Saturday, January 1, 2011

WANANCHI WATAKIWA KUTAFAKARI CHANGAMOTO ZA KIJAMII

Serikali mkoani Iringa imetoa wito kwa waumini na wananchi kutafakari changamoto zilizojitokeza katika jamii na kusababisha uvunjaji wa amani na mshikamano katika kuukaribisha mwaka mpya 2011.

Kauli hiyo imetolewa na kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kanali Issa Machibya katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista Kalalu katika mkesha mkubwa wa kitaifa uliofanyika katika uwanja wa Samora uliopo katika Manispaa ya Iringa.



       Askofu Dkt. Oderdenburg Mdegela akiteta jambo la Mwakilishi wa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista Kalalu. 
Bibi Kalalu amesema “natoa wito kwa waumini na wananchi wote kwamba tunapoukaribisha mwaka mpya, kila mmoja wetu atafakari ni mambo gain au changamoto zipi zilizojitokeza katika jamii na kusababisha uvunjifu wa amani na mshikamano wetu”. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na rushwa, mauaji ya walemavu wa ngozi (Albino), ubakaji, utoaji mamba, mauaji ya vikongwe na mauaji ya watu yanayoendelea kujitokeza.

Aidha, amesema kuwa changamoto hizo zimesababishwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii na kusisitiza kuwa waumini wa dini zote na madhehebu yote kuweka nguvu katika kuliombea taifa liepukane na mmomonyoko wa maadili. Amewataka kila mmoja kuwa mwalimu wa kutenda matendo mema yenye kumpendeza Mungu na kuendelea kudumisha amani iliyopo.

Vilevile amewataka waumini wote kuwaombea viongozi wa taifa kwa Mungu ili hekima, busara na ujasiri wa kutawala kwa moyo wa uadilifu. Ameongeza kuwa kila mwanajamii kwa nafasi yake awajibike katika kuleta maendeleo yake binafsi, kudumisha amani, mshikamano na maadili mema katika jami nzima.

Katika neno la utangulizi lililotolewa na Mhashamu Baba Askofu Dr.Oderdenburg Mdegela amesema dhumuni la mkesha huo ni kuiombea nchi ili iwe na amani, “tumekuja kuomba na kutembea pamoja ili nchi iwe na amani”. Amesema kuwa toba ni msingi wa kumkaribia Mungu na Mungu huleta mabadiliko katika familia, kazi, biashara na Taifa. Amesema kuwa mkesha huo ni mafuriko na utamfunika kila mtu katika kutenda mema. Aidha, aliwashukuru wale wote waliohusika kuruhusu uhuru wa kuabudu nchini pasipo kuvunja sheria.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Iringa wakipokea
baraka kavika uwanja wa Samora mkesha wa mwaka 2011



No comments:

Post a Comment