Thursday, January 26, 2017

IRINGA KUSIMAMIA UPIMAJI VIWANJA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umeendelea kusimamia upimaji wa viwanja na uandaaji wa michoro ya mipango miji ili kuwa na miji iliyopangwa vizuri. 

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa ya sekta ya ardhi mkoa wa Iringa kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dr. Angelina Mabula ofisini kwake hivi karibuni.

Masenza alisema “usimamizi wa miji na uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi umeendelea kufanyika na kusimamiwa katika Halmashauri zote za Mkoa. Ili kuhakikisha kunakuwepo na miji iliyopangwa, mkoa umeendelea kusimamia uandaaji wa michoro ya mipango miji na upimaji wa viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali katika Halmashaauri zote za Mkoa

Alisema kuwa jumla ya viwanja 37,463 vimepimwa mkoani Iringa. Aliongeza kuwa katika Halmashauri ya Manispaa viwanja 21,230, Halmashauri ya mji wa Mafinga viwanja 11,950, Halmashauri ya wilaya ya Iringa viwanja 1,500, Halmashauri ya wilaya ya Kilolo viwanja 2,020 na Halmashauri ya wilaya ya Mufindi viwanja 763.

Alisema kuwa mkoa umeendelea kusimamia na kuhakikisha makazi holela na ujenzi wa milimani unapungua na kuisha kabisa kwa kuchukua hatua madhubuti. Hatua hizo ni kusimamia ukamilishaji wa mpango kabambe wa mji wa Iringa (Iringa Master Plan) ili kuhakikisha maeneo yote yanakuwa na matumizi na kurahisisha usimamizi wake. Hatua nyingine ni kuendelea kusimamia zoezi la kurasimisha makazi ya wananchi. .  
=30=

No comments:

Post a Comment