Tuesday, December 11, 2012



Text Box:             MAFUNZO HAMASA YA KIBIASHARA
NA
           UIMARISHAJI WA BIASHARA NDOGO

Walengwa:  Vijana waliomaliza vyuo/shule; Mtu yoyote anayependa
                   kujiajiri; Mfanyabishara anayemiliki biashara ndogo.
Aina ya Bidhaa
Idadi ya siku
Ada
Usindikaji chakula: Tomato sauce, Chilli sauce, Jam, Mbilimbi, Mangle pickle, Cakes/Snacks, Juice, Peanut butter, unga wa lishe
Siku 12
150,000/-
Sabuni za unga, vipande na maji [za harufu tofauti]
Siku 10
130,000
Utengenezaji wa Batiki
 Siku 12
120,000
Utengenezaji wa ‘Tie and dye’
Siku 6
80,000
Kutengeneza mishumaa ya aina na harufu mbalimbali
Siku 6
75,000
Ufugaji kuku wa kienyeji , mayai na wa nyama kibiashara
Siku 5
70,000
Bidhaa za mikono [urembo aina tofauti]
Siku 10
100,000
Wasiliana nasi simu Na. 0754 787 133   NA  0754 072 869

RC AKEMEA WIZI YA VIFAA VYA UJENZI




Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amekemea vikali wizi wa vifaa katika ujenzi wa barabara unaoendelea katika maeneo mengi ya Mkoa wa Iringa na kuwataka wananchi kuimarisha ulinzi shirikishi na kuwabaini wale wote wanaohusika na uhalifu huo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kauli hiyo ameitoka katika kijiji cha Nyang’oro kilichopo katika Wilaya ya Iringa alipotembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma kwa kiwango cha lami na kuzungunza na wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi huo.

Dkt. Christine amesema kuwa Serikali ya awamu ya nne inatengeneza barabara kwa fedha nyingi lengo likiwa ni kuharakisha kuwaletea maendeleo wananchi wake. Amesema kuwa jitihada hizo za Serikali zimekuwa zikikwamishwa na baadhi ya watu wasio na mapenzi mema na nchi niongoni mwao ni wananchi wanaozunguka ujenzi wa mradi huo wa barabara kwa kufanya vitendo vya wizi wa mafuta na vifaa mbalimbali vya ujenzi kama saruji. Amesema “wizi si kitu kizuri, wizi unaupa sifa mbaya mkoa wetu na nchi yetu, ninyi wezi mnaonisikia tafadhali acheni wizi huo mara moja” alisisitiza Dkt. Christine.

Amewataka wananchi kufanya mikutano ya kuwabaini wezi hao ili waweze kufikishwa katika vyombo vya dola na kusisitiza ulinzi shirikishi. Akionesha masikitiko yake na kwa ukali alisema kuwa kama watafumbia macho vitendo hivyo ni dhahiri kwamba ujenzi huo wa barabara utakapokamilika wezi hao watawaibia wananchi wenyewe.

Aidha, amewataka vijana kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali kwa ajili ya kufanya kazi za maendeleo. Amesema kwa kuwa mvua zinanyesha, ni vizuri vijana hao wakajikita katika kilimo.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa- Dodoma kwa kiwango cha lami (Km 260) Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa, Mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema kuwa mradi huo unaofadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Africa (ADB), Shirika la Misaada la Japan (JICA) na Serikali ya Tanznaia umetekelezwa kwa asilimia 35 na muda uliotumika ni miezi 16 sawa na asilimia 47 ya muda wote wa utekelezaji wa mradi huo na Mkandarasi yupo nyuma kwa miezi minne. Amesema ili kuongeza kasi ya utekelezaji, katika sehemu ya kwanza ya (Lot 1) Iringa- Migori (Km 95.2) Mkandarasi anatumia timu nne. Amezitaja timu hizo kuwa ya kwanza imeanzia Nyang’oro kuelekea Izazi, timu ya pili imeanzia Izazi kuelekea Migori, timu ya tatu inafanya kazi ya kupasua miamba eneo la mlima Nyang’oro wakati timu ya nne inafanya kazi kati ya Nyang’oro na Igingilanyi.

Sehemu ya pili (Lot 2) Migori- Fufu Escarpment (Km93.8) kiwango cha utekelezaji wake hadi Septemba, 2012 kilikuwa wastani wa asilimia 40 wakati muda uliotumika ni miezi 18 sawa na asilimia 50 na Mkandarasi yupo nyuma kwa miezi mitatu.

Aidha, Sehemu (Lot 3) Fufu Escarpment – Dodoma (Km 70.9), amesema kuwa sehemu hiyo inasimamiwa na Meneja wa Wakara wa barabara Mkoa wa Dodoma.
Akielezea changamoto katika mradi huo, Mhandisi Rwesingisa amesema kuwa wizi wa vifaa vya ujenzi kama mafuta na saruji umekuwa ukikwamisha maendeleo ya utekelezaji wa miradi kwa kuwa Makandarasi wamekuwa wakitumia muda mwingi kujaribu kupambana na wizi huo badala ya kutumia muda huo kufanya kazi za mradi. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni migomo ya wafanyakazi wakidai nyongeza ya mishahara na posho. Nyingine ameitaja kuwa ni upasuaji wa miamba yam awe mlima Nyang’oro kwa ajili ya kupanua barabara umbali wa Km. 15 na ukosefu wa maji katika eneo hilo.
=30=

