Thursday, September 12, 2013

IRINGA YAKOMESHA UDANGANYIFU KATIKA MITIHANI




Na. Bruno Machary
Serikali Mkoani Iringa imejidhatiti kufanikisha mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi unafanyika pasipo kuwepo na vitendo vya udanyanyifu.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Mwl. Joseph Mnyikambi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake ili kujua jitihada zilizochukuliwa na Mkoa katika kukabiliana na vitendo vya udanganyifu kwa walimu na wanafunzi wakati wa mtihani huo.

Akitoa ufafanuzi, Mnyikambi amesema kuwa wamejitahidi kutoa semina kwa walimu ili kuhakikisha  kuwa mtihani huo unafanyika kwa haki na amani pasipo kuwepo kwa vitendo vyovyote vya udanganyifu kwa wanafunzi wala walimu watakaosimamia mtihani huo. Kwa upande wa wanafunzi, amesema kuwa kila mwanafunzi atatumia dawati lake ili kuondoa mianya inayoweza kushawishi udanganyifu.

Akiongelea upande wa maandalizi ya mtihani huo, amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na  vifaa vyote vimeshafika Mkoani na vimeshapelekwa kila Halmashauri. “Vifaa vyote vinavyohusu masuala ya mtihani huo vimeshafika Mkoani hapa na vimeshapelekwa katika wilaya zote” amesema Mnyikambi.

Afisa Elimu huyo amesema kuwa katika mwaka wa masomo 2013  idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani huo imepungua kwa jumla ya wanafunzi 1194 ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2012. Kwa mwaka 2012 kulikuwa na watahiniwa 24,342 wakati mwaka huu wapo watahiniwa 23,148.

Mtihani huo unaotarajiwa kuanza kufanyika siku ya jumatano ya tarehe 11/9/2013 kitaifa, utajumuisha shule za msingi 466 za  Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa una jumla ya wilaya tatu ambazo ni Iringa, Mufindi na Kilolo, zenye jumla ya Halmashauri nne.
=30=

No comments:

Post a Comment