Sunday, August 26, 2012

VYOMBO VYA HABARI IRINGA VYATAKIWA KUENDELEA KUHAMASISHA SENSA



Vyombo vya habari Mkoani Iringa vimeshauriwa kuendelea kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili liweze kufanikiwa katika Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma muda mfupi baada ya kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lililoanza usiku wa Kuamkia leo nchini kote.
Dkt. Christine amesema kuwa zoezi hilo vimeanza vizuri na mdadisi ameonekana kubobea katika kazi hiyo. Aidha, amewamwagia sifa wakufunzi na wadadasi kwa jinsi walivyoonesha juhudi katika kufundisha na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu uelewa wa zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Sensa ya Mkoa amevipongeza vyombo vya habari vya Mkoa wa Iringa kwa weledi katika kuhamasisha zoezi hili. Amesema uhamasishaji ni muhimu sana katika kutoa hamasa kwa kazi ya Sensa ili asitokee mtu ambaye atakuwa hakupata taarifa na elimu juu ya umuhimu wa Sensa na kuhesabiwa. Aidha, ametoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea na uhamasishaji huo kwa kipindi cha wiki nzima ili kulifanikisha zoezi hili katika Mkoa wa Iringa. “kufanikiwa kwa zoezi hili Mkoani Iringa sit u kutakuwa na manufaa kwa Mkoa wetu, bali kwa nchi nzima na jambo hili litafikiwa pale tu wananchi wote watakapokuwa wameelewa umuhimu wa zoezi hili na kushiriki katika kulifanikisha” alisisitiza Dkt. Christine.

Akiongelea matukio yasiyo ya kawaida katika zoezi hili, Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi hilo limeanza katika hali ya utulivu mkubwa na hakuna tukio lolote lisilo la kawaida lililotokea na kuripotiwa. Aidha, amewata wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa pindi watakapopita katika maeneo yao na kujibu kwa usahihi maswali watakayokuwa wakiulizwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka, akitoa maoni yake baada ya kuhesabiwa asubuhi ya leo amesema kuwa kazi ya kuhesabu na kuhesabiwa ni jukumu la kila mtanzania pasipo kujali mipaka ya aina yoyote. Amesema kila mtanzania anayo haki ya kuhesabiwa katika Sensa hii ili kuhakikisha Serikali yake inapata taarifa sahihi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake.
Mpaka amesema “miongoni mwa michango ya wananchi katika jitihada za kujiletea maendelea kwa kushirikiana na Serikali yao ni pamoja na kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu”. Amesema zipo njia mbalimbali za kushiriki katika shughuli za maendeleo katika kipindi hiki kutoa taarifa sahihi ni jukumu namba moja ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi. 

Sensa ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini ikiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa’ ipo katika siku yake ya kwanza nchini kote na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa mara moja tu.
=30=

Wednesday, August 22, 2012

...AMIA HUKU DIGITALI



Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa elimu kwa umma ni nyenzo muhimu sana katika kuwaandaa wananchi kuhama kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analojia na kuingia katika mfumo wa digitali.

Ameyasema hayo katika mkutano wa viongozi wa mkoa wa Iringa kuhusiana na mabadiliko ya mfumo wa utangazaji kutoka analojia kwenda digitali uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu Huria, tawi la Iringa.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa akisoma hotuba yake

Picha ya Pamoja ya washiriki wa Warsha hiyo

Amesema katika kufanikisha jitihada hizo, “umeonekana umuhimu wa kuelimisha umma kwa kushirikisha wizara, idara za Serikali pamoja na wananchi wote ili kuweza kufanikisha mabadiliko haya kwa ufanisi bila kuathiri upatikanaji wa huduma za utangazaji nchini”. Ameishauri kamati maalumu ya kitaifa inayofanya kazi ya kuwaelimisha wananchi nchini juu ya mabadiliko ya teknolojia ya utangazaji kuhakikisha wananchi wengi wanapata elimu hiyo ili kuwaandaa na mabadiliko hayo. Amesema maana ya mabadiliko ya teknolojia, matarajio ya baada ya mabadiliko na wajibu wa mwananchi katika kufanikisha mabadiliko hayo ni mambo ya muhimu kutiliwa mkazo katika utoaji wa elimu kwa wananchi.

