Monday, March 26, 2018

Viongozi Iringa kupunguza Maambukizi ya Kifua Kikuu-RC Masenza



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Viongozi mkoani Iringa wametakiwa kujipanga kuhakikisha maambukizi ya kifua kikuu yanapungua ili wananchi waweze kutekeleza shughuli za maendeleo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yaliyofanyika ngazi ya mkoa katika mji wa Ilula wilayani Kilolo hivi karibuni.
 
Masenza alisema kuwa viongozi katika ngazi zao wanajukumu la kuhakikisha maambukizi ya kifua kikuu yanapungua katika jamii inayowazunguka ili jamii hiyo iweze kufanya kazi za kuzalisha mali. “Kwa hiyo katika vikao vyote vitakavyofanyika katika maeneo yetu ya kazi, katika ngazi zote kifua kikuu iwe ni agenda ili kuweza kupanga mikakati ya uboreshaji wa huduma za kifua kikuu” alisema Masenza. 

Aidha, alizitaka Halmashauri katika mkoa wa Iringa kupanga na kufanya shughuli za uchunguzi wa dalili za kifua kikuu katika makundi hatarishi. Aliyataja makundi hayo kuwa ni shule, magareza na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Mkuu wa mkoa alisema kuwa katika kuadhimisha juma la siku ya kifua kikuu duniani, katika eneo la Ilula Sokini, huduma mbalimbali zilikuwa zikitolewa kwa wananchi bila malipo. Huduma hizo alizitaja kuwa ni uchunguzi wa dalili za kifua kikuu na matibabu, upimaji wa maambukizi ya VVU, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, uchangiaji na utoaji wa damu, huduma ya uzazi wa mpango, elimu kuhusu lishe, na elimu kuhusu kifua kikuu.

Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yamefanyika ngazi ya mkoa katika mji wa Ilula yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘viongozi tuwe mstari wa mbele kuongoza mapambano ya kutokomeza kifua kikuu’.
=30=

No comments:

Post a Comment