Wednesday, October 9, 2013

RC ASISITIZA AMANI NA UMOJA WA KITAIFA



Wananchi wametakiwa kudumisha amani na umoja wa kitaifa kwa kuenzi juhudi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alizoziweka wakati wa kuweka misingi ya Taifa kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na wiki ya vijana kitaifa mkoani Iringa. 

Dk. Christine amesema kuwa wananchi wanawajibu wa kuhakikisha amani na umoja wa kitaifa vinadumu na kuwa endelevu nchini. Amesema kudumisha amani na utulivu ni njia mojawapo ya kuenzi misingi na kazi alizofanya baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa Taifa la Tanzania. Amesema “sehemu yoyote yenye amani na utulivu, yapo maendeleo kwa sababu wananchi wanafanya shughuli za maendeleo kwa uhuru, hii ndiyo maana yam bio za Mwenge wa Uhuru” alisisitiza Dk. Christine.

Akiongelea ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2013, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2013, zimebeba ujumbe usemao: “watanzania ni wamoja” wenye kaulimbiu “tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini, itikadi, rangi na rasilimali”. 

Amesema lengo la ujumbe huo ni kutoa msisitizo kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuimarisha umoja na amani nchini. Amesema kuwa ni ushahidi kwa nchi jirani unaonesha madhara ya kuichezea amani na kuongeza kuwa ni rahisi sana kupoteza amani na umoja lakini ni vigumu sana kuirejesha. Amesema kutokana na umuhimu huo, Serikali imeona ni vizuri kutumia mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2013 kuhimiza umoja wa kitaifa. 

Akiongelea wiki ya vijana kitaifa iliyoanza tarehe 08/10/2013, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa maonesho hayo yameandaliwa vizuri ili yaweze kuwa na mvuto muda wote. Amesema kuwa vijana kutoka nchi nzima wanashiriki katika maonesho hayo na kutoa rai kwa vijana wote kutumia maonesho hayo kujifunza shughuli wanazofanya za kujiletea kipato. 
   
Ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kutembelea mabanda ya maonesho katika uwanja wa shule ya msingi Mlandege kuanzia ufunguzi hadi kilele tarehe 14/10/2013.

Amesema kuwa sambamba na maonesho hayo kutakuwa na midahalo ya vijana itakayofanyika kuanzia tarehe 9/10/2013-13/10/2013 katika ukumbi wa chuo cha VETA itakayohusisha vijana zaidi ya 300 kila siku. Amesema kuwa midahalo hiyo itarushwa na vyombo vya habari na kuwataka vijana kushiriki kikamilifu katika midahalo hiyo.
  =30= 

No comments:

Post a Comment