Sunday, December 9, 2012

MATUKIO YA MAADHIMISHO YA MIAKA 51 YA UHURU KATIKA PICHA

 Baadhi ya viongozi walioshiriki maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara kimkoa

 Baadhi ya viongozi na maafisa waandamizi walioshiriki maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara kimkoa katika tarafa ya Mahenge Wilayani Kilolo

  Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Dickolagwa (wapili kushoto) akisaini kitabu cha wageni


 Viongozi wakitafakari kwa kina juu ya miaka 51 ya Uhuru wa tanzania Bara

Ritta Kabati, Mbunge (CCM) Viti Maalum akisaini kitabu cha wageni (kulia) Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Dickolagwa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati) akisaini kitabu cha wageni kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Joseph Muhumba na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Helman Msua (kulia)


Baadji ya wananchi waliojumuika katika maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara

UHURU UENDE SAMBAMBA NA UWAJIBIKAJI NA UZALENDO




Wananchi na viongozi Mkoani Iringa wametakiwa kuongeza uwajibikaji na uadilifu kwa kutanguliza mbele uzalendo na maslahi ya Taifa katika shughuli zao za kila siku za kujiletea maendeleo yao na maendeleo ya Taifa.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Iringa wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa katika Tarafa ya Mahenge Wilayani Kilolo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati) akisaini kitabu cha wageni, kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Josheph Muhumba na Helman Msua, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Wilaya ya Kilolo (kulia)

Dkt. Christine amesema “ni ukweli usiopingika tukiwajibika ipasavyo, tukiwa waadilifu, na wazalendo kuanzia kwenye kaya hadi Taifa tutalitumikia Taifa na kupata maendeleo yanayohitajika. Hivi vitu vitatu ni msingi mkubwa sana wa maendeleo ya nchi yetu, hivyo kila mmoja inampasa kutimiza kauli mbiu hii”.

Akiongelea mafanikio yaliyopatikana mkoani Iringa tokea Uhuru, Mkuu wa Mkoa ameyataja kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa pato la Mkoa na pato la mkazi. Amesema mwaka 1961 pato la Mkoa lilikuwa ni shilingi 5,693,000 na wastani wa pato la mtu kwa mwaka lilikuwa shilingi 103. Amesema kwa mwaka 2011 pato la Mkoa limekuwa na kufikia shilingi 1,985,708,000 wakati pato la mkazi limeongezeka na kufikia shilingi 1,225,503.
Katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kumekuwapo na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato hayo kwa mwaka 2011/2012 mapato ya Halmashauri yaliyokusanywa ni shilingi 9,357,013,391 kutoka vyanzo vya ndani, kukiwa na ongezeko la shilingi 9,355,366,502 yakilinganishwa na mapato ya mwaka 1961/1962 ya shilingi 1,646,889.
Kwa upande wa kilimo ambacho ni shughuli kuu ya kiuchumi, Dkt. Christine amesema kuwa Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza eneo linalolimwa kutoka Hekta 305,208.65 mwaka 1961/1962 hadi kufikia Hekta 411,116 mwaka 2011/2012. Amesema kuwa sambamba na kuongeza eneo hilo, pia elimu juu ya kilimo bora imeendelea kutolewa kwa wakulima na jumla ya mashamba darasa 1,603 yameanzishwa wakati wakulima 49,075 wamepatiwa mafunzo kwa vitendo kupitia mashamba hayo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 2011. Amesema katika kuhakikisha kuwa elimu inawafikia wakulima wengi, Mkoa umeanzisha vituo vya rasilimali watu wa kilimo katika kata 17.

Amesema kuwa Serikali imeendelea kuhimiza matumizi ya mbolea katika kilimo ili kuwawezesha wakulima kupata mazao mengi na bora. Amesema Mkoa wa Iringa umeweza kuongeza matumizi ya mbolea toka tani 16,826 na tani 300 za mbegu hadi kufikisha tani 42,250 za mbolea na tani 3,142 za mbegu kwa mwaka 2011.

Katika salamu zake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Joseph Muhumba, amesema kuwa matunda ya Uhuru wa Tanzania Bara ni mengi na katika wilaya ya Kilolo wanayachukulia kuwa ni heshima kubwa na kuipa uzito mkubwa. Amesema kuwa ili heshima hiyo iendelee kuenziwa, ni lazima wananchi kufanya kazi kwa bidii, kutunza amani na utulivu vilivyopo katika Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla. Muhumba ambaye pia ni diwani wa Kata ya Image amesema kuwa Uhuru utaendelea  kumhamasisha kila mwananchi kuongeza juhudi katika kufanya kazi halali za kujiletea maendeleo yake binafsi ya maendeleo ya ujumla.  

Akiwasilisha Taarifa fupi ya maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru na maendeleo yaliyopatikana katika wilaya ya Kilolo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Helman Msua, amesema kuwa pamoja na Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 2002 bado imepiga hatua sana katika nyanza mbalimbali. Akitolea mfano juhudi za kukuza kilimo kupitia matumizi ya zana bora za kilimo, amesema mwaka 2002 Wilaya yake ilikuwa na matrekta makubwa 41 na hadi kufikia mwaka 2002 matrekta hayo yameongezeka hadi kufikia 52. Amesema kuwa vyama vya ushirika vimeongezeka toka 15 mwaka 2002 hadi kufikia 54 mwaka 2012.

Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara inaadhimishwa nchini kote ikiongozwa na kauli mbiu isemayo “uwajibikaji, uadilifu na uzalendo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu”.
=30=