Tuesday, November 17, 2015

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHE. AMINA MASENZA KATIKA UZINDUZI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA KUNAWA MIKONO DUNIANI, SIKU YA CHOO DUNIANI NA WIKI YA USAFI TANZANIA KATIKA KIJIJI CHA UHAMBINGETO, HALMASHAURI YA WILAYA YA KILOLO MKOANI IRINGA NOVEMBA 14, 2015




Katibu Tawala Mkoa,
Wakurugenzi wa Halmashauri,
Viongozi wa Serikali na Taasisi mbalimbali
Waandishi wa Habari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kujumuika na kushiriki kikamilifu katika Siku ya  Uzinduzi wa Wiki ya Usafi wa Mazingira Kimkoa inayofanyika hapa kijiji cha Uhambingeto.

Napenda kutoa pongezi maalum kwa wananchi wa Uhambingeto kwa kufika hapa kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huu wa maadhimisho haya kimkoa. Kufika kwenu ndiyo ufanisi wa shughuli hii na mafanikio yake. Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru washirika wetu wa maendeleo kwa michango na misaada yao adhimu. Marafiki zetu wametuunga mkono katika juhudi zetu za kuboresha huduma za usafi wa mazingira mijini na vijijini. Ninawaomba, wawakilishi wa mashirika waliopo hapa, wazipokee na kuzifikisha shukrani zetu za dhati, kwa wakuu wa mashirika yao.

 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza

Umuhimu wa Maadhimisho

Ndugu Wananchi;
Maadhimisho ya Siku ya kunawa mikono Duniani, Siku ya choo Duniani na wiki ya Usafi Tanzania, ambayo yameanza rasmi mwaka 2013, ni ushahidi wa umuhimu ambao Serikali na wananchi wanaoutoa katika kuboresha usafi wa mazingira nchini. Kwa miaka mingi tarehe 19 Novemba dunia imekuwa ikiadhimisha  siku ya choo duniani na 15 oktoba siku ya kunawa mikono kwa sabuni Duniani. Mwaka 2013 Umoja wa Mataifa ulipitisha tarehe 19 Novemba kuwa ni siku rasmi ya maadhimisho ya Choo Duniani kutokana na ukweli kuwa kati ya malengo yote ya maendeleo ya milenia ndio lengo pekee ambalo liko nyuma kiutekelezaji. Katika mwaka huo huo Tanzania ilipitisha rasmi wiki ya tarehe 13 hadi 19 Novemba kuwa ni wiki ya Usafi Tanzania. Tanzania huadhimisha kwa pamoja katika wiki hii Siku ya Kunawa Mikono Duniani na Siku ya Choo Duniani. Kwa mwaka huu Maadhimisho haya Kitaifa yanafanyika Mkoani Njombe.

Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii ili iweze kuchukua hatua katika kukabiliana na changamoto za kukosa huduma za choo bora na uboreshaji wa usafi wa mazingira kwa ujumla, ambapo mkazo huwekwa katika uhamasishaji wa matumizi ya vyoo bora, unawaji wa mikono kwa sabuni, njia sahihi za kutibu na kutunza maji ya kunywa majumbani, na usafishaji wa maeneo yanayotuzunguka.

Maadhimisho haya pia yanatoa nafasi kwa wadau kujadili mafanikio yaliyopatikana na matatizo yaliyopo katika kuendeleza usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo bora na kuyatafutia ufumbuzi. Kwa pamoja, kama taifa, tunapata fursa ya kufanya tathmini ya tulikotoka, tulipo sasa na kuainisha malengo na mipango yetu kwa siku zijazo.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho

Ndugu Wananchi; Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ina ujumbe mzito sana: Kipindupindu  Hakikubaliki, Zuia Maambukizi Mapya, Zingatia Usafi wa Mazingira”. Ni ukweli ulio wazi kuwa bila kuchukua jitihada za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira yetu janga hili la kipindupindu litaendelea kuwepo na watu wataoendelea kupoteza maisha na kupunguza nguvu kazi.

Kwa kutambua ukweli huo kuhusu usafi wa mazingira, katika siku ya leo na katika wiki yote hii tafakuri zetu tuzielekeze kwenye kutafuta mikakati na mbinu za kuhakikisha kuwa tunaboresha usafi wa mazingira katika maeneo yetu. Naomba tutambue kuwa mkakati wowote kwa ajili hiyo hauna budi ujielekeze katika kufanya mambo yafuatayo:
1.  Kujenga vyoo bora na kuvitumia
2.  Kunawa mikono kwa maji safi na sabuni katika nyakati tano muhimu,
3.  Kusafisha maeneo yanayotuzunguka,
4.  Kuboresha usafi binafsi na kuaacha tabia ya kutupa taka ovyo.