Akiongelea Sensa ya Watu na Makazi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ametoa wito kwa washiriki hao kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi. Amesema “natoa wito kwenu washiriki wa mkutano huu hasa waandishi wa habari kutumia nafasi hii kuhimiza jambo hili na kutumia muda wenu na vyombo vyenu kuwaelimisha wananchi ili waweze kushiriki katika zoezi hili na kulifanya liwe la manufaa na kuleta tija katika Mkoa wetu wa Iringa na Taifa kwa ujumla” alisisitiza Dkt Christine.
=30=

WAZAZI WASHAURIWA KUSHIRIKI KATIKA MALEZI YA WATOTO



Wazazi wameshauriwa kutoa ushirikiano kwa walimu katika malezi ya wanafunzi ili kuhakikisha jamii inakuwa na watu wenye nidhamu na maadili mema. 

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alikokuwa akiongea na wananchi, walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Ilambilole iliyopo katika Kata ya Nduli, Wilayani Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa suala la nidhamu kwa wanafunzi haliishii shuleni pekee bali ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha inawasaidia walimu katika malezi ya wanafunzi. Amesema “nidhamu inaanzia nyumbani hivyo lazima tusaidiane na walimu katika kudumisha nidhamu ya watoto wetu, lakini tukiwaachia walimu peke yao hatuwezi kufanikiwa. Walimu wana nafasi yao katika kukuza na kudumisha nidhamu na wazazi pia wana nafasi yao katika hili”.

Akiongelea changamoto ya upungufu wa walimu wanaofundisha masomo ya sayansi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa upungufu huo upo kwa sababu wanafunzi wengi hawataki kusoma masomo ya sayansi. “Tunaupungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwa sababu watoto wetu hawasomi masomo ya sayansi” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Katika kukabiliana na hali hiyo, alishauri wanafunzi wahamasishwe kusoma masomo ya sayansi ili kuweza kuziba pengo hilo. Aidha, alisema kuwa Serikali inaendelea na mipango ya muda mrefu ya kuhakikisha changamoto hiyo inabaki historia.   

Akiwasilisha taarifa ya shule ya Sekondari ya Ilambilole, Mkuu wa shule hiyo, Vicent Ngaya amesema kuwa shule yake inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba za walimu na walimu wa masomo ya sayansi. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni kukosekana kwa mabweni hasa kwa wanafunzi wa kike na umbali wa makazi ya walimu kutoka shuleni jambo linalosababisha kuchelewa kufika shuleni na kufika wakiwa wamechoka sana.
Kuhusu ufauli, Ngaya amesema kuwa shule imepata mafanikio makubwa katika ufaulu wa wanafunzi, ambapo kwa mwaka 2010 ufaulu ulikuwa ni asilimia 78 na mwaka 2011 ufaulu ulikuwa ni asilimia 61.

Wakati huohuo, suala la wivu limeelezwa kuwa halina nafasi katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti, mwaka huu. Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Msaidizi wa Sensa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga wakati akifafanua masuala mbalimbali ya Sensa katika Kijiji cha Ikengeza, Wilaya ya Iringa. Millinga amewataka akina baba kutokuwa na dhana ya wivu wa aina yoyote pindi wake zao watakapokuwa wakihojiwa na makarani wa Sensa kwa sababu baadhi ya maswali yatawahusu akina mama pekee. Amesema maswali hayo hayatahusiana na ndoa bali ni masuala ya uzazi na kuwataka kuwapatia uhuru na nafasi pindi watakapokuwa wanahojiwa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi.

Millinga amesema kuwa Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu sana kwa nchi kwa sababu pasipo kufahamu idadi sahihi ya watu inawezekana wananchi kupewa huduma pungufu ya mahitaj yao. Amesema Sensa hiyo itawahusisha watanzania wote na wageni watakaokuwa ndani ya nchi siku hiyo ya Sensa.
=30=

Tuesday, August 21, 2012

OLE WAO WATAKAOVURUGA SENSA IRINGA!


Serikalili Mkoani Iringa imesema kuwa haitamvumilia mtu wala kikundi chochote kitakachojitokeza na kutaka kuvuruga ama kuharibu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajia kuanza nchini kote Agosti, 26, mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika moja ya mikutano yake ya hadhara katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi uliofanyika katika kijiji cha Ilambilole, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa kila mwananchi anayo haki ya kuhesabiwa, tena kuhesabiwa mara moja. Amesema “asitokee mtu wala kikundi cha watu kuwazuia kuhesabiwa wala kuwatoza hela kwa ajili ya zoezi hili, akitokea mtu wa aina hiyo toeni taarifa kwa Serikali nasi tutamshughulikia mara moja”. Amesema kuwa zoezi hilo lipo kisheria hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kwa uhuru na pasipo hofu wala bugdha yoyote. 

