Friday, August 19, 2011

SUMBAWANGA YAPUNGUZA VIFO VYA AKINA MAMA

Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imefanikiwa kupunguza idadi ya vifo vya akina mama hadi kufikia vifo 245 kati ya vizazi 100,000 mwaka 2010.

Hayo yamesemwa na Afisa Muuguzi wa Manispaa hiyo, A. Ngojo wakati akifafanua lengo namba mbili la Manispaa ya Sumbawanga la kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na ujauzito katika maonesho ya nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole- Mbeya.

Ngojo amesema kuwa hadi kufikia Disemba 2010 Manispaa ya Sumbawanga iliweza kufikia lengo kwa kupunguza vifo hiyo toka vifo 263 kati ya vizazi 100,000 mwaka 2008 hadi kufikia vifo 245 kati ya vizazi 100,000 Disemba, 2010.

Amezitaja hatua zilizofikiwa kuwa ni kutoa motisha kwa wakunga wa jadi wanaowapeleka wajawazito kujifungua kwenye vituo vya afya na kupata huduma za kitaalamu. Hatua nyingine ameitaja kuwa ni kuongeza watumishi wenye ujuzi kwenye vituo vya huduma za afya toka 61% kwa mwaka 2008 hadi 91% kwa mwaka 2010.

Vilevile, kuongeza huduma za mkoba za uzazi wa mpango kutoka vituo 7 kati ya 15 (47%) kwa mwaka 2008 hadi kufikia vituo 11 (73%). Pia kuihamasisha jamii kuhusu uzazi wa mpango na kuimarisha huduma za vifaa ikiwa ni pamoja na magari ya kubeba wagonjwa.

Aidha, Manispaa hiyo imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wa umri chini ya mwaka mmoja kutoka 37 kati ya watoto 1000 mwaka 2008 hadi 17 kati ya watoto 1000 kufikia Disemba 2010.


No comments:

Post a Comment