Sunday, November 12, 2017

WABABA IRINGA WATAKIWA KUSHIRIKI MAKUZI NA MAENDELEO YA WATOTO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wakina baba mkoani Iringa watakiwa kushiriki kikamilifu katika makuzi na maendeleo ya watoto ili kujenga jamii familia imara isiyokuwa na utapiamlo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza akipokuwa akizindua kampeni ya Mama Msosi Lishe katika bustani ya Manispaa ya Iringa jana.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza alimpatia uji mtoto Pricila Mgaya katika uzinduzi wa Kampeni ya Mama Msosi Lishe
Mheshimiwa Masenza alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dr John Magufuli inatambua umuhimu na kuwekeza katika masuala ya lishe nchini. 

“Huo ni mojawapo ya mkakati wa kufanikisha azma ya Serikali kufikia uchumi wa kipato cha kati na viwanda ifikapo 2025. Baraza la Umoja wa Mataifa liliweka azimio la kuwa kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2025 ni miaka ya kuchukua Hatua katika kutekeleza masuala ya lishe” alisema mheshimiwa Masenza. 

Aliwataka wananchi wa mkoa wa Iringa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupambana na tatizo la utapiamlo.
Aidha, aliwataka kina baba kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa makuzi na maendeleo ya watoto pasipo kuwaachia kina mama peke yao. 

Alisema kuwa hiyo ni njia ya kukabiliana na tatizo la utapiamlo mkoani Iringa. Njia nyingine aliitaja kuwa ni uandaaji wa chakula vizuri kutokana na maeneo mengi huloweka mahindi muda mrefu na kupoteza madini na vitamin. Aliongeza kuwa ulishaji wa watoto wadogo uzingatie vyakula mchanganyiko, idadi ya milo na kiasi cha chakula cha kumpa mtoto kulingana na umri kuanzia kipindi mtoto anapotimiza miezi 6 mpaka miaka miwili. 

Vilevile, aliwataka kina mama wajawazito kuanza mapema kliniki ya uzazi ili kupata huduma muhimu. Alizitaja huduma hizo muhimu kuwa ni kupata vidonge vya kuongeza damu, kusaidia ukuaji bora wa mtoto, dawa za minyoo, kuzuia Malaria na VVU.

Katika maelezo ya awali ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, yaliyotolewa na Katibu Tawala msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Nuhu Mwasumilwe alisema kuwa changamoto kubwa katika Mkoa wa Iringa ni uelewa mdogo katika jamii wa masuala ya lishe. Changamoto hizo alizitaja kuwa ani uandaaji wa chakula hasa ugali kwa kutumia mahindi yaliolowekwa kwa muda mrefu  maarufu kama ‘kiverege’ husababisha madini na vitamini zote kupotea. 

Changamoto nyingine ni watoto wadogo kulishwa milo ya watu wazima isiyozingatia vyakula mchanganyiko na ushiriki mdogo wa akinababa katika ufuatiliaji wa makuzi na maendeleo ya mtoto hivyo kumwachia mama majukumu yote. Na wakina mama wajawazito kuanza kliniki ya uzazi kwa kuchelewa.

Alisema kuwa changamoto hizo ziliifanya Ofisi ya Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau kuandaa shindano la Mama Msosi Lishe litakalohusisha wanawake watakao andaa chakula bora cha familia. Aliongeza kuwa katika uandaaji huo, watapimwa uelewa wao juu ya umuhimu wa lishe bora, usafi wa mazingira yanayomzunguka na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Kampeni ya Mama Msosi Lishe mwaka 2017 inaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Mama Msosi lishe’. Chimbuko lake ni kupambana na utapiamlo hasa udumavu kutokana na Mkoa wa Iringa kuwa miongoni mwa Mikoa 5 ya Tanzania yenye kiwango kikubwa cha udumavu, kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya afya (TDHS, 2015/2016) ukiwa na asilimia 42 ya udumavu.
=30=

MKOA WA IRINGA WAADHIMISHA SIKU YA KISUKARI KWA MAZOEZI YA VIUNGO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- Iringa
Wananchi wa mkoa wa Iringa wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili kuondokana na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari.

