Sunday, November 1, 2015

IRINGA TAYARI KWA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE 2015



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umekamilisha maandalizi ya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2015 na mitihani yote imefikishwa vituoni.

Kauli hiyo ilitolewa na kaimu afisa elimu mkoa wa Iringa, Mwalimu Euzebio Mtavangu alipokuwa akiongelea maandalizi ya mitihani ya kumaliza kidato cha nne kwa mkoa wa Iringa ulionza leo nchini kote ofisini kwake.

Mwalimu Mtavangu alisema kuwa mkoa wa Iringa una jumla ya vituo 196 vya kufanyia mtihani huo. Alivitaja vituo hivyo kwa kila halmashauri kuwa ni halmashauri ya Manispaa ya Iringa (44), halmashauri ya wilaya ya Iringa (33), halmashauri ya wilaya ya Kilolo (49), halmashauri ya wilaya ya Mufindi (70) na mitihani yote imefikishwa katika vituo husika.

Akiongelea idadi ya wasimamizi, alisema kuwa mkoa unao jumla ya wasimamizi 527. Alisema kuwa kwa mujibu wa muongozo wa mitihani hiyo msimamizi mmoja anatakiwa kusimamia wastani wa watahiniwa 40. Aliongeza kuwa wasimamizi hao miongoni mwao ni walimu kutoka katika shule za mkoa wa Iringa. Utaratibu wa kuwapata wasimamizi hao ni pamoja na kuwafanyia upekuzi wa kina na kula kiapo cha kutunza siri kwa mujibu wa sheria Namba 3 ya mwaka 1970. Alisema kuwa semina kwa wasimamizi wa mitihni hiyo zilianza kutolewa kwa halmashauri zote kuanzia tarehe 28-30/10/2015.

Kaimu afisa elimu mkoa wa Iringa alisema kuwa jumla ya watahiniwa 15,818 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari mwaka huu. Mgawanyo wa watahiniwa hao katika halmashauri ni halmashauri ya Manispaa (4,785), halmashauri ya wilaya ya Iringa (3,368), halmashauri ya wilaya ya Kilolo (2,784) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi (4,881).
Akiongelea matarajio ya ufaulu katika mkoa, Mwl Mtavangu alisema kuwa mkoa unatarajia kufanya vizuri na kupindukia matarajio ya BRN ya 80%. Alisema kuwa matarajio hayo yanatokana na mkoa kuwa uliboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Sababu nyingine alizitaja kuwa ni wanafunzi wa masomo ya sayansi kufanya majaribio halisi baada ya kuwa na maabara za kutosha na kufanya ufaulu kwa masomo ya sayansi kuwa mzuri. Aidha, wingi wa walimu wenye shahada umeongeza chachu ya mafanikio katika sekta ya elimu mkoani Iringa.
=30= 


Saturday, October 24, 2015

KUELEKEA SIKU YA KUPIGA KURA MKOANI IRINGA


Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mhe. Amina Masenza



"Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuwalinda wananchi wote, hivyo, rai yangu kwa Wananchi ni kuwa jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura mapema na baada ya kupiga kura rudini kwenye maeneo yenu kuendelea na shughuli nyingine. Wananchi wasibaki kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura'

Tuesday, October 20, 2015

MATUKIO WAKATI WA KUAPISHWA MKUU WA WILAYA MTEULE YA IRINGA RICHARD KASESELAm

Mhe. Richard Kasesela akisaini kitabu cha wageni

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa

Mkuu wa Utawala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Scolastica Mlawi (kulia)

Mhe. Richard Kasesela akiapa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Amina Masenza (kulia) akimkabidhi Katiba ya Jamhurir ya Muungano wa Tanzania Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu (kushoto)

DC IRINGA SIMAMIA ULINZI NA USALAMA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela ametakiwa kusimamia ulinzi na usalama katika wilaya ya Iringa ili mkoa uwe salama katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza muda mfupi baada ya kumuapisha mkuu wa wilaya mteule wa Iringa katika ofisi ya mkuu wa mkoa leo.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa Amina Masenza
Masenza alisema “suala la ulinzi na usalama ni muhimu sana katika wilaya ya Iringa ili mkoa uwe salama. Hivyo, lazima ulisimamie ipasavyo. Binafsi nina imani na wewe na utendaji wako wa kazi hivyo hautashindwa katika kutekeleza majukumu yako”. Alisema kuwa wilaya ya Iringa ikiwa salama wananchi wataendelea kushiriki katika mampeni za kisiasa kwa uhuru na amani na hatimae kupiga kura salama.

Mkuu wa mkoa alimtaarifu masuala ya kipaumbele kwa mkoa wa Iringa kuwa ni lishe, ukimwi na usafi wa mazingira. Alimtaarifu kuwa katika ratiba yake ya kazi lazima ijikite katika utekelezaji wa mpango mkakati wa mkoa unaolenga kukabiliana na changamoto za lishe, hali ya maambukizi ya ukimwi na usafi wa mazingira.

