Monday, December 27, 2010

WATOTO YATIMA WANAHITAJI UPENDO NA HURUMA …!
Jamii imekumbushwa kuwa watoto yatima wanahitaji upendo, huruma na kutimiziwa mahitaji yao ya msingi kama watoto wengine.

Kauli hiyo imetolewa na Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa viti maalumu (CCM) kupitia mkoa wa Iringa jana katika chakula maalumu alichokiandaa kwa ajili ya watoto yatima wa kituo cha Daily Bread Life Ministries kilichopo Mkimbizi nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.

Mhe. Ritta Kabati, Mbunge viti Maalumu (CCM) akiwa na mtoto yatima
ambaye jina lake halikufahamika mara moja katika chakula cha mchana
alichowaandalia watoto yatima wa kituo cha Daily Bread Life Ministries cha
Mkimbizi, Manispaa ya Iringa

Mheshimiwa Kabati amesema kuwa jamii lazima ikumbuke kuwa watoto yatima na wenye mahitaji maalumu ni wanajamii kama walivyo watoto wengine na wanahitaji upendo, huruma na kutimiziwa mahitaji yao ya msingi ya kila siku kama chakula, malazi, mavazi, matibabu na elimu. Jamii haiwezi kujivua jukumu hili lenye pande mbili; upande wa kiroho kama tendo la huruma na mapendo na upande wa kimwili kama kuhakikisha unatunzwa na kuuwezesha kutimiza majikumu yake ya kibinadamu.

Mheshimiwa Kabati ameelezea madhumuni ya kuandaa chakula hicho cha mchana kwa watoto yatima kuwa ni kukaa na kufurahi pamoja na watoto hao akiamini ni jambo jema hasa katika majira haya ya sikukuu. Amesema ‘kukaa na kufurahi pamoja ni jambo jema, na sisi ndiyo baba zenu na mama zenu”.

Watoto wa kituo cha makao ya watoto yatima wakijichana vilivyo

Mheshimiwa Kabati pamoja na mengine ametoa zawadi mbalimbali za Noeli kwa watoto yatima kama mablanketi, nguo, masweta, sabuni, dawa za meno, miswaki, biskuti pia aliahidi kukinunulia seti ya Luninga kituo hicho ili watoto waweze kujifunza na kufuatilia mambo yanavyokwenda ndani na nje ya nchi.

Nae Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Gervas Ndaki alisema kuwa suala la elimu kwa watoto yatima ni suala la msingi sana hivyo jamii inalazimika kuliangalia kwa jicho la karibu. Aidha aliahidi kuwalipia ada watoto wawili (2) waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza hadi watakapomaliza kidato cha nne (4).

Mhe. Ritta Kabati akikabidhi zawadi ya ndoo ya sabuni miongoni mwa zawadi nyingine

Mhe. Ritta Kabati akiwa amembeba mtoto mchanga aliyeokotwa muda jalalani muda mfupi baada ya kuzaliwa
Katika risala ya kituo hicho iliyosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa kituo, Swiga James amesema kuwa kituo chake kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo michango ya shule, gharama za matibabu kuwa kubwa kwa watoto na ubovu wa miundombinu hususani barabara kufikia kituo hicho. Aidha, alishauri iandaliwe sheria kali ya kuwadhibiti wazazi wanaokwepa majukumu yao kwa watoto.

Kituo cha Daily Bread Life Ministries kilianzishwa mwaka 2002 na kilianza rasmi kupokea watoto Aprili 2004 kutoka ustawi wa jamii na kina watoto 36, wakike 20 na wakiume 16.


No comments:

Post a Comment