Friday, May 25, 2012


UKUAJI WA UCHUMI UZINGATIE UHIFADHI WA MAZINGIRA
IRINGA

Serikali imeihimiza dhana ya ukuaji wa uchumi kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali yasiyoathiri mazingira kwa kuzingatia athari za muda za muda mrefu kwa mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal alipokuwa akihutubia uzinduzi wa jukwaa la uchumi wa kijani uliofanyika katika ukumbi wa St. Dominic mjini Iringa.

Dkt. Bilal amesema “matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali hauna manufaa katika dunia ya leo. Watu wanapaswa kuachana na mbinu za kizamani za ukuaji wa uchumi wa matumizi shinikizi ya rasilimali, ambapo maendeleo yamekuwa yakigharimu mazingira; badala yake, wanapaswa kufuata mbinu mpya ambazo tija huongezwa kwa kutumia na kusimamia maliasili kwa ufanisi zaidi”.

Amesema kuwa shughuli za kujiletea uchumi lazima ziangalie kwa makini athari za muda mrefu kwa mazingira na haja ya kuhifadhi urithi wa nchi kwa manufaa ya vizazi kilichopo na vizazi vijavyo. Amesema kuwa uchumi wa kijani ni muhimu kwa sababu huchochea ukuaji wa uchumi, mapato na ajira. Amesisitiza kuwa hii ndiyo aina ya uchumi inayoleta maendeleo ya kiuchumi ya muda mrefu na yanayotoa fursa kwa wananchi wengi.

Makamu wa Rais amesema kuwa katika sekta mbalimbali kama kilimo, ujenzi, misitu na usafiri, uchumi wa kijani ndio uchumi unaotengeneza ajira nyingi kuliko ajira zilizopo katika hali ya kawaida. Ametolea mfano wa sekta ya uvuvi, “uchumi wa kijani utalazimisha kushuka kwa mapato na ajira katika muda mfupi na wa kati ili kujazia hifadhi asilia, lakini hali hii hubakia ya muda mfupi na baadaye sekta hukua na kutoa tija kubwa wananchi”.

Dkt. Bilal amesema kuwa ili jitihada za maendeleo ziweze kufanikiwa nchini, lazima zielekezwe katika uhalisia wa mambo. Amesema “zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wan chi hii huishi vijijini. Hivyo, jitihada madhubuti za kupunguza umasikini na kuleta maendeleo lazima zilenge wakazi na uchumi wa vijijini ili kuwa na matokeo mazuri”.

Amesema kuwa upo uhusiano mkubwa wa wananchi masikini wa vijijini na mazingira yao kwa sababu huishi karibu na mazingira ya asili na hutegemea rasilimali za ardhi, maji na misitu kwa maisha yao.

Katika salamu za Mkoa wa Iringa zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa zoezi la kupanda miti na kuhakikisha inatunzwa ni mkakati shirikishi unaowashirikisha wananchi na taasisi mbalimbali. Kila Halmashauri inazingatia agizo la serikali la kuwa na uzalishaji wa miche ya miti kwenye vitalu vyake isiyopungua miche 1,500,000 kila msimu. Amesema kwa miaka mitano iliyopita Mkoauliweka malengo ya kupanda miti 197,910,000 na kufanikiwa kupanda miti 266,871,064.

Akiziainisha changamoto zinazokwamisha juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira amezitaja kuwa ni uchomaji moto ovyo, ukataji miti ovyo bila kufuata kanuni na kulima kwenye vyanzo vya maji na miteremko mikali.

Jukwaa la uchumi la kijani linaratibiwa na taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwa na uchumi endelevu nchini.
=30=

No comments:

Post a Comment