Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mwenge
wa Uhuru utatembelea miradi ya maendeleo 40 yenye thamani ya shilingi
24,427,360,696.40 mkoani Iringa na kutoa ujumbe maalum wa mwaka 2018.
Akitoa
taarifa ya ujuo wa Mwenge wa Uhuru kwa wananchi kupitia vyombo vya habari vya
mkoa wa Iringa, mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema kuwa Mwenge wa
uhuru utatembelea, kagua, kuzindua, kufungua na kuweka mawe ya msingi, jumla ya miradi 40. Aliongeza kuwa miradi
hiyo ina thamani ya shilingi 24,427,360,696.40.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akiongea na waandishi wa Habari |
“Miradi hiyo inatoka sekta za elimu (10), afya (7), maji (4) maliasili
(1), kilimo (5), viwanda viwili (2) uvuvi (1) na mapambano dhidi ya rushwa (4).
Gharama za miradi hiyo zimetokana na michango ya wananchi shilingi 1,251,610,850.00,
Serikali kuu shilingi 8,638,969,449.40, Halmashauri shilingi 253,564,461.00 na wadau
wa maendeleo shilingi 14,283,215,936.00”
Akiongelea
ujumbe wa mwenge wa uhuru mwaka 2018, mkuu wa mkoa wa Iringa alisema kuwa Mwenge
wa Uhuru utatoa ujumbe maalumu na ujumbe wa kudumu katika maeneo yote ambako
utakimbizwa. Ujumbe maalumu wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2018 ni: ‘Elimu ni Ufunguo wa Maisha; Wekeza sasa kwa
maendeleo ya Taifa letu’. Ujumbe
huu unalenga kutilia mkazo umuhimu wa uwekezaji katika elimu unaofanywa na
serikali pamoja na Wananchi ikiwa ni
mkakati madhubuti katika kupiga vita umaskini na kujenga taifa lenye maendeleo
ya viwanda alisema mkuu wa mkoa.
Pamoja
na kutoa ujumbe mahususi, Mwenge wa Uhuru utaendelea kuhimiza mapambano dhidi
ya UKIMWI chini ya kauli mbiu isemayo ‘mwananchi jitambue; pima afya yako sasa’. Ujumbe
mwingine aliutaja kuwa ni mapambano dhidi ya Malaria chini ya kauli mbiu
isemayo ‘Shiriki kutokomeza Malaria kwa
manufaa ya Jamii’
Ujumbe
mwingine ni mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya chini ya kauli mbiu
isemayo ‘Tuwasikilize na kuwashauri
watoto ili wasitumie dawa za kulevya’ na Mapambano ya kutokomeza Rushwa
chini ya kauli mbiu isemayo:-‘Kataa
Rushwa- Jenga Tanzania’.
Mwenge
wa Uhuru utakimbizwa mkoani Iringa kwa siku tano na kukabidhiwa mkoani Njombe
tarehe 28/5/2018.
=30=