Thursday, April 11, 2013

EX-RAS AWATAKA WAFANYAKAZI KUJITUMA ZAIDI IRINGA



Wafanyakazi mkoani Iringa wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma na kusimamia vizuri rasilimali zilizopo ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengi na hatimae kujiletea maendeleo yanayopimika.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma katika nasaha zake alizozitoa katika tafrija ya kumuaga Katibu Tawala Mkoa aliyestaafu Gertrude Mpaka baada ya kuutumikia Umma kwa zaidi ya miaka 36 na kuukaribisha mwaka 2013 iliyofanyika katika ukumbi wa St. Dominic Manispaa ya Iringa.

Dkt. Christine amesema “kwa kuwa tunaukaribisha mwaka 2013, natoa rai kwa watumishi wenzangu kuwa kila mmoja kwa nafasi yake awe msimamizi mzuri wa rasilimali mbalimbali tulizonazo”. Amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kutenda haki katika maeneo yao ya kazi na kuipiga vikali rushwa kwa sababu ni adui wa haki.

Amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kujituma na kujiwekea malengo yanayopimika ili kuhakikisha utendaji kazi unakuwa wa kiwango cha juu hasa katika kutoa huduma kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa amesisitiza suala la kudumisha amani ili taifa liendelee kuwa na utulivu. Amesema mahali penye amani maendeleo hujidhihirisha kwa sababu wananchi wanakuwa huru kufanya kazi za maendeleo.

Katika risala ya watumishi kwa Katibu Tawala Mkoa mstaafu, iliyosomwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Wamoja Ayubu amesema amempongeza kwa utumishi wake uliotukuka na kusema kuwa ataendelea kuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa watumishi wote katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na mkoa wa Iringa kwa ujumla. 

Amesema “tumefanya kazi pamoja kwa muda mrefu sana, kwa upendo na ushirikiano mkubwa na kwa kufuata taratibu na kanuni zilizopo kwa weledi katika utumishi wa Umma”. Amesema kuwa ushirikiano wake uliusaidia mkoa wa Iringa kufanya kazi kwa ufanisi na kupiga hatua kimaendeleo na kuwa mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine.

Tofauti na utendaji kazi wa Gertrude, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amezitaja sifa za kipekee alizokuwa nazo Katibu Tawala mstaafu kuwa ni mahusiano na ushirikiano mzuri kwa watumishi wote pasipo kujali nafasi zao. Wamoja amesema “hukuwa na ubaguzi kwa watumishi na ulihakikisha kuwa watumishi wanakuwa na mazingira mazuri ya kufanya kazi na kusimamia ujenzi wa Ofisi za Tarafa katika Mkoa wa Iringa na Njombe. Ameitaja sifa nyingine kuwa ni wepesi wake katika kushirikiana na watumishi wote wakati wa shida na raha.

Katika hotuba ya Katibu Tawala Mkoa mstaafu, Gertrude Mpaka, alipongeza mafanikio yaliyopatikana katika kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Njombe na kuyaita kuwa ni mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa watu mbalimbali. Ameongelea mafanikio katika sekta za kilimo, mifugo, elimu, afya, mazingira na maji.

Aidha, Gertrude alitumia muda huo kuwaomba radhi wale wote aliowakosea kwa namna moja au nyingine wakati akitekeleza majukumu yake. Amesema“nilikuwa nafanya kazi za kuwahudumia wananchi nikiwa na wenzangu inawezekana kabisa kwamba wapo watu ambao niliwakwaza au kuwaudhi kwa kauli au matendo yangu wakati wa utekelezaji wa kazi zangu, kama wapo watu wa aina hiyo naomba kutumia nafasi hii kuwaomba radhi. Sikudhamiria kumuudhi au kumkwaza mtu, kama ilitokea basi ni kwa bahati mbaya naomba mnisamehe. Vivyo hivyo kwa upande wangu sina yeyote ambaye nina kinyongo nae” alisisitiza Gertrude.
=30=

No comments:

Post a Comment