Monday, December 20, 2010

MADIWANI WAWEZESHWA KIMAFUNZO

Serikali imeamua kuwawezesha Waheshimiwa Madiwani na watendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa mamlaka za serikali za mitaa kwa kubadili mtindo wa utendaji kazi kwa mamlaka za serikali za mitaa imeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa mafunzo ya awali kwa Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Gertrude K. Mpaka.

Mpaka amesema Serikali imedhamilia kubadili mtindo wa utendaji kazi wa mamlaka za Serikali za Mitaa, chini ya Waheshimiwa Madiwani ili madhumuni ya kuanzishwa mamlaka za Serikali za Mitaa na sera ya ugatuaji madaraka kwenda katika mamlaka za Serikali za Mitaa iweze kutimizwa kwa vitendo kwa kuwawezesha Waheshimiwa Madiwani na watendaji kutoa huduma ipasavyo kwa wakazi wa mamlaka za serikali za mitaa.

Amefahamisha kuwa mada zitakazofundishwa katika mafunzo hayo zitajikita katika sheria ambayo ndiyo msingi wa kuongoza utekelezaji wa shughuli za Halmashauri. Ameyataja maeneo mengine kuwa ni kanuni za maadili ya Waheshimiwa Madiwani na kanuni za kudumu za Halmashauri. Ameongeza maeneo mengine kuwa ni mahusiano ya utendaji kati ya Serikali kuu na Serikali za Mitaa na sheria zinazoongoza mahusiano hayo, sheria ya fedha za Serikali za Mitaa na kazi na wajibu wa diwani kwa Halmashauri yake na kwa wananchi anaowawakilisha.

Gertrude Mpaka ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa akisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa wahusika amesema kuwa mafunzo hayo yanawahusu Waheshimiwa Madiwani wote hata kama walikuwepo katika baraza la kipindi kilichopita na kusisitiza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wote kupata uelewa wa wajibu kama wawakilishi wa wananchi ndani ya ya chombo cha wananchi.

Nae mtoa mada Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa katika Sekretarieti ya mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika mahojiano maalumu amesema kuwa baada ya mafunzo hayo mabadiliko ya kifikra yataonekana dhahiri katika utendaji wa Waheshimiwa Madiwani na kuongeza mahusino baina yao na watendaji katika Halmashari yao na wananchi wanaowawakilisha.

Mafunzo hayo maalumu ya Waheshimiwa Madiwani yameandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuendeshwa na kuratibiwa na Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa.


No comments:

Post a Comment