Katika salamu za mkuu wa wilaya ya Iringa mteule Richard Kasesela alimshukuru Rais wa Jamhuri kwa imani aliyonayo kwake. Aidha, alisema kuwa katika kipindi hiki suala la amani ni agenda yake ya mwanzo kuelekea uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015. Alisema kuwa yeyote katika wilaya ya Iringa atakayetishia watu kwenda kupiga kura hasa wanawake atashughulikiwa. Alisema kuwa lazima wananchi wote katika wilaya ya Iringa washiriki katika zoezi la kupiga kura kikamilifu pasipo woga ili wafurahie haki yao ya kupiga kura kikatiba.

Akiongelea masuala ya kimkakati katika mkoa, mkuu wa wilaya mteule alisema “nitajitahidi kuhakikisha suala la lishe bora kwa wananchi hasa wanawake wajawazito na watoto wachanga linaboreka katika wilaya ya Iringa na mkoa kwa ujumla. Tatizo hili lazima liishe”.
 
Mkuu wa wilaya ya Iringa, Mhe. Richard Kasesela
Aidha, suala la ukimwi aliahidi kukabiliana nalo ipasavyo. Alisema kuwa ngono zembe ni jambo linalohitaji kuangaliwa kwa umakini zaidi. Wilaya itaangalia upya viashiria vya ukimwi na mitego ili kuangalia jinsi ya kuitegua mitego hiyo hatimae kupunguza maambukizi mapya. Akiongelea usafi wa mazingira alisema “mtu ni afya hivyo usafi wa mazingira ni afya pia. Lazima usafi wa mazingira uanzie kwa mtu mwenyewe katika mazingira ya nyumbani kwake na mazingira yanayomzunguka”.

Mkuu wa wilaya ya Iringa aliapishwa leo mjini Iringa kufuatia uteuzi wa Rais wa wakuu wapya wa wilaya 13 na kuhamishwa kwa wakuu saba wa wilaya tarehe 4/10/2015.
=30=

NEC YAVITAKA VYAMA KUELIMISHA WANANCHI TARATIBU ZA UCHAGUZI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevitaka vyama vya siasa nchini kuwaelimisha wananchi kufuata taratibu ili kufanikisha uchaguzi huru na salama nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume hiyo Jaji Mary Longway alipokuwa akifungua mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa mkoani Iringa.
 
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Mstaafu) Mary Longway akifungua mkutano
Jaji Longway alisema “vyama vya siasa vina nafasi kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, Tume inaamini kwamba ili mpiga kura aweze kufanya maamuzi sahihi ni muhimu kwake kupata elimu sahihi. Hivyo basi, Tume inatarajia kuona mkitumia majukwaa yenu vema katika kuhamasisha na kuelimisha si tu wananchi wenu bali jamii ya watanzania”. 

Alisema kuwa kuelekea uchaguzi mkuu, Tume imeandaa vituo vya kupigia kura 64,736. Tanzania bara vituo 63,156 na Zanzibar vituo 1,580. Aliongeza kuwa kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wapiga kura 450 na wasizidi 500. “Hata hivyo kituo kinapokuwa na wapiga kura zaidi ya 500 kinabidi kigawanywe ili viwe viwili yaani kituo “A” na “B” na namba ya wapiga kura itakuwa nusu kwa nusu. Mnaombwa kuwahamasisha wapiga kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikishia kupiga kura siku nane kabla ya siku ya kupiga kura ili kuweza kujua vituo vyao halisi vya kupigia kura” alisisitiza Jaji Longway.

Kamishna Longway alisema kuwa Tume imekuwa ikisikitishwa na baadhi ya vyama vya siasa kutumia majukwaa vibaya wakati wa kampeni. “Tume kwa namna ya pekee inawaomba katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kutumia nafasi zenu majukwaani kuelezea sera za vyama vyenu ili kuweza kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi baada ya kuwa na taarifa sahihi”. 

Tume imekuwa ikisikia katika vyombo vya habari malalamiko juu ya uvunjifu wa maadili ya uchaguzi katika kipindi hiki cha kampeni, “nitumie nafasi hii kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa kupeleka malalamiko yenu katika kamati za maadili na si kukimbilia katika vyombo vya habarir kama ambavyo baadhi ya vyama vya siasa na wagombea mmekuwa mkifanya”.
Viongozi wa Vyama vya Siasa Mkoa wa Iringa

Ndani ya ukumbi wa Siasa ni Kilimo

Aidha, aliwataka kuepuka kutoa taarifa na shutuma zisizo sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kujikita katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa wafuasi na wananchi kwa ujumla na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba, 2015.
=30=