Wednesday, January 17, 2018

KILIMO KINACHANGIA ASILIMIA 85 YA PATO LA MKOA IRINGA




Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Sekta ya kilimo inachangia katika usalama wa chakula na utoaji ajira na uchumi wa Mkoa wa Iringa.


Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa wajumbe kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa waliofanya ziara ya mafunzo ya siku tano mkoani Iringa katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa jana.

Masenza alisema “sekta ya kilimo katika Mkoa ni muhimili mkuu wa uchumi na inachangia katika usalama wa chakula na utoaji wa ajira. Sekta hii inachangia takribani asilimia 85 ya pato la Mkoa kwa mujibu wa wasifu wa kiuchumi na Kijamii, mwaka 2013”. Alisema kuwa lengo la Mkoa ni kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na chakula cha kutosha, wanaongeza kipato na uhakika wa upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda.


Akiongelea sekta ya mifugo na uvuvi, mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema kuwa Mkoa wa Iringa una mashamba makubwa ya mifugo 20 yanayomilikiwa na serikali na watu binafsi. Alisema kuwa mashamba hayo huzalisha maziwa, mitamba na madume bora.
Mkoa wa Iringa hadi kufikia Juni, 2017 ulikuwa na jumla ya ng’ombe 330,372, mbuzi 160,227, kondoo 62,475, nguruwe 109,131 na kuku wapatao 1,341,718 na eneo linalotumika kwa malisho ni jumla ya hekta 209,003” alisema mkuu wa Mkoa.

Kwa upande wa uvuvi, alisema kuwa Mkoa una mabwawa madogo 1,893 yaliyochimbwa yanayotumiwa kwa shughuli za uvuvi. Alisema kuwa Mkoa una wavuvi 5,807 ambao hufanya shughuli za uvuvi kama mtu mmoja mmoja na katika vikundi.

Mavuno ya samaki yamekuwa yakiongezeka kutoka Tani 913.50 mwaka 2011/2012 hadi kufikia Tani 1,186.99 mwaka 2014/15.

Akitoa neno la shukrani, kiongozi wa wajumbe kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi Capt. Msafiri Hamisi alipongeza kwa mapokezi ya Mkoa na kazi zinazofanywa na Mkoa za kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo. Aidha, aliahidi wanafunzi wa chuo cha Taifa cha ulinzi kuwa balozi wazuri kwa mkoa wa Iringa.

Kwa matokeo ya Sensa ya mwaka 2012 Mkoa wa Iringa ulikuwa na watu 941,238 kati ya hao wanaume walikuwa 452,052 na wanawake 489,186 na wastani wa ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka ni asilimia 1.1. Makadirio ya idadi ya watu kwa mwaka 2017 ni watu 1,000,040; wanaume wakiwa 480,293 na wanawake 519,747.
=30=

No comments:

Post a Comment