubuti za kupunguza umasikini na kuleta maendeleo lazima zilenge wakazi na uchumi wa vijijini ili kuwa na matokeo mazuri”.

Amesema kuwa upo uhusiano mkubwa wa wananchi masikini wa vijijini na mazingira yao kwa sababu huishi karibu na mazingira ya asili na hutegemea rasilimali za ardhi, maji na misitu kwa maisha yao.

Katika salamu za Mkoa wa Iringa zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa zoezi la kupanda miti na kuhakikisha inatunzwa ni mkakati shirikishi unaowashirikisha wananchi na taasisi mbalimbali. Kila Halmashauri inazingatia agizo la serikali la kuwa na uzalishaji wa miche ya miti kwenye vitalu vyake isiyopungua miche 1,500,000 kila msimu. Amesema kwa miaka mitano iliyopita Mkoauliweka malengo ya kupanda miti 197,910,000 na kufanikiwa kupanda miti 266,871,064.

Akiziainisha changamoto zinazokwamisha juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira amezitaja kuwa ni uchomaji moto ovyo, ukataji miti ovyo bila kufuata kanuni na kulima kwenye vyanzo vya maji na miteremko mikali.

Jukwaa la uchumi la kijani linaratibiwa na taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwa na uchumi endelevu nchini.
=30=

WAFANYAKAZI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA JUHUDI 

MUFINDI
Serikali Mkoani Iringa imewataka Wafanyakazi Mkoani hapa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na nidhamu ili kujiletea maendeleo katika kazi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika katika ngazi ya Mkoa Wilayani Mufindi.

Dkt. Christine amesema ili mfanyakazi yeyote aweze kuheshimika katika jamii, inampasa kuelewa umuhimu wa nafasi yake katika jamii, kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na nidhamu na kujituma kazini kwake, bila ya kufuatwafuatwa”. Kwa waajiri amesema “mwajiri anao wajibu mkubwa wa kutoa vitendea kazi bora, kujali usalama wa wafanyakazi na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wafanyakazi wake”.

Akiongelea wajibu wa vyama vya wafanyakazi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa vyama hivyo vinawajibika kuwaelimisha wananchama wao ambao ni watumishi wa Serikali, taasisi, mashirika mbalimbali, wafanyakazi wa hoteli na wafanyakazi wengine juu ya kuheshimu nafasi waliopewa katika jamii na kuelewa msingi wa ufanyakazi bora wa umma. Amesema miongoni mwa wajibu huo ni kuelimisha juu ya sheria, taratibu na kanuni za kazi, kufanya kazi kwa hekima na uadilifu, kuheshimu maadili na taaluma, kutunza siri za serikali, kutekeleza wajibu wake kama wafanyakazi,pasipo upendeleo.

Akiongelea kero dhidi ya wafanyakazi, Dkt. Christine amesema kuwa serikali imeendelea kutatua kero nyingi zinazowakalibi wafanyazi katika utendaji kazi wao. Amesema “hapo awali kulikuwepo kero nyingi zinazohusu wafanyakazi, kama vile ucheleweshaji wa mishahara, ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu, kero ya kutopata mikopo kwenye benki”. Amesema kuwa hali hiyo kwa sasa imerekebishwa na wafanyakazi ni mashahidi. Aidha, amekiri kuwa maboresho haya hayajafikia kiwango cha asilimia mia moja.

Akiongelea Sensa ya watu na makazi, Dkt. Christine amewataka wafanyakazi wote kushiriki kutoa taarifa na elimu kwa wananchi dhidi ya sensa ya watu na makazi itakayofaanyika tarehe 26 Agosti, 2012. amesema kuwa lengo la Sensa hii ni kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsi, mahali wanapoishi, hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. Amesema sensa hiyo ni muhimu sana kwa sababu inalenga kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Mkakati wa Kupunguza Umasikini na kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA) na mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA). Napenda kuwahamasisha wananchi wote kujitokeza kwa wingi na kutoa taarifa zao kwa usahihi ili kufanikisha zoezi hilo.

Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yalianza katika karne ya 19 huko ulaya wakati wafanyakazi kwenye viwanda vya nguo na vingine walipoamua kudai maslahi na mazingira bora ya kufanyia kazi. Maandhimisho hayo mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘mshahara duni, kubwa kubwa na mfumuko wa bei ni pigo kwa wafanyakazi’.
 =30=  



