Saturday, February 10, 2018

IRINGA KUCHOCHEA UTARII KARIBU KUSINI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa unatumia mkakati wa maonesho ya utalii karibu kusini kuchochea na kukuza utalii kwa ukanda wa kusini mwa Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa kwa Makamu wa Rais katika rest house ya NSSF Iringa mjini jana.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza
Masenza alisema “maonesho ya utalii kusini yanatumika kama mkakati maalum wa kufungua sekta ya utalii kwa ukanda wa kusini ambao umejaa fursa na vivutio vya kipee katika utalii. Mkoa wa Iringa ukiwa mratibu umeandaa mipango ya kuboresha wa maonesho haya kwa kutenga eneo la Kihesa Kilolo kama eneo maalum kwa ajili ya maonesho ya utalii kusini. Eneo hili litatumiwa na wadau wa utalii na wadau wa maendeleo kujenga miundombinu kwa ajili ya kuonesha huduma na bidhaa za sekta ya utalii”.

Idadi ya watalii waliotembelea vivutio vya utalii kwa mwaka 2015 walikuwa 8,112 kati ya hao watalii wa nje walikuwa 6,875 na watalii wa ndani walikuwa 3,072. Kwa mwaka 2016 jumla ya watalii 36,736 kati ya watalii hao watalii wa ndani walikuwa 22,280 na watalii wa nje walikuwa 14,456 alisema mkuu wa Mkoa.

Aidha, Mkoa kwa kushirikiana na wadau unaendelea kuvihifadhi na kuvitangaza vivutio hivyo ili kukuza utalii. Alisema kuwa Mkoa wa Iringa ambao ni kitovu cha utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini umeweza kuratibu kwa kuandaa maonesho ya utalii karibu kusini kwa miaka miwili mfululizo (mwaka 2016 na mwaka 2017).

Maonesho ya utalii karibu kusini hushirikisha mikoa ya nyanda za juu kusini ambayo ni Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Rukwa na Katavi.

Makamu wa Rais yupo katika ziara ya siku tano mkoani Iringa pamoja na mambo mengine atazingua mradi wa kuendeleza utalii ukanda wa kusini REGROW.
=30=

IRINGA YAJIVUNIA HIFADHI YA TAIFA RUAHA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa

Mkoa wa Iringa unajivunia hifadhi kubwa ya taifa ya Ruaha yenye upekee unaovutia watalii wa ndani na nje ya nchi kuitembelea.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa kwa Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan jana katika rest house ya NSSF mjini Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza

Masenza alisema kuwa Mkoa wa Iringa una hifadhi za taifa mbili hifadhi ya Taifa Ruaha na hifadhi ya Taifa ya Udzungwa. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ina ukubwa wa Kilometa za mraba 20,226. 

“Asilimia 38 ya eneo la hifadhi ya Ruaha ambayo ni sawa na Kilometa za Mraba 777 zipo katika Mkoa wa Iringa. Hifadhi ya Ruaha ni kubwa kuliko hifadhi zote za Tanzania na ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya ile ya Kafue iliyopo nchini Zambia” alisema Masenza. Aliongeza kuwa upekee wa hifadhi hiyo ni uwepo wa mwingiliano wa bioanuwai za kusini na kaskazini mwa Tanzania.

Akiongelea hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 1,990 ambapo asilimia 80 sawa na Kilometa za mraba 1,596.8 za eneo lote la hifadhi ya Milima Udzungwa ipo katika Mkoa wa Iring alisema kuwa hifadhi hiyo ni hifadhi pekee iliyopo katika milima ya tao la mashariki. 

“Hifadhi hii ina hazina ya aina nyingi za mimea, ndege, vyura wa Kihansi na wanyamapori ambao hawapatikani katika sehemu nyingine yoyote duniani. Baadhi ya viumbe hao ni mbega mwekundu wa Iringa (Iringa red colobus monkey) na Sanje Crested mangabey” alisema Masenza.
=30=

IRINGA KINARA TUZO YA RAIS UTUNZAJI MAZINGIRA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa

Mkoa wa Iringa unatekeleza vizuri mwongozo wa tuzo ya Rais ya utunzaji wa mazingira na uhifadhi ya vyanzo vya maji na Manispaa ya Iringa kushika nafasi ya kwanza kwa Manispaa zote nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa kwa makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan aliye katika ziara ya siku tano mkoani Iringa jana.

Mkuu wa Mkoa, Amina Masenza

Masenza alisema kuwa Mkoa wa Iringa ulipokea na kutekeleza mwongozo wa tuzo ya Rais ya utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji. 

“Katika mwaka 2015 Manispaa ya Iringa ilishika nafasi ya pili, mwaka 2016 ilishika nafasi ya kwanza kwa Manispaa zote Tanzania na mwaka 2017 ilishika nafasi ya tatu kwa Manispaa zote Tanzania” alisema Masenza.

Akiongelea zoezi la upandaji miti na uhifadhi wa mazingira, mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Mkoa kwa kushirikiana na wadau wa maliasili umeweza kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti na uhifadhi wa mazingira. Aliyataja mafanikio yaliyopatikana kuwa nikuvuka lengo la upandaji miti 55,000,000 kwa msimu 2016/2017 na kupanda miti 56,108,532. 

Katika zoezi hilo miti 47,766,366 sawa na asilimia 86.84 ilipona. Juhudi nyingine alizitaja kuwa ni kufanya oparesheni maalum ya kubaini na kuondoa wavamizi na mifugo katika hifadhi ya jamii ya Mbomipa wilayani Iringa. Alisema kuwa oparesheni ilifanyika chini ya kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa ilikamata watuhumiwa 38 wakiwa na mifugo 2,067 na kesi 6 zilifunguliwa mahakamani.

“Halmashauri zote Mkoani Iringa zimetakiwa kuendelea kudhibiti maeneo yote ya hifadhi yasiingizwe mifugo na pia kuendelea kutambua na kupiga chapa mifugo katika maeneo ya Halmashauri ili kuweza kudhibiti mifugo inayoingia bila kufuata taratibu” alisema Masenza.
Kuhusu shindano la usafi wa mazingira lililohusisha halmashauri za majiji, miji na wilaya kwa mwaka 2014, katika ngazi ya Manispaa zote Tanzania, Manispaa ya Iringa ilishika nafasi ya kwanza kitaifa na wilaya ya Mufindi ilishika nafasi ya pili kitaifa wakati kijiji cha Ifunda kikishika nafasi ya kwanza kitaifa.
=30=