Monday, November 26, 2012

UKATILI WA KIJINSIA...WANAUME WAWAJIBIKE



Unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa nchini kutokana na baadhi ya dhana na mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka na kuwanyima wanawake haki zao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake wakati wa uzinguzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga unyanyasaji wa kijinsia maadhimisho yaliyofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa Manispaa ya Iringa.

Dkt. Christine amesema “unyanyasaji wa kijinsia unaweza kutokea kwa jinsi yeyote ile, mwanamke, mwanaume au watoto. Ila huwapata sana kina mama na vijana hasa watoto wa kike. Unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa ulimwenguni kote, nchini Tanzania, kadhalika katika mikoa yetu ya Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi”. Amesema kuwa baadhi ya dhana kama umasikini, mila na desturi hasa zinazowapa wanaume mamlaka na kuwanyima wanawake haki zao ni moja klati ya viini vinavyopelekea unyanyasaji wa kijinsia nchini. Amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Tanzania Demographic Health Survey mwaka 2010, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inakuwango cha wastani wa vitendo unyanyasaji wa kijinsia. Amesema “Iringa 54%, Ruvuma 55%, Mbeya 55%, Mtwara 26%, Lindi 22% na Rukwa 56%” amesema kuwa kwa mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa wastani wa kiwango ni mkubwa ukilinganisha na na kiwango cha wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 44.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa katika kupambana na hali hiyo, Serikali kupitia Mpango wa kupambana na Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA), mabadiliko ya Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana, imefanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo la ukatili wa kijinsia. Aidha, amesema kuwa Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau utaendelea kuwajengea uwezo watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali ili waweze kutatua na kuzifanyia kazi kesi zinazohusi ukatili wa kijinsia.

Miongoni mwa jitihada hizo, Mkuu wa Mkoa amezitaja kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi na kusisitiza kuwa wananchi wahamasishwe kwenda kutoa taarifa, kuhakikishiwa usalama wao na kuamini kuwa madawati yale yako kwa ajili yao. Amesema katika kuliwekea mkazo tatizo hilo, Mkoa umeziagiza Halmashauri kuendelea kutenga bajeti katika mipango yao kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, haki za binadamu, sheria na madhara yatokanayo na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Dkt. Christine amesema “yatupasa tukumbuke kuwa ukatili wa kijinsia sio suala la wanawake ama watoto pekee. Ni muhimu sana kwa wakati huu; hasa kwa kina baba kuwa chachu ya mabadiliko kwa kupinga vitendo vya ukatili na hata kukemea tabia hizo”. Amesema ni vema viongozi na jamii ikatumia ushawishi wake kuamsha majadiliano juu ya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia, kuvipinga kwa nguvu zote na kuwa mfano bora wa kuigwa ili kuimarisha ustawi wa nchi ya Tanzania.
=30=

No comments:

Post a Comment