Wednesday, November 2, 2011

KAMATI YA VOCHA NAYO YANYOOSHEWA KIDOLE

Kamati ya vocha ya ruzuku ya pembejeo za kilimo ngazi ya Mkoa wa Iringa imetakiwa kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa katika kusimamia menejimenti ya vocha za pembejeo za kilimo ikiwa ni pamoja na mfumo wa uchaguzi wa mawakala unaozingatia vigezo na uwezo.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo ngazi ya mkoa ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma “kamati na kila mmoja ni lazima awe mwangalifu katika kusimamia menejimenti ya ugawaji na usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo ili kuhakikisha zoezi zima linafanikiwa”. Ameongeza kuwa lazima utumike mfumo mzuri na madhubuti wa kuwapata mawakala utakaozingatia vigezo na uwezo wao ili kuondoa ubabaishaji ambao umekuwa ukijitokeza na kusababisha wakulima kutokunufaika na ruzuku hiyo ya serikali wakati mawakala wakiendelea kutajirika kupitia migogo ya wakulima. Amesisitiza kuwa ni vizuri kuwa na mawakala wachache wenye vigezo kuliko kuwa na mawakala wengi wasio na vigezo.     

Akiwakilisha taarifa ya upatikanaji na usambazaji wa vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mwaka 2010/2011, Afisa Kilimo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni amesema kuwa Mkoa umepokea vocha zenye thamani ya shilingi Bilioni 21.6. Amesema vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo zilizopokelewa na Mkoa ni za kutosha Kaya 336,635 ambazo ni sawa na vocha 1,009,905 kwa ujumla wa nakala moja moja ya vocha.

Akiongelea idadi ya mawakala kwa Mkoa wa Iringa katika kipindi husika, Nyoni amesema kuwa Mkoa ulikuwa na mawakala 514 waliofanya kazi ya kusambaza pembejeo za kilimo. Amesema miongoni mwa mawakala hao mawakala 390 ndio waliofanya kazi ya kusambaza pembejeo katika ngazi ya vijiji na kata kwa utaratibu wa mfumo wa ruzuku ya pembejeo.

Nyoni amesema changamoto kubwa ni malalamiko kutoka kwa wakulima juu ya kuongezeka kwa bei ya mbolea ilikinganishwa na msimu uliopita. Amesema msimu uliopita bei mkulima alichangia shilingi 48,000 hadi 65,000 ikilinganishwa na msimu 2010/2011 aliochangia shilingi 85,000 hadi 90,000 kwa pembejeo za ekari moja yaani mbegu bora, mbolea ya kupandia na kukuzia. 

No comments:

Post a Comment