Wednesday, November 21, 2012

JAPAN KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA AFYA



Serikali ya Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali hasa sekta ya afya na kilimo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akimkabidhi kitabu cha profile ya Mkoa wa Iringa Balozi wa Japan nchini Tanzania

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika ziara iliyolenga kusaini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Balozi Okada amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha uchumi unakuwa kwa kasi zaidi kwa kukuza biashara baina ya nchi mbili hizo. Amesema kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo, ni lazima kipato chao kiongezeke ili waweze kunufaika na kilimo hicho kama shughuli yao kuu ya kiuchumi. Amesema kuwa Serikali yake inao mpango wa kuisaidia sekta ya kilimo nchili ili kuhakikisha kilimo cha mpunga kinaongezeka mara dufu kwa kuwa nchi ya Japan inasifika kwa uzalishaji wa mpunga duniani.

Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuahidi kuziunga mkono juhudi hizo kwa karibu.

Awali katika salamu za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesifu juhudi za Serikali ya Japan katika kusaidia maendeleo kwa mkoa wa Iringa na kusema ni juhudi za kupongezwa sana. Amesema kupitia misaada ya Japan, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweza kupata ufadhili katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, kilimo, maji na umwagiliaji.

Akiongelea maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kwa kujibu wa utafiti wa mwaka 2008, mkoa wa Iringa ulikuwa na takribani asilimia 16 ya maambukizi, kiwango ambacho ni karibu mara tatu ya kiwango cha maambukizi kitaifa. Amesema kuwa hali hiyo haikubaliki na zinaihitajika juhudi za pamoja kati ya Tanzania na Japan katika kuendeleza mapambano hayo. Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Japan za kuisaidia Tanzania katika sekta ya afya na ustawi wa jamii kupitia miradi mbalimbali kwa lengo la kuboresha afya ya mama na familia katika  mkoa wa Iringa.

Balozi wa Japan nchini Tanzania yupo mkoani Iringa kwa ajili ya utiaji saini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga unaogharimu dola za kimarekani 123,339 kwa lengo la kuongeza ubora wa huduma za afya na kupunguza vifo vya wanawake na watoto mkoani Iringa.
=30=


No comments:

Post a Comment