Monday, June 23, 2014

IRINGA WATAKIWA KUKIMBIZA MWENGE KWA UTULIVU



Na. Dajari Mgidange, IRINGA

Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru katika maeneo mbalimbali utakayokimbizwa mkoani Iringa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mkoani Iringa mwaka 2014 ofisini kwake leo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma

Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa
Dkt. Ishengoma amesema kuwa ni vizuri wananchi wakajitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru pindi utakapopita katika maeneo yao. Amesema “ninawasihi wananchi kuendela kudumisha amani na utulivu wakati wote ambapo Mwenge wa Uhuru utakuwa ukikimbizwa katika mkoa wetu na hata baada ya kuhitimisha mbio hizo katika mkoa wetu”.
Akiongelea uhamasishaji katika halmashauri, Mkuu wa Mkoa amesema “ninapenda kutumia fursa hii kuviomba vyombo vya habari na ninyi waandishi wa habari kuwahamasishwa wananchi katika halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge wa Uhuru katika maeneo yote ambako utapita, kushiriki katika mikesha ya Mwenge pamoja na kupokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu 2014”.
Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Mkoa wa Iringa utakagua, kuweka mawe ya msingi, kufungua na kuzindua jumla ya miradi ya maendeleo 42 yenye thamani ya Tsh. 3,109,958,020/=. Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru utatoa ujumbe katika maeneo yote ambako utakimbizwa. Ameitaja miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru kuwa ni miradi ya barabara, elimu, afya, kilimo na ufugaji. Miradi mengine ameitaja kuwa ni miradi ya vijana na wanawake na hifadhi ya mazingira.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2014 unaongozwa na ujumbe usemao “katiba ni sheria kuu ya nchi’’ wenye kauli mbiu isemayo ’ jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya’.
=30=

No comments:

Post a Comment