SERIKALI KUTATUA KERO ZA WAFANYAKAZI 

MUFINDI

Serikali itaendelea kutatua kero za wafanyakazi ili kuwawezesha wanyakazi kufanya kazi katika mazingira bora na rafiki ili wazidishe ufanisi katika utendaji kazi wao.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa Mkoa wa Iringa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika kimkoa mjini Mafinga wilayani Mufindi.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa hapo awali zilikuwepo kero nyingi zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi, nakuzitaja kero hizo kuwa ni ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu, ucheleweshaji wa mishahara, na kero ya kutokupata mikopo katika benki. Amesema “hali hii sasa imerekebishwa na wafanyakazi ni mashahidi wa haya ninayoyazungumza, ingawa maboresho haya hayajafikia kiwango cha asilimia mia moja”. Amesema “kero inayoendelea hivi sasa ni suala la mishahara duni iliyo na kodi kubwa ambayo haiendani na hali ngumu kiuchumi inayoikabili nchi yetu.  Serikali inalitambua hilo na inaendelea kulifanyia kazi ili kuipatia ufumbuzi wa kudumu”.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa lazima wafanyakazi watambue nafasi yao katika jamii na kuwataka kufanya kazi kuwa juhudi, nidhamu na maarifa na kujituma kazini pasipo kufuatwafuatwa. Amesema kufanya hivyo kutawafanya wafanyakazi kuheshimika katika jamii. Amewataka waajiri kuendelea kutoa vitendea kazi bora na kutoa kujali usalama wa wafanyakazi wote ili kuboresha utendaji kazi wao.

Aidha, Dkt. Ishengoma amevitaka vyama vya wafanyakazi kuwajibika kuwaelimisha wanachama wao ambao ni watumishi wa Serikali, Taasisi, Mashirika mbalimbali, Watumishi wa hotelini na Majumbani pamoja na Wafanyakazi wengine juu ya kuheshimu nafasi waliyopewa katika jamii na kuelewa msingi wa utumishi bora kwa Umma.

Akiongelea mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya, Mkuu wa Mkoa amewataka wafanyakazi wote kushiriki katika kuhamasisha na kuwaeleza wananchi ili washiriki katika mchakato huo kwa kutoa elimu. Amesema “napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuwa huru kutoa maoni yenu kwa Tume itakapopita na kukusanya maoni yenu”.

Chimbuko la maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniali lilianza karne ya 19 huko ulaya na mwaka huu Kauli Mbiu ya Maadhimisho haya ni ‘maisha duni, kodi kubwa na mfumuko wa bei ni pigo kwa wafanyakazi’.

=30=





WAANDISHI HABARI HAMASISHENI SENSA

Mkuu wa Mkao wa Iringa amewataka waandishi wa habari, viongozi wa dini na wazee mashuhuri Mkoani Iringa kuhamasisha wananchi juu ya uelewa wa Sensa ya watu na Makazi ili waweze kujitokeza na kuhesabiwa hapo Agosti 26, 2012.

Wito huo ameuto Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari, viongozi wa dini, wazee mashuhuri na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu uhamasishaji wa wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi leo alipokutana nao katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa kutokana na umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi nchini, nafasi za makundi mbalimbali ni muhimu sana katika kusaidia kutoa elimu na hamasa, amesema “hamna budi kufahamu kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ndizo zitakazoiwezesha Serikali kutambua hali halisi na mahitaji halisi ya huduma zilipo katika maeneo yenu hivyo kuingizwa katika mipango ya maendeleo ya taifa”.

Amesema kutokana na msingi huo makundi hayo aliyokutana nayo yanapaswa kuhamasisha wananchi ili waweze kuhesabiwa na kusisitiza kuwa kuhesabiwa huko iwe ni mara moja tu kuwezesha takwimu zitakazokusanywa ziwe sahihi na za uhakika. Amesema kuwa iwapo takwimu zote zitakazokusanywa zitakuwa sahihi, huo ndio utakuwa utimilifu wa takwimu za Sensa kitaifa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mambo muhimu ya kuzingatia wakati ya kuhamasisha wananchi ni pamoja na tarehe ya Sensa, umuhimu wa Sensa na yatakayojiti wakati wa zoezi la kuhesabu watu.
Akiwatoa hofu wananchi kuhusu mawazo potofu dhidi ya zoezi la Sensa, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Iringa, Fabian Fundi amesema kuwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi halihusiani kabisa na hofu walizonazo wananchi. Amesema “ni muhimu sana kuwatoa hofu wananchi kwa kuwaelimisha kuwa zoezi la Sensa halihusiani kabisa na hofu au imani walizonazo”.

Fundi, amesisitiza kuwa wananchi wawe huru kutoa taarifa watakazoulizwa katika dodoso na kuwahakiihsia kuwa taarifa hizo zitatumika kwa mambo ya kitakwimu pekee na kwa usiri mkubwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka amesema amewataka wananchi kuwatoa watoto wote na watu wenye ulemavu ili waweze kuhesabiwa na kuiwezesha Serikali kuangalia njia bora ya kuwahudumia vizuri zaidi. Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya wanajamii kuwaficha watoto wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali kutokana na ulemavu walionao.
=30=