Friday, September 13, 2013

BRN KUTEKELEZWA KWA VITENDO IRINGA



Na. Bruno Machary, IRINGA
Serikali Mkoani Iringa imejipanga kutekeleza kwa vitendo utaratibu wa matokeo makubwa sasa (BRN) ili kufikia malengo yaliyowekwa kitaifa ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma

Hayo yamejidhihirisha jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Dkt. Christine Ishengoma kufanya ziara katika Halimashauri za Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuhamasisha utendaji wa kazi kwa wafanyakazi wa kada mbalimbali kupitia utaratibu wa matokeo makubwa sasa. Katika ziara hizo pamoja na mambo mengine amekuwa akisikiliza changamoto na kero na kuzipatia ufumbuzi.

Akiongea na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Ishengoma amesema kuwa wataalamu hawapaswi kukaa ofisini tu ila wanapaswa kutoka na kuwasikiliza wananchi ili kutatua kero zinazowakabiri kwa urahisi. 

Amesema kuwa wataalamu hao ndio suluhisho la kero hizo zinazowakabili wananchi katika kufikia maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii. Amesema kuwa kila mfanyakazi analo jukumu la kujitazama na kujihoji yeye wenyewe jitihada alizofanya katika kufikia malengo ya Serikali.

“Utendaji kazi ubadilike na kila mmoja aipende kazi yake kulingana na kada aliyonayo” amesema Dkt. Ishengoma.

Akiongelea dhana ya mawasiliano katika kuleta ufanisi wa kazi, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mawasiliano ni jambo la muhimu sana kwa wafanyakazi kwasababu yanasaidia kuleta ushirikiano na upendo miongoni mwa wafanyakazi hatimae kuondoa chuki baina yao. Amesema kuwa mawasiliano yanapokuwa mazuri ufanisi wa kazi unakuwa mzuri pia.

Amewashauri wafanyakazi kuwashirikisha wakuu wa idara zao pale wanapokabiliwa na matatizo mbalimbali katika utendaji kazi wao. Amesema kuwa ni vizuri kutatua matatizo yanayojitokeza kupitia vikao rasmi vya idara kabla ya kuyawasilisha ngazi za juu.

Matokeo makubwa sasa (B.R.N) ni utaratibu wa utendaji kazi ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kutoa ufanisi wa kazi unaopimika haraka. Maeneo ya kipaumbele katika BRN ni elimu, nishati, maji, uchukuzi, mapato na kilimo.
=30=



No comments:

Post a Comment