Kauli hiyo ilitolewa na mratibu wa Mkoa kwa magonjwa yasiyoambukizwa Dr. Tatu Mbotoni alipokuwa akielezea umuhimu wa mazoezi katika uwanja wa kumbukumbu ya Samora mjini Iringa katika mazoezi maalum ya viungo katika maadhimisho ya siku ya kisukari duniani jana.


Dr. Mbotoni alisema “mazoezi ya leo tarehe 11 Novemba, 2017 yamefanyika ngazi ya mkoa kuadhimisha siku ya kisukari duniani kwa mkoa wetu wa Iringa. Nichukue nafasi hii kuwataarifu kuwa tarehe 18 Novemba, 2017 tutafanya zoezi la upimaji wa afya hasa ugonjwa wa kisukari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kisukari duniani”. 

Alisema kuwa wananchi watatangaziwa eneo zoezi hili litakapofanyika baada ya taratibu za kiutawala kukamilika.

Alisema kuwa ugonjwa wa kisukari ni kati ya magonjwa yasiyoambukiza unaosababishwa na mfumo wa maisha usio wa kiafya. Mifumo hiyo aliitaja kuwa ni unene uliopitiliza na uzito mkubwa. 

“Ni muhimu kufanya mazoezi ili kupunguza uzito na mafuta hatarishi mwilini vitu ambavyo visipothibitiwa vinaweza kusababisha ugonjwa wa kisukari” alisisitiza Dr. Mbotoni.

Mazoezi maalum ya viungo kwa mkoa wa Iringa yamefanyika kuadhimisha siku ya kisukari dunuani yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Wanawake na kisukari, haki yetu ya afya bora ya baadae’. 

Mazoezi hayo yamehudhuriwa na mamia ya wakazi wa Manispaa ya Iringa na viunga vyake pamoja na watumishi kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi wakiongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa.
=30=  

Thursday, November 2, 2017

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA MKUU WA MKOA KATIKA KATA YA NDULI

MATUKIO KATIKA PICHA ZIARA YA MKUU WA MKOA KATIKA KATA YA NDULI

MENEJA UWANJA WA NDEGE IRINGA APONGEZWA NA MKUU WA MKOA



Na Mwandishi Maalum, Iringa

Meneja wa kiwanja cha ndege cha Iringa amepongezwa kwa kutatua matatizo ya jamii inayouzunguka uwanja wa ndege wa Iringa.

Pongezi hizo zilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mhe Amina Masenza alipokagua ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika shule ya msingi Nduli iliyopo pembeni mwa uwanja wa ndege wa Iringa katika kata ya Nduli.

Mhe Masenza alisema “pongezi nyingi kwa meneja wa uwanja wa ndege wa Iringa. Tukiwa na watumishi wa umma 10 kama meneja huyu, shule zote zingekuwa na vyoo bora na miundombinu madhubuti”. 

Alisema kuwa miundombinu bora inawafanya watoto kuipenda shule na walimu kuwahudumia vizuri wanafunzi kwa kuwafundisha kwa moyo. Aliutaka uongozi wa shule hiyo kuvitunza vizuri vyoo hivyo ili viweze kudumu na kuwahudumia wanafunzi wengi zaidi.

Katika taarifa ya mradi wa ujenzi wa choo matundu 10 ya wanafunzi iliyosomwa na mwl Erick Kadope, alisema kuwa shule ya msingi Nduli ilikuwa na vyoo ambavyo si rafiki kwa wanafunzi. 

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa, kutokana na hali ya choo kuwa si rafiki kwa wanafunzi wetu, kiasi cha kupelekea hofu ya kupatwa na magonjwa ya mlipuko, hivyo meneja wa uwanja wa ndege wa Iringa, bi Hana Kibopile alichukulia uzito wa kipekee ili kunusuru afya za watoto ili wafurahie masomo yao. Aliamua kutafuta mfadhili ambaye ni mdau mkubwa wa maendeleo katika mkoa wa Iringa, anatoka kampuni ya Makota farm” alisema mwl Kadope.    

