Wednesday, October 4, 2017

ELIMU YA UJASIRIAMALI KWA WAJASIRIAMALI YATOLEWA



Na Dennis Gondwe, IRINGA
Maadhimisho ya siku ya utalii ya utalii duniani, maonesho ya karibu kusini na maonesho ya wajasiriamali wa viwanda vidogo mikoa ya nyanda za juu kusini yamefanikiwa kutoa elimu ya ujasiriamali na utalii.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika salamu zake wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za wajasiriamali wa wa viwanda vidogo wa mikoa ya nyanda za juu kusini yaliyofanyika mkoani Iringa jana.
Mhe Amina Masenza

Masenza alisema kuwa maonesho hayo yamekuwa ya manufaa kwa jamii. “Maonesho haya yametoa elimu ya masuala ya utalii na ujasiriamali, ajira kwa watoa huduma mbalimbali wakati wa maonesho na washiriki wameweza kubadilishana uzoefu na kupata masoko ya bidhaa” alisema Masenza. 

Mafanikio mengine, mkuu wa mkoa wa Iringa aliyataja kuwa ni kuongezeka kwa wadau wanaotaka kuwekeza katika mikoa ya nyanda za juu kusini.

Masenza alisemaa kuwa maonesho ya karibu kusini mwaka 2017 yalijumuisha maeneo sita ikilinganishwa na maeneo matatu ya mwaka 2016. Aliyataja maeneo hayo kuwa ni ziara za kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na baadhi ya vivutio, maonesho ya wanyama hai, maonesho ya ngoma za asili, kongamano la utalii endelevu na uendeshaji viwanda kwa mikoa ya nyanda za juu kusini na maonesho kwenye mabanda kwa kuonesha bidhaa za wajasiriamali wa viwanda vidogo na watoa huduma za utalii. 

Maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za wajasiriamali wa SIDO yamehusisha mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Songwe, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam, Geita, Lindi, Morogoro, Kilimanjaro, Tabora na nchi ya Kenya. Maonesho hayo yamehusisha mashine mbalimbali, bidhaa za usindikaji, bidhaa zilizosindikwa, bidhaa za ngozi, kazi za mikono na dawa.
=30=

No comments:

Post a Comment