Akielezea umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi hilo lina umuhimu wa kipekee kwa sababu takwimu zitakazokusanywa katika zoezi hilo zitatumika katika kutathmini utekelezaji wa mipango mikubwa ya maendeleo sambamba na utekelezaji wa malengo ya milenia 2015.  

Akiongelea mabadiliko ya Sera mbalimbali za nchi kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, Mratibu Msaidizi wa Sensa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga amesema kuwa takwimu hizo zitakazokusanywa katika Sensa ndizo zitakuwa msingi wa kubadili Sera mbalimbali zilizopo ili ziendane na hali halisi nchini. Amesema takwimu hizo pia zitasaidia katika kuainisha maeneo ya kuboreshwa kwa kufanya tafiti mbalimbali za kina kwa lengo la kupata suluhisho la matatizo yaliyopo.

Millinga amesema kuwa kuanzia alhamisi tarehe 23 mwezi huu, makarani wa Sensa wataanza kupita katika maeneo mbalimbali mkoani kukusanya taarifa za dodoso la jamii na kuomba wapewe ushirikiano. Akifafanua kuhusu dodoso la jamii, amesema kuwa dodoso hilo litajazwa ndani ya siku tatu kabla ya siku ya Sensa. Mratibu msaidizi wa Sensa Mkoa amesema kuwa dodoso hilo litakusanya taarifa mahususi zinazohusu huduma za jamii kama afya, zahanati, masoko, vituo vya afya, shule vyanzo vya maji, miundombinu na huduma a kifedha. 

Amesema katika dodoso hilo viongozi wa jamii husika ndio watahusika katika kujibu maswali ya dodoso hilo kutokana na uelewa wao mpana wa huduma zitolewazo katika eneo husika. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa yupo katika ziara ya kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012,  kukagua shughuli mbalimbali na kuhamasisha maedeleo na kuwahamasisha wananchi juu ya mchakato wa mabadiliko ya katiba mpya katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Katika siku yake ya kwanza amefanya mikutano minne ya hadhara katika vijiji vya Ilambilole, Uhominyi, Nyang’oro na Ikengeza.
=30=



Thursday, August 16, 2012




UBALOZI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WASHINGTON D.C.



UNAWALETEA  
SIKU YA MTANZANIA
Mahali: Tanzania House, 1232 22Nd Street, N.W. Washington D.C.; 20037                                   Tarehe: SEPTEMBA 15, 2012  Kiingilio: BURE                                                                                                                                                                                Muda: (Saa 4:00 asubuhi – Saa 12 Jioni)
Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani, Washington D.C. unawakaribisha Watanzania wote waishio  maeneo ya DMV (District of Columbia, Maryland na Virginia) na vitongoji vyake, kuhudhuria siku ya Mtanzania, ambapo Watanzania watashiriki kwenye kuonyesha bidhaa, tamaduni, mila na desturi za Kitanzania kwa wageni (Wamarekani na wa Mataifa mengine) watakaotembelea ubalozini.

Madhumuni makuu ya Ubalozi kuandaa Siku ya Mtanzania kwanza ni kuwaelimisha wenyeji wa Marekani kuhusu Tanzania. Pili kuitangaza zaidi Tanzania kwa kuvutia watalii wengi kutembelea Tanzania. Tatu ni kutambulisha na kutangaza biashara mbalimbali na huduma zitolewazo na Watanzania waishio hapa Marekani.

Ubalozi unaomba Watanzania wenye bidhaa mbambali za Kitanzania, mapishi (wenye leseni), vikundi vya ngoma, muziki, mitindo, na Watanzania wenye kampuni za utalii, kujiandikisha ubalozini kuanzia tarehe 1 hadi 15 Agosti, 2012 kwa maandalizi ya siku hiyo.

Kwa Watanzania watakaopenda kujitolea kushiriki siku hiyo au kuonyesha bidhaa mbalimbali wajiandikishe kwa wafuatao:
Dkt. Switbert Mkama 202 884 1087 au barua pepe smkama@tanzaniaembassy-us.org
Asia Dachi 202 884 1096 barua pepe adachi@tanzaniaembassy-us.org
Rosemary Mziray 202 884 1081 au barua pepe rmziray@tanzaniaembassy-us.org

Ubalozi unapenda kuwahamasisha Watanzania kuvaa vazi la Kitanzania.
Karibuni Wote.




EMBASSY OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA IN WASHINGTON D.C.