Akiongelea ujenzi wa choo hicho, alisema kuwa ujenzi ulianza mwaka 2017 na umefikia 90% ikiwa imebaki kazi ya kuweka mabomba ya ndani na kupaka rangi. Alisema kuwa mradi huo umegharimu shilingi 28,000,000.

Ikumbukwe kuwa Shule ya msingi Nduli ilianzishwa mwaka 1969.
=30=


BENDERA NYEKUNDU NYUMBA ZISIZO NA CHOO MANISPAA IRINGA



Na Mwandishi Maalum, Iringa

Mkuu wa mkoa wa Iringa, mhe Amina Masenza ameiagiza halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuziwekea bendera nyekundu nyumba zote ambazo hazina vyoo bora na kuzipa muda maalum wa kujenga na kukamilisha vyoo hivyo.

Agizo hilo alilitoa katika shule ya msingi Nduli baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa vyoo bora na usafi wa mazingira ya halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa robo ya kwanza Julai-Septemba, 2017.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza

Mhe Masenza alisema kuwa halmashauri ya Manispaa haina sababu ya kuwa na nyumba isiyo na choo. “Sioni sababu ya halmashauri ya Manispaa kuwa na nyumba ambayo haina choo bora, kwa sabababu nyumba zote zinajengwa kwa ramani baada ya kutolewa kibali cha ujenzi kilichokubaliwa na bwana afya baada ya kujiridhisha kuwa mchoro umebainisha ujenzi wa choo bora” alisema mhe Masenza. 

Aidha, aliitaka Manispaa ya Iringa kuziwekea bendera nyekundu nyumba zote ambazo hazina vyoo bora na kuzipa muda maalum kukamilisha ujenzi wa vyoo na kaya zitakazoshindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zichukuliwe. Aliitaka Manispaa ya Iringa kuweka mkakati wa kukamilisha ujenzi wa vyoo kwa kaya ambazo hazina vyoo.

Wakati huohuo, mkuu wa mkoa alimtaka mkuu wa wilaya ya Iringa kutoa maelezo ya sababu zinazofanya baadhi ya nyumba katika Manispaa ya Iringa kutokuwa na vyoo.

Mkuu wa mkoa wa Iringa, alifanya ziara ya siku moja katika kata ya Nduli, Manispa ya Iringa kukagua hali ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo.
=30=

NGOs ZATAKIWA KUFANYA KAZI ZINAZOONEKANA



Na Mwandishi Maalum, Iringa
Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotaka kufanya kazi kuwahudumia wananchi mkoani Iringa yatakiwa kufanya kazi zinazoonekana na kupimika.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza alipokuwa akiongea na jumuiya ya shule ya msingi Nduli iliyopo katika Manispaa ya Iringa alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua hali ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo katika kata ya Nduli.

Mhe Masenza alisema kuwa mashirika yote yasiyo ya kiserikali yanayotaka kufanya kazi za kuwahudumia wananchi mkoani Iringa, lazima yaeleze kazi zitakazofanyika na ziwe zinazoonekana na kupimika. 

Alisema kuwa yapo mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakipata fedha kwa kusingizio cha kuwahudumia wananchi katika usafi wa mazingira lakini yamekuwa hayafanyi hivyo. Alisema kuwa anataka mashirika makini na yanayowajibika kwa wananchi na serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akiongelea hali ya usafi wa mazingira katika kata ya Nduli, mkuu wa mkoa alisema kuwa hali ya usafi wa mazingira hairidhishi. 

“Katika ziara hii tumejionea jinsi maeneo mengi yalivyotapakaa takataka, nichukue nafasi hii kuwaagiza watendaji wote, kusimamia ipasavyo zoezi la usafi katika maeneo wanayoyasimamia. Haipendezi kusimamiwa na viongozi katika kazi ambazo ni majukumu yenu ya kila siku” alisema mhe Masenza.
=30=