Wednesday, May 6, 2015

SHULE ZA IGOWOLE NA KAWAWA ZAPONGEZWA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Shule za sekondari za Igowole na Kawawa zimepongezwa kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita mwaka 2014 na kuung’arisha mkoa wa Iringa kitaifa.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya mitihani wa Mkoa wa Iringa, bibi. Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mitihani inayoendelea ya kidato cha sita nchini ofisini kwake.

Wamoja amesema “nichukue nafasi hii kipekee kuzipongeza shule za sekondari za Igowole na Kawawa zote zipo katika halmashauri ya wilaya ya Mufindi kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita mwaka 2014, ambapo Igowole iliahika nafasi ya kwanza kitaifa na Kawawa ilishika nafasi ya kumi. Hongereni sana kwa matokeo hayo yaliyoufanya mkoa wetu kung’ara.” “Aidha, nichukue nafasi hii pia kuzipongeza shule zote za mkoa wa Iringa kwa kuwa kwa ujumla wake zilifanya vizuri katika matokeo hayo kati ya shule 22 zilizokuwa na watahiniwa wa kidato cha sita mwaka 2014 shule 18 zilifaulisha kwa asilimia 100 kwa maana hakukuwa na mwanafunzi aliyepata daraja la 0”, aliongeza bibi. Wamoja.

Akiongelea mitihani inayoendelea ya kidato cha sita, Mwenyekiti wa Kamati ya Mitihani wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mkoa unavyo vituo 23 vya mtihani wa kidato cha sita vyenye jumla watahiniwa 2,162. Amesema kuwa vituo hivyo vitasimamiwa na wasimamizi 73 kati yao wasimamizi wakuu 23 na wasimamizi wasaidizi kutoka nje wapatao 50. 

Kwa mitihani ya ualimu, amesema vipo vituo 4 vyenye jumla ya watahiniwa 324 kati yao 122 ni ngazi ya Cheti na 202 ngazi ya Diploma. Ameongeza kuwa vituo hivyo vitasimamiwa na wasimamizi wakuu wanne na wasimamizi wasaidizi saba kutoka nje.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amewataka wasimamizi kutokuwa na tamaa ya fedha itakayowasababishia kujiingiza katika vitendo vya uvujishaji mitihani. Aidha, amewataka kuzingatia ratiba zilizotolewa ili kila mtihani ufanyike kwa wakati uliopangwa na kuwepo katika chumba cha mtihani kipindi chote ili kutotoa mwanya kwa watahiniwa kutazamiana.

Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, bibi. Amina Masenza amewatakia heri watahiniwa wote wa mitihani ya kidato cha sita mkoani Iringa na kuwataka kutokuwa na hofu na kufanya mitihani hiyo kwa kujiamini kwa kuzingatia yale yote waliyojifunza.

Mitihani wa kumaliza kidato cha sita na ualimu imeanza tarehe 04 Mei na itaendelea hadi tarehe 27 nchini kote.
=30=

No comments:

Post a Comment