Wednesday, May 18, 2011

WIZARA YAANZISHA MPANGO WA KUENDELEA UTALII NCHINI

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanzisha mpango kamambe wa kuendeleza sekta ya utalii nchini utakaohusisha rasilimali za utalii zilizopo.

Hayo yamesemwa na Deograsias Mdamu, Afisa Utalii Mkuu kutoka Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, wakati akiwasilisha mada juu Sera ya Utalii na Mkakati ya kuendeleza Utalii nchini katika kikao cha Kamati ya Uchauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo leo.

Mdamu amesema “mpango huu ni mkakati unaoelekeza jinsi ya kuendeleza utalii nchini kwa kuzingatia rasilimali za utalii, maendeleo ya mifumo mbalimbali, vivutio vikuu vya utalii, masoko ya utalii, taaluma ya kuhudumia sekta ya utalii, sera, sheria, taratibu na miongozo iliyopo”.

Akifafanua mikakati ya kukuza utalii, Mdamu ameitaja kuwa ni kuendeleza mazao mapya ya utalii, kutafuta masoko mapya na kuimarisha masoko ya zamani pia kuimarisha utafiti katika eneo la utafiti.

Vilevile, kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji baina ya Wizara na Taasisi za Serikali zinazohusika na maendeleo ya sekta ya utalii pamoja na kuongeza mapato ya utalii kutokana na leseni za biashara, mikataba ya uwekezaji na kodi.
Mikakati mwingine ameitaja kuwa ni pamoja na kuhimiza ubora wa huduma kwa utalii kama afya, benki, usalama na mawasiliano.

Kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi na haki za binadamu katika sekta ya utalii.
Kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya sekta za uzalishaji wa bidhaa na huduma nyingine zitumikazo na sekta ya utalii na kupanua ushiriki wa sekta hizi katika biashara za utalii.

Afisa Utalii Mkuu, ameongelea pia mtawanyiko wa sekta ya utalii na kusema kuwa sekta hiyo ni kubwa na imetawanyika katika makundi anuai huku kundi kubwa likiwa ni wafanyabiashara wenye mitaji midogo huku kundi dogo sana likiwa ndilo lenye wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa.

Aidha, ameupongeza mkoa wa Iringa kwa kuwa na Maafisa Utalii katika Halmashauri zake ukiwa ni mkoa pekee wenye maafisa hao katika kila Halmashauri na kuahidi kuwapa ushirikiano stahiki katika kuiendeleza sekta ya utalii nchini.

Sekta ya utalii huchangia katika kuzalisha ajira, mapato ya fedha za kigeni na maendeleo katika sehemu mbalimbali mijini na vijijini.    

No comments:

Post a Comment