Thursday, September 12, 2013

WATAHINIWA DARASA LA SABA WAPUNGUA IRINGA




Na Charles Amulike
Idadi ya watahiniwa wanaotarajia kufanya mtihani wa darasa la Saba mkoani Iringa imepungua kwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana 2012 kutoka wanafunzi 24,342 mpaka kufikia 23,148 kwa mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Joseph Mnyikambi, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kwa mwaka 2013.

Mnyikambi amesema kuwa jumla ya wanafunzi 23,148 tayari wamesajiliwa kufanya mtihani huo wa darasa la saba kwa mwaka huu 2013. Ameongeza kuwa kati ya watahiniwa hao wavulana 10,752 na wasichana 12,396. Akiongelea idadi ya watahiniwa hao kwa ulinganifu na mwaka jana, amesema “idadi ya watahiniwa waliofanya mtihani mwaka jana 2012 ni kubwa kuliko ya mwaka huu 2013”. Amefafanua kuwa mwaka jana jumla ya watahiniwa ilikuwa 24,342 waliofanya mtihani wa kumaliza darasa la saba. Kati yao wavulana walikuwa 11,484 na wasichana walikuwa 12,858.

Mnyikambi amesema kuwa idadi ya wanafunzi waliopungua kwa mwaka huu wa 2013 ni 1194 kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na mwaka jana 2012.

Akiongelea maandalizi ya kufanyika kwa mtihani huo, Mnyikambi amesema “maandalizi yamekamilika, ikiwa ni pamoja vyumba vya kufanyia mtihani huo na madawati ya kutosha wanafunzi wote wanaotarajiwa kufanya mtihani huo”. Amesema katika kukomesha vitendo vya udandanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, Mkoa umejipanga vizuri kuhakikisha kila mtahiniwa anakaa kwenye dawati lake peke yake. Ameongeza kuwa  wasimamizi wa mitihani wamepatiwa semina ili kuhakikisha wanadhibiti udanganyifu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza katika mitihani hiyo.

Afisa Elimu Mkoa amesema kuwa tayari vifaa vya mitihani vimefika na vimepelekwa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa. Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza Mkoani hapa.
=30=ᘖ

No comments:

Post a Comment