PROUDLY PRESENTS
TANZANIA DAY
Venue: Tanzania House, 1232 22Nd Street, N.W. Washington D.C.; 20037                                   Date: SEPTEMBER 15, 2012                                                                                                               Fee: FREE                                                                                                                                          Time: (10:00 a.m – 6:00p.m)
Have you ever climbed Mt.Kilimanjaro the highest mountain in Africa?     Have you ever been on a Safari through the Ngorongoro Crater?                                     Have you ever seen the wildebeest migration through the Serengeti Plains?                 And did you know that the 3.6 billion years old footprints of human ancestors were discovered in Laeitoli, Tanzania?
Come discover the land of Kilimanjaro and Zanzibar, wrap yourself with Swahili culture, music, food, dancing and many more in this memorable one day event packed with fun activities.
In addition to culture expose, there will also be experts on trade and investment in Tanzania, tour operators selling different Tanzanian packages and many more, ruffle drawings of interesting Tanzanian gifts.
Come one, come all, we have something for everybody!
KARIBUNI TANZANIA
MAMBO POA

Monday, August 13, 2012





 

HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA GERTRUDE K. MPAKA WAKATI WA KUFUNGA MAFUNZO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI MWAKA 2012 KWA WAANDISHI WA HABARI WA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI PAMOJA NA MIKOA YA LINDI NA MTWARA YALIYOFANYIKA CHUO KIKUU RUAHA IRINGA,  TAREHE 13 AGOSTI, 2012


Ndugu Mwenyekiti,
Mratibu wa Mratibu wa Sensa Mkoa,
Watendaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Watendaji kutoka Sekretarieti ya Mkoa,
Ndugu Washiriki wa Mafunzo,
Mabibi na Mabwana,


Ndugu Mwenyekiti,kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa na kuhudhuria mafunzo haya hadi kufikia hatua ya mwisho yaani hatua ya kumaliza.  Aidha nachukua fursa hii kuwashukuru sana washiriki wote kwa kuheshimu mwaliko wa kuhudhuria mafunzo haya muhimu ambayo yalihusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na nafasi ya vyombo vya habari katika kufanikisha zoezi hilo.

Ndugu Mwenyekiti, nilipopata mwaliko kuwa Mgeni Rasmi kufunga mafunzo haya kwanza nilifurahi kwa kuwa niliona nimepata fursa ya pekee kukutana na kundi kubwa la waandishi wa habari kwa pamoja kitu ambacho ni nadra kutokea katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku. Pili nimefarijika na mwaliko wenu kwa kuwa utanipa fursa ya kuchangia mawazo katika baadhi ya maeneo ambayo yamezungumziwa katika mafunzo haya.

Ndugu Mwenyekiti, mafunzo haya nimeelezwa kuwa yamezungumzia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi iliyopangwa kufanyika tarehe 26 Agosti, 2012. Nimeelezwa kuwa jumla ya mada tano ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa kina ambapo pia washiriki walipata fursa ya kufanya mazoezi kwa vitendo kwa baadhi ya mada walizojifunza.

Kwa ujumla nimeelezwa kuwa mada zote ziliibua majadiliano na hoja mbali mbali pamoja na changamoto za hapa na pale lakini jambo muhimu ni kuwa lengo la majadiliano hayo yalilenga katika kujifunza zaidi na kuongeza ufahamu kwa kila mshiriki juu ya masuala ya msingi kuhusu Sensa. Mimi naamini kuwa wataalamu wetu hapa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu wamejitahidi kadri ya utaalamu wao na uwezo waliojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuyafafanua kinagaubaga masuala yote yanayohusu Sensa ambayo yalihitaji maelezo ya ziada ya yale yaliyowasilishwa. Mbali ya maelezo ya wataalamu nimeelezwa kuwa mmepatiwa nyaraka muhimu zenye kueleza na kufafanua masuala ya msingi ya Sensa. Nyaraka hizo zitawasaidia kuongeza ufahamu wenu kuhusu suala zima la Sensa.

Ndugu Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo ninaamini kuwa ndugu washiriki mmefaidika na maelezo hayo na sasa mmekamilika katika suala zima linalohusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Maana yake ni kuwa sio tu mko katika nafasi nzuri ya kuandika na kutangaza kwa usahihi habari za Sensa lakini pia mafunzo haya yatakuwa yamewatia shime na ari ya kushiriki katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012. Matarajio yetu basi ni kuona taarifa zaidi za Sensa hasa zile za kuhamasisha wananchi kushiriki zinatolewa mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini na hususan vyombo vyetu vilivyomo katika mikoa ya kanda yetu.

