Wednesday, May 18, 2011

AHADI ZA DR. JK ZAANZA KUTEKELEZWA NA TANROADS IRINGA

Ofisi ya Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa (TANROADS) imeanza utekelezaji wa ahadi za Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010 kuhusu sekta ya barabara mkoani hapa.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Iringa,
Mhandisi Paul Lyakurwa

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ahadi hizo katika kikao cha Bodi ya Barabara ya mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, meneja wa wakala wa barabara (TANROADS), Mhandisi Paul Lyakurwa amesema ujenzi wa barabara ya Iringa-Mtera-Dodoma yenye urefu wa Km 260 kwa kiwango cha lami umeanza.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika sehemu tatu za Iringa-Migoli (Km 95.2), Migoli- Fufu (Km 93.2) na Fufu- Dodoma (Km70.9).
Aidha, mkataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Iringa-Migoli (95.2)  ulisainiwa tarehe 13 Januari, 2011 kati ya TANROADS na Mkandarasi M/S China Sichuan International Cooperation Co. Ltd kwa gharama ya Tshs. 84,216,378,355.50 wakati muda wa kukamilisha kazi ni miezi 35. Sehemu ya Migoli-Fufu (93.2) mkataba ulisainiwa tarehe 13 Januari, 2011 kati ya TANROADS na Mkandarasi M/S China Sichuan International Cooperation Co. Ltd kwa gharama ya Tshs. 73,612,329,958.67 wakati muda wa kumaliza kazi ni miezi 35. Sehemu ya Fufu-Dodoma (Km 70.9) mkataba ulisainiwa tarehe 13 Januari, 2011 kati ya TANROADS na Mkandarasi M/S China Communication Construction Co. Ltd kwa gharama ya Tshs. 64,327,389,129 wakati muda wa kukamilisha kazi ni miezi 27 na mkandarasi anaendelea na ujenzi wa kambi.

Kuhusu kukamilisha ujenzi wa barabara ya Njombe- Makete yenye urefu (Km 109) kwa kiwango cha lami, Meneja wa TANROADS amesema kuwa ujenzi wa Km 9.5 kati ya Mang’oto na Tandala ndani ya Wilaya ya Makete umekamilika. Aidha, ujenzi wa Km 2 maeneo ya Mang’oto unaendelea na unatarajia kukamilika ndani ya mwaka wa fedha 2010/2011.

   Aseri Msangi, Mwenyekiti (wa pili kulia), Gertrude Mpaka, Katibu (wa pili kushoto), Dr. Binilith Mahenge, Makamu Mwenyekiti (wa kwanza kulia) na Deo Sanga, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa (wa kwanza kushoto)

Akiongelea mpango uliopo kwa mwaka 2011/ 2012 Meneja huyo ameutaja kuwa ni kufanya upembuzi yakinifu, usanifu pamoja na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara yote kwa kiwango cha lami kama fedha zitapatikana.

Kuhusu maeneo korofi amesema yataendelea kuimarishwa kwa changarawe ili barabara iendelee kupitika kipindi chote cha mwaka.

No comments:

Post a Comment