Tuesday, September 19, 2017

MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WAPYA IRINGA KULETA MABADILIKO CHANYA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya katika ofisi ya mkuu wa mkoa Iringa yataleta mabadiliko chanya katika utumishi wa umma mkoani Iringa.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Takwimu katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Iringa, Hildegarda Kimaro katika mahojiano maalum yaliyofanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa jana.
Afisa Takwimu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Hildegarda Kimaro

Kimaro alisema “mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya ni mazuri, tumejifunza mambo mbalimbali ambayo hatukuyafahamu awali. Mfano sheria ya utumishi wa umma na kanuni zake na utunzaji wa kumbukumbu”. 

Aliongeza kuwa awali utunzaji kumbukumbu lilifahamika kuwa ni jukumu la watunza kumbukumbu wasaidizi katika ofisi ya mkuu wa mkoa, lakini baada ya mafunzo imebainika kuwa utunzaji kumbukumbu ni jukumu wa watumishi wote wa umma kwa nafasi zao.

Akiongelea umuhimu wa mafunzo hayo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma, Kimaro alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kutokuvunja sheria za utumishi. “Mafunzo haya ni muhimu na yatatusaidia kutokuvunja sheria ambazo tungevunja bila kufahamu. Kwa mafunzo haya tumeweza kufahamu jambo ambalo ni sahihi kufanya katika utumishi wa umma na ambayo si sahihi kufanya katika utumishi wa umma” alisema Kimaro.     

Kimaro alishauri kuwa watumishi wapya wanapoajiriwa wapewe mafunzo elekezi ya awali angalau ndani ya miezi mitatu ya awali. 

Katika kuongeza umakini wa mafunzo, ni vizuri mafunzo hayo yakatolewa nje ya eneo la kazi ili kuwawezesha washiriki wa mafunzo kujikita katika mafunzo kuliko kutekeleza majukumu mengine ya kiutumishi jambo linaloathiri utulivu na usikivu wakati wa mafunzo” alishauri Kimaro.

Mafunzo elekezi ya awali ya siku tano kwa watumishi wapya wa umma yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na chuo cha utumishi wa umma (TPSC) yakishirikisha watumishi wapya 107 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi za wakuu wa wilaya na hospitali ya rufaa ya mkoa.
=30=





No comments:

Post a Comment