Ndugu Mwenyekiti, nafasi niliyopewa ni kuyafunga mafunzo haya lakini kabla ya kufanya hivyo ningependa kusisitiza mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la ushirikiano. Waswahili tuna msemo usemao ‘kidole kimoja hakivunji chawa’. Kama ilivyoelezwa na wataalamu, mafanikio ya Sensa yanategemea sana ushiriki na ushirikishwaji wa kila mdau katika nchi. Kwa maana hiyo ni ukweli usiopingika kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikisha Sensa kwa sababu mchakato wake ni mkubwa unaohitaji ushiriki wa wadau wa kila aina na kutoka sekta mbalimbali. Miongoni mwa wadau hao ni vyombo vya habari.

Hivi sasa nchi yetu inajivunia utajiri mkubwa wa vyombo vya habari ambavyo ni matokeo ya mabadiliko ya sheria ya umiliki wa vyombo habari iliyopitishwa na Serikali. Dhamira ya Serikali kufanya marekebisho hayo ni kuwapa fursa zaidi watanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa kwa kuamini kuwa vyombo hivi vitatumika kuwaendeleza wananchi kwa kuwaelimisha, kuwahabarisha na kuwaburudisha.

Historia ya nchi yetu inaonyesha kuwa vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Serikali sio tu katika kuboresha hali ya maisha ya kila mwananchi bali pia katika kuimarisha uzalendo na mshikamano miongoni mwa wananchi. Hivyo, wito wa Serikali kwa vyombo vya habari ni kuviomba viendeleze ushirikiano na mshikamano wa watanzania kama vinavyovyofanya katika masuala mengine yenye maslahi na Taifa letu ili kufanikisha Sensa.   

Ndugu Mwenyekiti, naelewa kuwa Serikali haina shaka hata kidogo kuhusu uwezo wa vyombo vya habari katika kulieleza jambo hili kwa usahihi kwani mnalifahamu na kwa mafunzo na uzoefu mlionao nyinyi ni walimu na wasemaji wazuri hivyo tumieni ujuzi na uwezo wenu huo kuwaeleza wananchi kwa ufasaha kuwa Sensa ni muhimu kwao na kwa Taifa lao hivyo wasisite kushiriki. Kwa hiyo, matarajio ya Serikali ni kuona kuwa mnakuwa waelimishaji wazuri na wahamasishaji makini wa Sensa ili kila mwananchi kwa hiari yake aone kuwa ana wajibu wa kuhakikisha anahesabiwa na anahesabiwa mara moja tu.

Ndugu Mweneykiti,
Jambo la pili ni suala la kutoa taarifa sahihi na kwa wakati. Leo zimebaki siku 12 tu kufika siku ya Sensa tarehe 26 Agosti 2012. Hivyo vyombo vya habari na wasemaji wote wa Sensa hawana budi kuepuka kufanya makosa katika uhamasishaji na zaidi walenge katika mambo muhimu ambayo mwananchi anapaswa kuyafahamu. Mambo hayo aliyaeleza Mkuu wa Mkoa wakati alipofungua mafunzo haya nami sina budi kuyarudia ili kuweka msisitizo.

1.0      Kuwa Sensa ya Watu na Makazi itafanyika tarehe 26 Agosti, 2012.
2.0      Watakaohesabiwa ni wale tu watakaokuwa nchini usiku wa Jumamosi tarehe 25 Agosti kuamkia Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012.
3.0      Watakaohesabiwa katika Kaya ni wale watakaokuwa wamelala katika Kaya usiku wa kuamkia Siku ya Sensa ambao, kama nilivyoeleza awali, ni usiku wa Jumamosi ya tarehe 25 Agosti, 2012 kuamkia Jumapili terehe 26 Agosti, 2012 pamoja na wanakaya wanaofanya kazi za usiku ambao kwa usiku ule hawakulala kwenye Kaya.  Hawa ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya, ulinzi na usalama na hata sekta ya habari.
4.0      Ni muhimu Mkuu wa Kaya akaweka kumbukumbu sahihi za watu wake wote zikiwemo za umri,kiwango cha elimu, ajira anayofanya, mahali anaposhinda mwanakaya wakati wa mchana na kwa wanawake hali zao za uzazi.

Ndugu Mwenyekiti, mwisho, ningependa kueleza furaha yangu kwa washiriki wote kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa na uvumilivu wakati wote wa mafunzo. Ushirikiano na uvumilivu wenu huo ulikuwa muhimu katika kufanikisha mafunzo haya hadi sasa tunayafunga rasmi. Nichukue fursa hii kuwatakia safari njema wageni wetu wote kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na wenzetu kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara.

Baada ya kusema hayo naomba sasa nitamke kuwa Mafunzo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa waandishi wa habari wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja mikoa ya Lindi na Mtwara yamefungwa rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza
 
SENSA KWA MAENDELEO: JIANDAE KUHESABIWA