Ndugu Wananchi;
Huduma duni za usafi wa mazingira zinachangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa milipuko ya magonjwa ya kuhara ikiwemo kipindupindu na kusababisha vifo ambavyo vingeweza kuzuilika. Katika mlipuko wa Kipindupindu unaoendelea nchini takriban watu 106 wameshapoteza maisha.   Idadi hii ni kubwa na pengo kubwa kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Kwa mujibu wa Shirika la UNICEF na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Ugonjwa wa kuhara bado ni miongoni mwa magonjwa makuu matano yanayochangia katika vifo kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano nchini Tanzania. Takwimu zinaonyesha kwamba moja ya tatu ya vifo vya watoto vinavyotokea ndani ya mwezi wa kwanza wa maisha ya watoto vinatokana na maambukizi au magonjwa ya kuhara yanayosababishwa na:
·        Ukosefu wa maji safi na salama,
·        Mazingira machafu na kutozingatia tabia za usafi.
·        Madhara mengine yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama,
·        Mazingira machafu na kutozingatia tabia za usafi ni kudumaa (mtoto kuwa na kimo kifupi kisichoendana na umri na kuathiri ukuaji)
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 53 ya watoto chini ya miaka mitano mkoani Iringa wamedumaa.
Kunawa mikono kwa sabuni ni mojawapo ya njia rahisi na yenye gharama nafuu kuzuia maambukizi. Njia hii hupunguza uwezekano wa kupata maambukizi kwa 50% na matumizi ya choo bora hupunguza kwa 32%. Takwimu za utafiti uliofanywa na shirika la UNICEF katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya zinaonyesha kuwa kaya zenye vyoo bora ni 23%, kaya ambazo zina vyombo vya kunawia mikono na sabuni ni 9%, uoshaji wa mikono baada ya kumhudumia mtoto ni 56%, uoshaji wa mikono kabla ya kuandaa chakula ni 2% na uoshaji wa mikono kabla ya kumlisha mtoto ni 18%.
Ndugu Wananchi;
Uboreshaji wa usafi wa mazingira na kuzingatia kanuni zake ndio ngao pekee ya kujikinga na janga hili kubwa la ugonjwa wa kipindupindu. 

Hatua Zilizochukuliwa na Serikali kukabiliana na changamoto

Ndugu Wananchi;

Baadhi ya jitihada zinazofanywa na Serikali kukabili changamoto za usafi wa mazingira nchini ni:

(i) Utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira ambayo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye vyoo bora na kuboresha usafi wa mazingira katika maeneo ya mikusanyiko, maeneo ya barabara kuu na kwenye Taasisi. Kwa mkoa wa Iringa kupitia Kampeni hii jumla ya mafundi 156 kutoka vijiji 156 wamefundishwa jinsi ya kujenga vyoo bora kwa gharama nafuu. Nawaomba tuwatumie mafundi hawa ili tuweze kujenga vyoo bora vijijini kwetu.

Nimesikia kuwa Mkoa wa Iringa tayari kuna kata 33 zinatekeleza Kampeni hii, naomba Wakurugenzi wa Halmashauri wapanue utekelezaji huu katika kata nyengine kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato. Aidha, utekelezaji wa Kampeni hii kwa mkoa wetu hauridhishi kulingana na malengo kama tulivyosikia katika Taarifa ya Mganga Mkuu wa Mkoa. Hivyo nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kila Halmashauri inafikia malengo kwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Kampeni hii na kuwachukulia hatua watendaji wasio wajibika.  Katika utekelezaji wa Kampeni hii ili mwisho wa siku kila wananchi awe na Choo bora.


(ii) Kusimamia sheria zilizopo za usafi wa mazingira na kuwachukulia hatua wale wote wanaoenda kinyume na sheria hizi zikiwemo sheria ndogo za Halmashauri na vijiji.

Hivyo nachukua nafasi hii kuaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu Sheria hizo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka na kuifanya Kampeni hii isifanikiwe.


Ndugu  Wananchi;
Usafi wa Mazingira ni jukumu letu sote , na ni jukumu endelevu rai yangu kwenu ni kuendelea kufanya usafi katika maeneo yote yanayotuzunguka na kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo bora ya vyoo kwa afya ya kaya na Taifa kwa ujumla.  Lazima tuzingatie Kanuni zote za Usafi kama tunavyoelekezwa na wataalamu wa Afya. 

Baada ya kusema haya natamka kuwa uzinduzi wa maadhimisho siku ya kunawa Mikono Duniani, Siku ya Choo Duniani, na wiki ya Usafi wa Mazingira Tanzania imezinduliwa rasmi,

Aksanteni kwa kunisikiliza.



HAPA KAZI TU!!

No comments:

Post a Comment